Miaka kadhaa iliyopita, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, aliwaita wahariri wa vyombo vya habari ofisini kwake, Dar es Salaam. Akazungumza mambo mengi.
Nilipata bahati ya kualikwa, na ya kumuuliza swali. Swali langu, ukiacha ule mgogoro alioshindwa kuutatua- mgogoro wa ardhi Kwembe-Kati, lilihusu ukwasi alionao. Akatoa maelezo marefu kwa kusema ana nyumba za kawaida- Pugu, Dar es Salaam na Kibaoni, Katavi.
Kwenye fedha, akasema akikusanya fedha kwenye akaunti zake zote, haziwezi kuzidi Sh milioni 20 au 25 hivi. Jibu hilo likawa gumzo. Wapo waliomsifu kwa “uadilifu” wake, lakini wengine wakamkosoa kwa kusema umaskini si sifa ya kiongozi. Sijui, lakini lililokuwa muhimu kwa kiongozi, hasa muumini aina ya Mheshimiwa Pinda, nadhani ni “kiasi” kama inavyozungumzwa kwenye Biblia.
Kwenye mkutano huo, kwa kuwa aliwapa fursa wanahabari kumuuliza maswali mengi kadri wapendavyo, akaulizwa swali jingine la kama ana nia ya kuwania urais mwaka 2015. Akajibu kuwa asingependa kushika wadhifa huo mkubwa. Hoja yake ilikuwa kwamba urais ni kazi ngumu mno. Akasema anamhurumia “Mzee Kikwete” (alitumia maneno hayo) kwa kazi hiyo ngumu; kwa hiyo yeye asingependa kubebea mzigo huo.
Majibu ya Mheshimiwa Pinda kwa wakati huo pengine yalisababishwa na uchanga wake kwenye nafasi hiyo ya Uwaziri Mkuu. Kadri muda ulivyosonga mbele, nadhani Pinda akaanza kuonyesha uhalisia wake. Akanogewa. Zikawapo fununu mitaani za yeye kuwa miongoni mwa wanaoutaka urais. Hatimaye mwaka jana akakata mzizi wa fitna. Akatumia fursa aliyopewa na Idhaa ya Kiswahili ya BBC London, kutamka wazi kuwa nautamani urais.
Mwishoni mwa wiki alipotangaza rasmi kuwania nafasi hiyo, nilitarajia ndugu zangu wanahabari wangemuuliza uki-geugeu wake. Hawakufanya hivyo. Hawakufanya hivyo, ama kwa kuogopa, au kwa sababu wameshasahau. Tatizo moja kubwa linalotukabili wanahabari sasa ni usahaulifu. Kama ningeshirikishwa kwenye mkutano huo, ningemuuliza kwa nini wakati ule aliiona kazi ya urais kuwa ni ngumu na hata akasema haitamani, lakini sasa kaiona nyepesi kiasi kwamba anaitaka.
Sitaki kuingia kwenye maneno ya mitaani ya kwamba utitiri huu wa wanaoutaka urais ni kutokana na rais wetu wa sasa kuifanya kazi hii kuonekana nyepesi hata kuwafanya wakulima wa kawaida kabisa nao kujitokeza kuitaka.
Inawezekana Mheshimiwa Pinda amebadili mawazo kwa sababu ameona kama Mheshimiwa Kikwete kauweza urais kwa miaka 10, ni kwa nini yeye ashindwe. Wapo wanaodai kwamba Mheshimiwa Kikwete kaifanya kazi ya urais ionekane nyepesi kuliko wengi walivyodhani.
Lakini inawezekana ni kwa sababu naye anataka apate fursa njema ya kusafiri huku na kule ughaibuni ili walau wajukuu zake wawe na rekodi ya kujivunia iliyofikiwa na babu yao! Lakini inawezekana uamuzi wa Mheshimiwa Pinda umetokana na stress anazopata kila anapowaza adha za foleni atakazopambana nazo akiwa nje ya madaraka; ambazo kimsingi alipaswa kuzimaliza au kuzipunguza kwa miaka yake minane, lakini hakufanya hivyo.
