Kocha wa zamani wa Simba, Mzambia Patrick Phiri, amewashauri Simba kuacha kuwaza ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu na kuwataka kupigania angalau nafasi ya pili katika msimamo.
Akizungumza katika mahojiano maalum na mwandishi wa makala hii, Phiri, aliyetimuliwa Simba katikati ya msimu huu, anasema Simba ni timu bora, lakini wana changamoto kubwa.
Anasema kuwa kama wanang'ang'ania kutaka ubingwa kwa sasa watajichanganya ingawa Yanga na Azam zikizubaa zinaweza kuipa upenyo wa kutwaa taji hilo kubwa katika mashindano ya soka Tanzania Bara.
“Lakini kwa sasa wasiwaze ubingwa,” anasema Phiri ambaye amedai anafuatilia maendeleo ya klabu hiyo pamoja na Ligi Kuu Bara.
“Najua wanataka ubingwa kwa sababu ya kuifunga Yanga, lakini naona bado,” anasema na kuongeza; “Wanachotakiwa ni kugombea kufanya vizuri, kushinda na kupata pointi tatu katika kila mechi japo kuwa ni ngumu sana katika kila mechi kupata ushindi, sema wakijituma wataweza kupata nafasi nzuri zaidi kuliko kugombania ubingwa.”