Serikali imesema kuanzia sasa watumishi wabadhirifu wa fedha za umma hawatahamishiwa vituo vingine vya kazi, bali watachunguzwa na ikibainika watafukuzwa kazi mara moja.
Msimamo wa Serikali umetolewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipowasilisha hotuba ya Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2012/2013, jana.
“Watumishi wa umma watakaotuhumiwa kufanya ubadhirifu wa fedha za umma, watachunguzwa na tuhuma zikibainika ni za kweli watavuliwa madaraka waliyonayo na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
“Napenda kusisitiza kwamba Serikali haitawahamisha watumishi wa aina hiyo, bali hatua za kinidhamu na kisheria zitachukuliwa wakiwa kwenye vituo vyao vya kazi. Natoa wito kwa watendaji wakuu wa Serikali, Bodi za Wakurugenzi wa Mashirika ya Umma na madiwani kuhakikisha wanashiriki ipasavyo katika kusimamia fedha za umma kwa mujibu wa sheria, taratibu, miongozo na kanuni zilizopo.
“Nawaagiza wakurugenzi watendaji wa mamlaka za Serikali za Mitaa kubandika kwenye mbao za matangazo za makao makuu ya halmashauri na katika vituo vyote vya utoaji huduma, kiasi cha fedha kinachopelekwa kila mwezi na matumizi yake. Hii itawezesha wananchi kufuatilia matumizi ya fedha zilizopelekwa kwa ajili ya utoaji huduma kwenye maeneo yao ,” ameagiza Pinda.
Ununuzi wa mashangingi
Waziri Mkuu amesema katika mwaka huu wa fedha wa 2012/2013 Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kupunguza matumizi yasiyo na tija, hasa ununuzi wa magari makubwa ya kifahari (mashangingi).
Amekiri kuwa gharama za ununuzi na uendeshaji magari hayo ni kubwa mno. Miongoni mwa hatua alizotangaza ni kuweka ukomo wa ukubwa wa injini za magari ambayo Serikali Kuu, taasisi na Serikali za Mitaa, zitanunua.
“Chini ya utaratibu huo, magari yatakayonunuliwa yatakuwa ni yale yasiyozidi ukubwa wa injini wa cc 3000 kwa viongozi na watendaji wakuu; na yasiyozidi cc 2000 kwa watumishi wengine wanaostahili ya kutumia magari ya Serikali.
“Vilevile, ili kupunguza matumizi ya magari kwa viongozi na watendaji wakuu kwa safari za mikoani, Serikali itaanzisha vituo vya kanda vya magari ya Serikali yatakayotumika mikoani kwa shughuli za kazi. Mwongozo wa utekelezaji utatolewa.
Inatarajiwa kuwa utaratibu huu utapunguza matumizi ya fedha za Serikali kwa kiwango kikubwa,” amesema.