Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera  Bunge na Uratibu) na Mbunge wa Jimbo la Perahimo,  Jenista Mhagama amewataka wananchi  wa Jimbo hilo kurasimisha biashara zao ili kwenda na wakati na kujiletea maendeleo ya uhakika.

Waziri Mhagama ameyasema hayo  Jana kwenye ukumbi wa Njunde uliopo kata ya Peramiho katika Halmashauri ya Wilaya Songea vijijini,wakati wa kuhitimisha mafunzo ya siku moja kwa wananchi wa Jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma, yaliyotolewa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).

Mhagama amesema kuwa wananchi wa Songea kwa ujumla wamekuwa wakijishughulisha na kilimo na shughuli nyingine za kiuchumi, hivyo kutokurasimisha biashara zao BRELA kuna sababisha kukosa manufaa mengi zaidi.

Mhagama ametumia fursa hiyo pia kuipongeza BRELA kwa kufanikisha mafunzo hayo kuhusu huduma inazozitoa kwani wamekuwa lango la kufungua biashara nchini, hivyo wananchi wa Peramiho watanufaika na  elimu hiyo.

” Niwapongeze BRELA mmefanya jambo zuri sana kufika katika eneo hili na kukutana na wananchi hawa wa Jimbo la Peramiho na inaonesha wameelewa na watafanyia kazi, hivyo BRELA tutawahitaji wakati mwingine mje msajili hapa hapa watu wapate vyeti vyao, naomba salamu hizi mzifikishe kwa Afisa Mtendaji Mkuu na tunashukuru sana sisi wana Peramiho”, ameongeza Waziri Mhagama.

Aidha Waziri Mhagama amewakumbusha wananchi kuchangamkia fursa ya mafunzo hayo kwa kuanza mchakato wa kujisajili BRELA ili kupata manufaa zaidi.

“Hili ni kwenu wananchi elimu hii ambayo ni muhimu muifanyie kazi na hakika mtaona manufaa yake kwani sisi ni wazalishaji wazuri wa mahindi na tunafanya biashara, hivyo tukisajili itakuwa rahisi hata kufanya biashara na mataifa mengine”, ameongeza Waziri Mhagama. 

Mafunzo hayo ya siku moja yamewakutanisha wananchi zaidi ya 600 kutoka katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri  ya Wilaya ya Songea ambayo yameratibiwa na BRELA pamoja na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Peramiho.

Kwa upande wake Msajili Msaidizi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bi Fatma Jumanne  alisema kuwa Brela imerahisisha Sana usajiri wa biashara kwa Wafanyabiasha ambao wanahitaji kufungua kampuni na leseni.

Bi.Jumanne alisema kuwa popote ulipo unaweza kujisajiri kupitia simu janja yako na kwamba ada ni elfu 20 ambapo mchakato mzima wa kusajili Majina na Biashara na Kampuni umeelezwa waziwazi.

Naye Afisa Leseni Koyan Ndalway ametoa elimu kuhusu  hatua zinazohitajika ili kupata  Leseni za Biashara kundi “A” na umuhimu wa kupata Leseni za Viwanda pamoja na usajili wa Viwanda Vidogo, 

Kwa upande wake Afisa Sheria  Andrew Malesi aliwaeleza washiriki juu ya umuhimu wa  kusajili Alama za Biashara na huduma ili bidhaa zao ziweze kujitofautisha sokoni.