• • Ni jengo lenye ofisi nyingi kuliko lolote duniani
  • • Limeenea kwenye eneo la hekta 29
  • • Hutoa huduma za simu zipatazo maili 100,000
  • • Posta za jengo hilo hupokea barua zaidi ya 100,000 kila siku 
  • • Ni jengo lenye madirisha 7,754 

BAGAMOYO

Na Walter Sawe

Ni miaka 20 imetimia tangu mashambulizi yanayodaiwa kuwa ya kigaidi maarufu kama ‘September Eleven’ au 9/11 yalipotokea.

Kwa unayesoma makala hii, ninadhani utakuwa haujawahi kusikia historia ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani au kusoma kama hivi.

Ni hapo ndipo yalipo Makao Makuu ya ulinzi ya taifa kubwa la Marekani yanayojulikana kwa jina la Pentagon

Ni moja ya taasisi kubwa sana za ulinzi hapa duniani na eneo hilo ndilo la kwanza kukumbwa na misukosuko ya mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11, 2001; miaka 20 iliyopita.

Pentagon historia yake inaonyesha kwamba lina uwanja wa hekta 29 na lipo kwenye umbile la mzunguko. Katikati ya jengo kuna eneo la wazi, yaani ua lenye ukubwa wa hekta tano.

Ni jengo ambalo lipo kwenye eneo la hekta 29 na ni moja ya maeneo makubwa zaidi ya jengo lolote lile hapa duniani kutumika kama ofisi. 

Jengo hilo ambalo leo ninalizungumzia kupitia gazeti hili ili kila mmoja alifahamu kwa undani, ni jengo ambalo lina ofisi nyingi, ambazo kwa haraka haraka kwa mujibu wa vyanzo hivyo, ni zaidi ya mara tatu ya ofisi za Empire State Building, jengo lenye ghorofa 102 lililopo New York, kwa mujibu wa taarifa za mtandao wa Sky News.

Hili ndilo jengo refu zaidi kwa kwenda juu lililopo nchini Marekeani tangu mwaka 1954. 

Pentagon lina umbo la mviringo, lenye pembe tano zinazolizunguka kila upande, moja kwenda pembe nyingine, ukubwa wake tunaelezwa kwamba ni sawa na ukubwa wa ukumbi wa Bunge la Marekani linalojulikana kwa jina la National Capitol.

Ni Makao Makuu ya Wizara ya Ulinzi na vyombo vyote vya ulinzi vya ndani na nje ya taifa hilo kubwa kiuchumi duniani.

Humo zimo ofisi za ulinzi, ofisi za wanadhimu, pia ofisi za makatibu wote wa idara tatu za jeshi la nchi hiyo. 

Tunaelezwa na vyanzo hivyo vya habari kuwa jengo lipo ndani ya eneo la futi za mraba 6,500,000; eneo la futi za mraba 3,800,000 ndilo lenye uwezo wa watu kuishi.

Mtandao huo wa habari unasema hata wakati Vita Kuu ya Pili ya Dunia ilipopamba moto, watu zaidi ya 33,000 walipewa hifadhi ya kuishi na kufanya kazi ndani ya jengo hilo.

Nikiri hapa kwamba ili nipate kueleweka vizuri kwa wasomaji wangu popote pale lisomwapo gazeti hili la JAMHURI, nitaziweka hapa takwimu nilizoperuzi kwa umakini kuhusu jengo hilo. 

Sasa fuatana nami uweze kuona maajabu ya Pentagon; jengo kubwa kabisa duniani namna lilivyo:  

1. Lipo kwenye eneo la hekta 583. 

2. Lenyewe hasa limo ndani ya hekta 29. 

3. Eneo la katikati ambalo ni wazi ni hekta tano. 

4. Barabara zinazoingia na kutoka kwenye eneo hilo zina urefu wa maili 30.

5. Eneo hilo lina vichochoro 21.

6. Maegesho ya magari ndani ya jengo hilo yana ukubwa wa hekta 67. 

7. Magari yanayoweza kuegeshwa kwa wakati mmoja ndani ya eneo hilo ni 8,770.

8. Eneo la sakafu za jengo hilo ni zaidi ya futi za mraba 6,636,360.

9. Eneo la ukuta wa nje wa jengo hilo ni futi 921.

10. Eneo pia la kwenda juu ni futi 77.

11. Eneo la ghorofa ya chini sakafuni ni mm 5.

12. Idadi (korido) za njia  kwenye ukumbi huu ni 284.

13. Eneo la kwenda kupata maji ya kunywa lina ukubwa wa mita za mraba 691.

14. Taa zilizofungwa ndani ya jengo hilo jumla yake ni 16,250.

15. Taa zinazoharibika kila siku ni 250.

16. Madirisha ya jengo hilo ni 7,754.

17. Eneo lililopandwa nyasi maarufu kama ‘ukoka’ ni hekta 7.1, sawa na futi 309,276.

18. Simu zinazopigwa kila siku ndani ya jengo hilo ni zaidi ya 300,000.

19. Vifurushi vya barua vinavyopokewa katika posta iliyomo ndani ya jengo hilo ni 200,000 kwa siku.

20. Barua zinazopokewa posta ya ndani ya jengo hilo ni 1,200,000.

21. Idadi ya nguzo za zege za jengo hilo ni 41,492.

Nimejaribu kuelezea hayo machache kuhusu Pentagon kutokana na kuvutiwa na taarifa iliyochapishwa na gazeti hili toleo la Septemba 7 -13, 2021 ukurasa wa 10.

Taarifa hiyo inahusu namna Rais wa Marekani, Joe Biden, alivyotaka kuwekwa wazi kwa baadhi ya nyaraka za mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11, 2001.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari nilivyovichambua kutoka kwenye mitandao ya kimataifa, nikaona kupitia hapa Watanzania wenzangu mpate kusoma na kulielewa kwa undani jengo hilo linalosifika kwa ulinzi mkali. 

Taarifa zinasema jengo hilo lina sura ya pembe tano zinazolingana.

Sehemu ya kwanza ya jengo hilo ni njia za ndani za eneo la ukumbi, ambazo kama zitanyooshwa zitakuwa na urefu wa maili 17.5.

Iwapo nguzo 41,492 za Pentagon zitatandazwa chini na kunyooshwa; kwa hesabu ya haraka, zinaweza kufika umbali wa kilomita 320; yaani umbali wa kutoka Dar es Salaam hadi Tanga kwa njia ya barabara. 

Ujenzi wa Pentagon ulianza rasmi Septemba 11, 1941; yaani miaka 60 kamili kabla ya shambulio la kigaidi la Septemba 11, 2001, na sasa ni miaka 80.

Taarifa zinahitimisha zikisema kuwa hata vifaa vilivyotumika kwenye ujenzi wa jengo hilo vilikwenda sambamba na matatizo yaliyokuwapo wakati ule; yaani Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Wakati huo haikuwa rahisi kupatikana kwa vifaa vya ujenzi kama mbao na matofali, kwa hiyo vifaa vilivyotumika vilikuwa ni vipande vya chuma na zege. 

Makala hii imeandaliwa na mwandishi na mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii anayepatikana kwa barua pepe: sawe.walter @yahoo.com na simu namba 0717 699 729.