Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alipewa taarifa zinazoaminika kuwa alidanganywa na Afisa Kilimo wa Wilaya ya Geita, kuhusu utekelezaji wa mradi wa umwagiliaji katika vijiji viwili vya Nyamboge na Nzela wilayani hapa.
Wakati huo huo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) walipigwa chenga na watumishi wa Idara ya Kilimo kuhusu matunizi ya Sh milioni 200 zilizotolewa na Serikali kugharamia mradi huo.
Pinda alifanya ziara mkoani Geita Septemba 2012. Akiwa wilayani Geita alisomewa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo zinazogharamiwa Serikali.
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Manzie Mangochie, wakati akisoma taarifa ya wilaya hiyo, Pinda alitaka kufahamu wilaya hiyo imetekeleza namna gani Programu ya Uwezeshaji Kilimo ya Wilaya (DASIP), hasa kilimo cha umwagiliaji.
Mkuu wa Wilaya alimtaka Afisa Kilimo wa wilaya hiyo atoe ufafanuzi kuhusu miradi ya DASIP ya umwagiliaji iliyotekelezwa wilayani.
Afisa Kilimo, Peter Mutagwaba, alimweleza Waziri Mkuu; “Tulipokea shilingi milioni 200 kutoka DASIP kwa ajili ya skimu ya umwagiliaji ya Nyamboge-Nzela, tulitumia shilingi milioni 130 kufanya upembuzi yakinifu na zikabaki milioni 70 ambazo zitatumika kujenga ghala la kuhifadhi mazao katika Kijiji cha Nyamboge.”
Pinda alilazimika kuhoji matumizi hayo na kuonesha wasiwasi kwa idara hiyo kutumia pesa nyingi kwenye upembuzi yakinifu.
“Hivi hamna huruma jamani? Pesa zote hizo mmezitumia kwenye upembuzi yakinifu peke yake jamani?” Alihoji.
Wakati Pinda akiambiwa kuwa Sh milioni 70 zitapelekwa Nyamboge kujenga ghala la kuhifadhi mazao, uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa kiasi kilichopelekwa kijijini humo ni Sh milioni 40.
Afisa Kilimo alipoulizwa alikuwa na nia gani kutoa taarifa isiyo sahihi kwa Waziri Mkuu kuwa atajenga ghala kwa Sh milioni 70 lakini akapeleka Sh milioni 40 kijijini, na Sh milioni 30 zilizobaki zitatumika kufanya kazi gani, alisema pesa hizo zote zimeshatumika kuandika andiko la mradi wa skimu kuomba pesa kutoka ASDP Sh bilioni 1.8 za kugharamia ujenzi wa skimu ya umwagiliaji ya Nyamboge-Nzela.
Mkuu wa Wilaya alipoulizwa kuhusu kutoa taarifa ya isiyo ya kweli kwa Waziri Mkuu kuhusu Sh milioni 70 kujenga ghala wakati wakulima wamepelekewa Sh milioni 40 ambazo hazitoshi kukamilisha ujenzi wa ghala hilo, alisema:
“Hakuna aliyemdanganya Waziri Mkuu, ila mimi siyo mtaalamu wa kilimo, ngoja nimwite Afisa Kilimo akupe majibu sahihi, maana hata Rais hawezi kujua miradi yote.”
Afisa Kilimo wa Wilaya akiwa mbele ya Mkuu wa Wilaya, alimwambia mwandishi:
“Zile milioni 40 tulizopeleka Nyamboge kijijini zimepatikana sehemu nyingine tofauti na zile milioni 70 tulizomwambia Waziri Mkuu zilizosalia kwenye skimu, milioni 70 bado zipo zote benki hazijatumika popote.”
Alipoulizwa kuhusu maelezo aliyoyatoa kwa Waziri Mkuu kuwa Sh milioni 70 zilizobaki kwenye upembuzi wa skimu zitajenga ghala lakini anasema amepeleka pesa nyingine, kama siyo kumdanganya kiongozi huyo na kitendo hicho kuchukuliwa kama kuficha matumizi mabaya ya fedha hizo, alijibu kwa kulalamikia mwandishi kuwa anatumiwa na watu kumfuatilia ofisa huyo.
“Mkuu wa Wilaya, bahati nzuri tumeshajua huyu jamaa anatumwa na nani, hivyo mwache waandike tutajieleza mbele kwa mbele maana haya mambo ni ya muda mrefu sasa sijui huu ni uandishi wa aina ipi wa kufuatilia mambo ya muda wote huo kama hatumiki,” alijibu Mutagwaba.
