DAR ES SALAAM
NA CLEMENT MAGEMBE
Wafanyakazi wa Kampuni ya Mikopo ya Platinum Credit Ltd Tanzania
wamelalamikia kitendo cha kampuni hiyo kuwatoza wateja wake riba
kubwa na kushinikiza taasisi za umma kuingia katika mikataba ya
mikopo kwa rushwa.
Wafanyakazi hao ambao hawakutaka majina yao kuandikwa
wamelieleza JAMHURI kuwa Kampuni ya Platinum inatoza riba kubwa
ya mikopo tofauti na taasisi nyingine za kifedha hapa nchini.
Wamesema wao kama maofisa masoko inawawia vigumu kuingia
mikataba na taasisi mbalimbali za umma ambazo ndiyo wateja wao
wakubwa kutokana na ugumu wa mikataba iliyopo na viwango vikubwa
vya riba, tofauti na kampuni nyingine za mikopo.
“Mtu anayekopa Sh milioni 10 analipa riba ya asilimia 3.75 kwa miezi 60
ambayo inakuwa Sh milioni 22.5, hivyo pamoja na mkopo wake analipa
zaidi ya Sh milioni 32.
“Huu ni wizi wa wazi wazi kwa Watanzania, tumewaeleza viongozi lakini
hawataki kupunguza kiasi hicho cha riba na badala yake wanatumia
rushwa kuingia mikataba na taasisi hizo za umma,” wamesema.
Wamesema taasisi zote za umma ambazo wameingia nazo mkataba,
awali waligoma kusaini kwa madai kuwa masharti ni magumu mno na
wanaporudisha taarifa viongozi wa kampuni hiyo wanawapa rushwa
maofisa utumishi na wanasheria wa taasisi hizo ambao wanaipitisha
bila kuwajulisha watumishi wa ngazi za chini.
Taasisi za umma ambazo zimeingia mikataba ya mikopo na kampuni
hiyo ni Jeshi la Polisi, Magereza, Tamisemi, vyuo vikuu vya umma
isipokuwa Chuo Kikuu Cha Ardhi ambacho kilikataa kuingia mkataba na
kampuni hiyo baada ya kutokubaliana na masharti yaliyoainishwa.
Wamesema wao kama mawakala wa kampuni hiyo wenye jukumu la
kutafuta masoko, kinachowashangaza ni kuona baadhi ya watumishi
kupewa mikopo bila mkataba na kampuni hiyo.

Wamesema kigezo kinachotumika cha kutoa mikopo kwa haraka ndiyo
kimekuwa chambo cha kuwanasa watumishi wengi wa umma
wakiwamo wasomi bila kuelewa kwamba wanalipa riba mara mbili zaidi
ya mikopo wanayokopeshwa.
Pamoja na hayo wafanyakazi hao wamesema wanawatafuta wateja
maeneo ya mijini na vijijini nchi nzima kwa gharama zao wenyewe huku
wakiambulia asilimia 5 tu kama sehemu ya malipo (udalali) kwa kila
mteja anayepatikana.
“Kinachotushangaza ni kukatwa tena michango ya NSSF kutoka katika
malipo hayo, lakini mwajiri hazifikishi fedha zetu katika mfuko huo,”
amesema mmoja wa wafanyakazi hao.
Wamesema ni makosa kisheria mwajiri kukata michango ya
wafanyakazi kutoka katika mapato yaliyo nje ya mishahara yao lakini
bado wao wameendeleza utaratibu huo.
Mteja ang’aka
Fredy Kibaibai aliyekopeshwa mkopo wa Sh milioni 3, ambao unadumu
kwa kipindi cha mwaka mmoja ameulalamikia uongozi wa kampuni
hiyo kukamata gari lake, Toyota RAV 4 lenye namba za usajili T 123
DAP aliloliweka kama dhamana ya mkopo.
Kibaibai amelieleza JAMHURI kuwa tangu alipokopeshwa mkopo huo
Oktoba mwaka jana alitakiwa kulipa Sh 460,000 kila mwezi kuanzia
mwezi Novemba hadi Oktoba mwaka huu na amelipa kwa miezi minne
isipokuwa Februari hakuweza kufanya marejesho yoyote kutokana na
matatizo yaliyokuwa yanamkabili.
Amesema kwa kipindi cha miezi mitano alitakiwa kurejesha Sh milioni 2.
3 lakini kutokana na matatizo aliyokuwa nayo alirejesha Sh milioni 1.48
kwa miezi minne ndipo kampuni hiyo ikaamua kukamata gari lake
kupitia kampuni ya udalali.
“Hawa jamaa siwaelewi kabisa, kwani bado sijamaliza mkataba nao
ambao unakamilika Oktoba mwaka huu na kadi ya gari wanayo, kitendo
cha kukamata gari langu hakina nia njema.
“Wamekamata gari langu likiwa barabarani wakati bado ni mteja wao
huku wakidai fedha zinazozidi milioni 9 ikiwa mara tatu ya mkopo
walionipa,” amesema Kibaibai.
Amesema pamoja na kuwaomba kwamba atalipa malimbikizo hayo yote
wakati akiendelea na mkataba wake, bado uongozi wa Kampuni ya
Platinum umeendelea kulishikilia gari lake huku akitakiwa kulipa