Mwisho, inawezekana ndio kule kukamilisha ule msemo wa mlamba asali kanogewa, na sasa anataka kuchonga mzinga! Ukichanganya hayo na mengine ya ushauri kutoka kwa wanafamilia na wapambe wengine wanaomzunguka, unafikia hitimisho la kwa nini atautaka urais.
Sina namna yoyote ya kumwezesha wala kumkwaza Mheshimiwa Pinda kufikia matamanio yake ya urais. Sina kura ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Sina jukwaa pana na refu la kuwahamasisha wana CCM wamnyime au wampe heshima hiyo. Lakini kwa kuwa ameshaonyesha dalili za kunifanya mimi niwe sehemu ya Watanzania wakaoweza kumwita “mheshimiwa rais”, nimeona nina wajibu wa kumjadili japo kidogo.
Mheshimiwa Pinda, angepumzika tu. Ushauri huu ni mgumu. Rafiki yangu, Leonard Derefa aliyepata kuwa Mbunge wa Shinyanga Mjini, alipata kunieleza kwamba kuwa mwanasiasa ni sawa na kula nyama ya mtu. Ukiizoea, huiachi. Akasema mtu akishaingia mwenye siasa, inakuwa vigumu sana kuiacha. Akatoa mfano kwamba ndio maana wanasiasa wengi wako radhi wafilisike hata kama wanajua wapigakura hawapo upande wao. Hili lipo kwa Mheshimiwa Pinda.
Miaka minane na zaidi akiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Pinda, hana jambo madhubuti la kuweza kujivunia alilowafanyia Watanzania. Hajatueleza kwanini kashindwa akiwa Waziri Mkuu, na sasa ataweza akiwa rais. Lakini kauli yake siku ile pale bungeni alipowajibu wabunge kuhusu David Jairo, aliposema “kama ningekuwa na mamlaka”, anaweza kuitumia kuhalalisha kwamba kwenye Uwaziri Mkuu wake alikwazwa na nguvu iliyokuwa juu yake, yaani Rais. Kwa sababu hiyo, anataka kusema kama akiwa rais, basi Watanzania watarajie kuona umahiri wake! Sijui.
Aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, Jaji Joseph Warioba, wakati wa Awamu ya Pili, alipoona mambo hayaendi vema, alitangaza kujiuzulu. Kuna habari kwamba Rais Ali Hassan Mwinyi, alimgomea, lakini baadaye ikaonekana Jaji Warioba alikuwa na hoja. Nayo ilikuwa kwamba kama mawaziri wake walikuwa wazembe na wasiowajibika vilivyo, mzigo wa lawama ulikuwa kwake yeye. Akajiuzulu. Baraza la Mawaziri likavunjika.
Kuna mambo mengine ambayo Mheshimiwa Pinda alipaswa kuona hayaendi kwa sababu, ama anakwazwa na Rais, au mawaziri wake. Kwa hatua hiyo, alipaswa kujiuzulu. Pinda hajawahi kuwa na wazo la aina hiyo. Hata alipohusishwa moja kwa moja kwenye kashfa za Tokomeza na Escrow, bado aliendelea kuwa mbali na msamiati wa “kujiuzulu”.
Yalipotokea mauaji ya albino, heshima kubwa aliyowapa walemavu hao ni kumwaga chozi bungeni. Akaishia hapo. Mauaji yameendelea wakati wake wote. Kwa sababu sasa anautaka urais, nadhani ndiyo maana ameonyesha dhamira kidogo ya kukabiliana na uharamia huo.
Mheshimiwa Pinda kila alipobanwa bungeni kutokana na uzembe wake au wa Serikali ambayo yeye ndiye mtendaji mkuu wa kila siku, alimwaga chozi na kutumia lugha ya “chonde chonde”. Alipoona staili hiyo imeshazoeleka, akaibuka na kauli kali ya “wapigwe tu”. Kweli, tumeshuhudia watu, si tu polisi wanavyowapiga raia, bali wanavyouawa kwa risasi.
Mheshimiwa Pinda, akiwa Waziri Mkuu ameshindwa kusimamia na kutekeleza agizo la Rais la kuhakikisha kila shule ya sekondari inakuwa na maabara. Agizo la mwaka 2012 hadi leo 2015 halijakamilika. Je, anataka awe rais ndipo akamilishe kazi hiyo?
