Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Dodoma

WAZIRI Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda, amewataka wafanyabiashara nchini kuwa waadilifu na kujiepusha na kuchakachua bidhaa kwa kuwa inachangia kushusha ubora.

Pinda ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa Kongamano la Uongozi na biashara lililoandaliwa na Taasisi ya Kingdom Leadership Network Tanzania (KLNT).

Pinda amesema kuwa kuna wafanyabiashara kwa tamaa zao za kujipatia fedha kwa urahisi hukosa uadilifu na kuchakachua bidhaa hali inayosababisha kukosa ubora na kuharibu soko.

“Uadilifu katika biashara ni muhimu na kujiepusha kuchakachua bidhaa ili kupata fedha kwa urahisi, pia tunakutegemea uchangie serikalini ulipe kodi na ushuru unaotakiwa wewe ndio wa kwanza kukwepa, halafu unasema mimi mjasiriamali mzuri wewe sio mzuri,”amesema.

Hata hivyo amesema kuwa viongozi wa serikali wana wajibu wa kuwajibika kusaidia wafanyabiashara na wajasiriamali ili wafanye vizuri kwenye shughuli zao.

“Sisi ndio tumewaweka mtuongoze, sisi wafanyabiashara wadogo ndio tumewaweka mtuongoze, ni lazima ukitoka hapa useme nitafanya juu na chini kuwasaidia wajasiriamali wadogo wafanye vizuri kwenye shughuli zao, kama hujali wewe sio kiongozi mzuri” amesema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Balozi Ombeni Sefue, ameipongeza taasisi hiyo kwa kuandaa program za kujenga vijana na wajasiriamali kwenye misingi ya uadilifu na ujasiriamali.

“Haitoshi kila mtu kulalamika hakuna ajira na hakuna wa kutengeneza ajira, nchi haiwezi kwenda mbali lakini lazima kuwapa vijana ujuzi wanaohitaji ili kuanzisha biashara vizuri inavyopaswa na sio kukurupuka, kile unachotaka kufanya kipime kwa vigezo,”amesema.

Awali,Meya wa Jiji la Dodoma, Prof.Davis Mwamfupe,amesema katika mabadiliko ya kidunia lazima kuwe na viongozi ambao wameandaliwa vyema.

“Mkutano huu unalenga kusisitiza katika hali ya kubadilika lazima uwaandae viongozi na maandalizi ya hao viongozi iwe wajasiriamali, kuna umuhimu wa kuandaa viongozi wafuate zile kanuni za msingi katika utawala, watende haki wawe na uwazi,”ameeleza.