Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Manyara
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Geophrey Pinda ametembelea na kukagua eneo limepimwa viwanja kwa ajili ya kuhamisha waathirika wa Mafuriko yaliyotokana na maporomoko ya mawe na tope kutoka mlima Hanang.
Pinda amefanya ukaguzi huo tarehe 5 Januari 2024 akiambatana na mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga pamoja na viongozi wengine wa mkoa pamoja na wa wilaya ya Hanang.
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeshiriki pamoja na na wadau wengine katika zoezi la kutathmini kiwango cha uharibifu uliotokana na maafa yaliyotokea tarehe 3 Des 2023 na kushauri juu ya maeneo yanayoweza kutumika kuhamisha waathirika.
Akiwa katika eneo hilo tarehe 5 Januari 2024 wilayani Hanang mkoani Manyara, Mhe Pinda alielezwa na Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Manyara Wenceslaus Mtui kuwa, jumla ya ekari 100 kutoka Jeshi la Magereza kwenye eneo la Warret zimetolewa kwa ajili ya waathirika.
Tarehe 21 Desemba 2023 Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenister Mhagama alielekeza wizara ya Ardhi kuhakikisha viwanja kwa ajili ya kuhamisha waarhirika maeneo ya Gendavi, Jorodom, Ganana na Katesh – Hanang vinapimwa na kukamilika kabla ya Des 31. 2023
Kwa mujibu wa Mtui, zoezi la upimaji viwanja katika eneo hilo lililotolewa na Jeshi la Magereza umefanyika kwa weledi na kukamilika ndani ya siku saba ambapo jumla ya viwanja 269 vilipimwa na kupandwa mawe