Mheshimiwa Pinda, aliingia kwenye mzozo na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, kwa sababu tu waziri huyo aliamua kusimamia sheria ya uzito unaostahili kwa malori. Waziri alikuwa na nia njema kisheria ya kulinda barabara zinazojengwa kwa fedha za Watanzania. Pinda akamzuia kabisa. Matokeo yake tunaona hali ya barabara ilivyo mbaya. Huyu akiwa rais hawezi kuwa na wazo la kuboresha wala kujenga reli!
Alimzuia Dk. Magufuli kuwaondoa wavamizi wa hifadhi ya barabara. Hata pale makandarasi walipopewa fedha kuanza kazi, wavamizi walikaidi kuhama kwa maelekezo ya Waziri Mkuu.
Nchi yetu ilipofika inamhitaji rais asiyeonea haya kusimamia sheria. Hatuhitaji kuwa na rais ambaye kila mtu anakuwa na changuo la kufuata, au kutofuata sheria. Tunamtaka rais wa kuhakikisha organ zote za Serikali zinafanya kazi kwa mujibu wa sheria, na hiyo kazi ionekane. Haki za binadamu si kuruhusu watu kufanya wanachotaka. Wala demokrasia haisemi mtu anayetaka kufuata sheria, afuate; na asiyetaka aache! Hakuna kitu cha aina hiyo.
Mheshimiwa Pinda, ameonyesha udhaifu mkubwa kwa kuruhusu kufutwa kazi kwa mawaziri mahiri kabisa. Hadi sasa sijapata sababu za msingi za kufukuzwa kwa Profesa Sospeter Muhongo. Mheshimiwa Pinda alikuwa dhaifu wakati wote wa mjadala wa Escrow kiasi kwamba akakosa uwezo kabisa wa kuwaokoa mawaziri.
Chini ya uongozi wake amewapoteza mawaziri kama Balozi Khamis Kagasheki, badala yake Wizara nyeti ya Maliasili na Utalii amepewa mtu dhaifu na mhujumu uchumi anayevunja sheria wazi wazi. Kila siku magazeti yanaanika uoza wa waziri huyu, lakini Waziri Mkuu hana habari kabisa. Leo Pinda na Nyalandu wanautaka urais! Hivi kweli tumeishiwa watu makini wa kutuongoza? Endapo hata walioshindwa kazi sasa wanautaka urais, nani atasita kutangaza nia?
Kwenye Operesheni Tokomeza kuna maneno kwamba Mheshimiwa Pinda alipelekewa taarifa mara kadhaa na mawaziri wake, hasa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, ili operesheni hiyo isimamishwe. Alifanya hivyo kwa sababu ile operesheni ilikuwa ya kijeshi hivyo ilikuwa juu ya mamlaka ya waziri wa kawaida. Waziri Mkuu hakujishughulisha. Inawezekana hata hakumweleza Rais, na kama alimweza, basi ilikuwa juu juu tu. Akaacha mambo yaharibike. Moto ulipopamba bungeni, hakuwa na uwezo wala hoja ya kuwatetea mawaziri wake. Akawatosa. Kama watu wanauawa hashituki, itakuwaje siku mahasimu wetu wakaamua kusogeza mpaka? Hataagiza tuwaachie tu? Au ndio atamwaga chozi na mambo yakaishia hapo!
Ukiwatafakari Mheshimiwa Pinda na Mheshimiwa Frederick Sumaye (miaka 18.5 ya uongozi wao), unashawishika kuwapa ushauri wa bure wa kwamba jamani imetosha. Pumzikeni. Mmeshatoa mchango kwa Taifa lenu. Waachieni wengine.
Bado nitaendelea kuamini kuwa Pinda hawezi kuwa rais makini. Hilo linathibitishwa na rekodi yake, ikiwamo ya kushindwa kuwasimamia mawaziri wake.
Tanzania ya sasa ni kama treni iliyohama reli. Anahitajika rais makini na mahiri wa kuirejesha nchi kwenye mstari. Sina hakika nani ataiweza kazi hiyo, lakini walau naamini kuwa kati ya hao Pinda na Nyalandu hawamo.