gharama zote za matunzo ya gari hilo.
Platinum wazungumza
JAMHURI limezungumza na uongozi wa kampuni ya Platinum Credit
Ltd, ambayo imeyakana malalamiko hayo na kwamba yana nia isiyo
njema kwa kampuni hiyo.
Meneja Rasilimali Watu na Utawala wa Kampuni hiyo, Ladislaus
Mwongerezi, amesema katika kampuni hiyo hakuna mtumishi yeyote
ambaye anafanya kazi bila kuwa na mkataba.
Amesema kila mmoja amepewa mkataba kulingana na makubaliano na
mwajiri, huku wale walio katika timu ya mauzo ambayo imepewa
malengo yake na wanapouza zaidi hulipwa sawa na kazi yao.
“Wewe siyo wa kwanza kuja kuhoji masuala mbalimbali
yanayolalamikiwa katika kampuni hii, mwaka jana walifika waandishi
sita kutoka kutoka vyombo vya habari kadhaa hapa nchini kuhoji
maswali haya haya.
“Kutokana na masharti ya kulipwa mshahara (Basic salary)
wanaolalamika ni wale ambao hawatekelezi majukumu yao sawa na
malengo tuliyokubaliana,” amesema Mwongerezi.
Amesema kwa kawaida akisaini mikataba ya wafanyakazi hao
inarudishwa kwa mameneja wa matawi ambao wanapaswa kuwapa
nakala watumishi hao na iwapo hawafanyi hivyo ni kosa.
Mwongerezi amesema mwaka 2016 aliwasainisha mikataba watumishi
wote wa kampuni hiyo na kuihuisha tena mwaka jana ambayo bado
inatumika hadi sasa.
Pamoja na hayo, amekiri kwamba awali kulikuwa na utaratibu wa
kukata michango ya NSSF kutoka katika malipo yao nje mishahara yao.
Amesema Juni mwaka jana walisitisha makato ya michango ya
wafanyakazi hao kupitia fedha za udalali baada ya kutafuta masoko,
kwani ilikuwa ni kinyume cha sheria na kwamba wale waliohitaji
kuendelea na utaratibu huo kwa hiari yao wenyewe wanafanya hivyo.
Hata hivyo, amesema kampuni hiyo kwa sasa ina wafanyakazi katika
vitengo mbalimbali nchini wanaofikia 510 huku mfanyakazi wa kigeni
akiwa mmoja tu kutoka nchi ya Kenya ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji.
Kuhusu riba
Amekiri kuwa baadhi ya wateja wamekuwa wakilalamika kuwa riba ni

kubwa hivyo hawawezi kuwalazimisha kuingia katika mikataba nao
tofauti na madai yaliyotolewa na wananchi hao.
Amesema madhumuni ya kampuni hiyo ni kutoa mikopo ya kibiashara
kwa mujibu wa sheria zilizoidhinishwa na Wizara ya Viwanda na
Biashara na masharti ya leseni.
“Sisi tunakopa fedha kutoka benki ambazo tunazizungusha kwa
kuzikopesha kwa wateja wetu kwa lengo la kufanyia biashara, hii ni
biashara huria.
“Tunatangaza bidhaa zetu kwa wateja wetu zikiwamo taasisi za umma
na watu binafsi na mteja akivutiwa tunaingia naye mkataba bila
kumlazimisha,” amesema.
Pia amekana madai ya kushinikiza mikataba katika taasisi za umma
kwa kuwapa rushwa baadhi ya maofisa wa Serikali na kwamba
wanazingatia taratibu zote zinazohitajika.
Amesema mikopo kwa watumishi wa Serikali, dhamana ni makato
kupitia katika mshahara wa mtumishi na watu binafsi dhamana ni gari
analomiliki ambalo ni lazima lithaminiwe kabla ya kukopa.
Amesema iwapo mtu ameshindwa kurejesha mkopo wake kulingana na
masharti waliyokubaliana, inampasa kutoa taarifa ndani ya siku 14
kuomba upya utaratibu wa urejeshaji wa deni lake na asipofanya hivyo
anatozwa faini ya Sh. 40,000.