Mkuu wa Wilaya alipoelezwa kuwa ujenzi wa ghala hilo umejengwa chini ya kiwango, msingi na jamvi la ghala hilo limepasuka na mkandarasi ameagizwa na Mhandisi wa Wilaya abomoe ajenge upya lakini mkandarasi hajatii agizo hilo, na wakulima hawana sehemu ya kuhifadhi mazao kwa mwaka huu, alisema:
“Hiyo siyo kazi ya Mkuu wa Wilaya, hata Afisa Kilimo hahusiki na hilo tatizo lako, unahisi Afisa Kilimo amekula fedha huko Halmashauri.”
Wakati Afisa Kilimo akisema Sh milioni 70 bado ziko benki zote zilizobaki kwenye upembuzi wa skimu, gazeti hili limebahatika kuona nyaraka inayoonesha maelezo ya benki iliyotolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo mwaka 2012, kuhusu akaunti ya DASIP ikionesha pesa zilizokuwa zimesalia benki kwenye akaunti namba 31001200034 kuwa ni 59,663,349.30 na siyo Sh milioni 70 kama alivyosema Afisa Kilimo.
Wakati Afisa Kilimo huyo akitoa kauli mbili tofauti kwa mwandishi wa habari kuhusu matumizi ya Sh milioni 70, Kamanda wa Takukuru Wilaya ya Geita, Suzan Mwende, alisema waliwahi kupata malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu matumizi ya kutia shaka ya pesa za mradi wa skimu ya Nyamboge-Nzela.
“Tulipokea malalamiko kutoka kwa wananchi, tulianza kuchunguza lakini watumishi wa halmashauri idara ya kilimo walitwambia tatizo lilikuwa kwa wananchi, kwamba hawajui dhana ya upembuzi yakinifu, lakini mpaka hapo naona kuna haja ya kuanza kufanya uchunguzi mpya.
“Hatukujua kama kuna mambo mengi kama hayo ya taarifa za halmashauri kutofautiana kwenye nyaraka zake kwa mradi mmoja na takwimu za pesa kutofautiana, lazima tufungue jalada la uchunguzi na ninaomba tutakapoomba msaada wa mambo fulani uwe tayari kutoa ushirikiano.
“Sisi tuliambiwa eti upembuzi unagharimu pesa nyingi na wananchi wanalalamika kwa sababu hawaelewi upembuzi, tulikubaliana nao na hatukuendelea mbele zaidi ya hapo, sasa tutafuatilia kuanzia skimu pamoja na hilo ghala na baadaye tutatoa taarifa,” alisema Mwende.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Elisha Lupuga, alipotakiwa kufafanua kuhusu baraza la madiwani kubariki na kupitisha matumizi makubwa ya kufanya upembuzi yakinifu peke yake huku takwimu za matumizi hayo zikiwa na mashaka makubwa, alisema:
“Hata hivyo, wale jamaa ni wazalendo kweli maana walibakiza hata hizo milioni 70, hata hivyo hoja ya matumizi ya pesa hizo iliwahi kuhojiwa na Musukuma (Joseph Musukuma) lakini huyo bwana hajui maana ya upembuzi yakinifu na anapenda sana kufuatilia mambo ya wengine lakini wewe ukifuatilia mambo yake anakuwa mkali sana.”
Mwenyekiti huyo alitoa shutuma hizo kuelekeza kwa Musukuma huku kukiwa na muda mfupi tangu baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kumfukuza uenyekiti wa baraza hilo kwa tuhuma mbalimbali.
Naye Musukuma alipotafutwa kwa njia ya simu hakupokea simu, na alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi wa simu hakujibu.
Wilaya ya Geita imepata hati zenye mashaka kwa miaka mitatu mfululizo katika taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika ukaguzi wa 2009/2010, 2010/2011 na 2011/2012 na kubaini upotevu wa mamilioni ya shilingi katika miradi ya maendeleo ambapo Juni 2012 Takukuru iliwafikisha mahakamani kwa ubadhirifu watumishi watano wa halmashauri hiyo.
Waliofikishwa mahakamani ni Benson Tatala, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo; Frank Maganga (Mhasibu); Omary Dienga (Mganga Mkuu); Abdallah Zihila na Joseph Onditi wakituhumiwa kukwapua mamilioni ya shilingi yaliyotolewa kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa zahanati katika wilaya hiyo.