Shirika la Oxfam la nchini Uingereza limetoa taarifa hivi karibuni kubainisha kuwa watu 62 duniani wanamiliki zaidi ya nusu ya utajiri unaomilikiwa na nusu ya watu katika sayari hii. Watu 62 wanamiliki utajiri unaomilikiwa na watu 3,750,000,000.

Oxfam wanatuambia kuwa ni jukumu la kila raia ulimwenguni kuhoji hali hii ya utajiri mkubwa kiasi hicho kumilikiwa na idadi ndogo kiasi hicho ya watu, watu wanaoweza kuenea ndani ya basi moja linalofanya safari zake kati ya Musoma na Mwanza. Na inatoa hoja za msingi kabisa kutetea hoja yao.

Suala la msingi hapa si utajiri tu wa hawa watu 62, ila ni tatizo la kukithiri ulimwenguni kwa umaskini na ni kwa jinsi gani jitihada za kuupunguza zinaathiriwa na uwezo mdogo wa serikali ulimwenguni wa kukusanya kodi kutoka kwa matajiri wa aina hii.

Kwa mujibu wa taarifa hii ya Oxfam, tangu mwaka 2010 utajiri wa hawa vinara 62 umeongezeka kwa dola trilioni 1.7 za Marekani. Hiyo ni moja nukta saba ikifuatiwa na sifuri kumi na moja. Lakini katika kipindi hicho hicho utajiri wa nusu ya watu ulimwenguni umeporomoka kwa asilimia 38. Na si hivyo tu, idadi ya watu duniani imeongezeka kwa milioni 400. Maana yake ni kuwa idadi kubwa zaidi ya watu imeendelea kugawana umaskini wakati idadi ndogo ya watu imejiongezea mapato ya kugawana.

Matajiri wanazo njia nyingi za kukwepa kulipa kodi. Baadhi ya njia hizi ni halali na nyingine ziko ukingoni mwa uhalali ingawa si sahihi kusema moja kwa moja kuwa ni njia haramu kwa sababu tu ya kuwapo kwa mifumo ya kisheria ya nchi ambayo inaruhusu njia mbalimbali za ukwepaji kodi.

Njia zisizotiliwa shaka kisheria za ukwepaji wa kodi ni pamoja na misamaha ya kodi. Darasa la awali kabisa katika somo linalofundishwa kwa nchi maskini zinazotafuta kuvutia wawekezaji, misamaha ya kodi inasisitizwa katika kila hatua. Tunafundishwa kuwa nchi inapoongeza misamaha ya kodi itaongeza uwekezaji, ajira, na mauzo ya bidhaa nchi za nje; na hivyo kuongeza mapato ya nchi. Hiyo ni nadharia. Uhalisia uko tofauti kidogo.

Utafiti uliofanywa Kenya na mashirika mawili, Tax Justice Network-Africa na ActionAid International ulionesha kuwa nchi hiyo inapoteza mapato zaidi ya yale inayoyapata kutokana na misamaha ya kodi. Utafiti huo huo unazungumzia jitihada za nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kushindana baina yao kuvutia wawekezaji kwa kutoa misamaha ya kodi na namna ushindani wa aina hiyo unavyozorotesha makusanyo ya kodi katika nchi hizo.

Kwa hiyo pamoja na kuwapo kwa sheria ndani ya nchi mbalimbali zinazotoa misamaha ya kodi, bado ni suala linaloathiri ukusanyaji wa mapato ya serikali.

Ni kwa upande ule wa ukwepaji kodi uliopo ukingoni tu mwa uhalali ndipo matajiri wa ulimwengu wanapoonesha umahiri wao wa kukwepa kulipa kodi. Na ni hapa ndiyo tunaona nguvu ya hoja ya Oxfam dhidi ya utajiri uliyokithiri wa hawa matajiri 62 pamoja na wengine wanaotaka kufanana nao.

Kwa kawaida, matajiri hawa au mashirika wanayomiliki, kwa kutumia sheria zilizopo huweza kupunguza kwa kiasi kikubwa sana kodi wanazolipa na hufanya hivi kupitia nchi kadhaa ulimwenguni ambazo hupokea utajiri huu bila kutoza kodi yoyote. Oxfam wanaarifu kuwa kati ya mashirika 201 yanayoongoza ulimwenguni, 188 yameweka makao katika nchi hizi zisizotoza kodi. Inakadiriwa kuwa iwapo matajiri hawa na mashirika wanayomiliki yangekuwa yanalipa kodi, basi kiasi cha dola bilioni 190 za Marekani zingepatikana kama ongezeko la kodi kwa serikali mbalimbali kila mwaka.

Inakadiriwa pia kuwa karibia asilimia 30 ya utajiri wa fedha wa Bara la Afrika umefichwa kwenye nchi hizi zisizotoza kodi, ikiwa ni sawa na dola bilioni 14 za Marekani kila mwaka. 

Ni vita ambayo nchi maskini haziwezi kushinda zenyewe bila mikakati ya pamoja ya kimataifa. Haiwezekani kudhibiti maji yanayofika kwenye bomba linalotumiwa na wengi kama kwenye mfumo wa maji wapo wezi wanaotoboa bomba na kuvujisha maji njiani.

Na ni mikakati ambayo haiwezi kufanikiwa bila matajiri wakubwa na mashirika wanayomiliki kukubali kuanza kulipa kodi stahiki inayolingana na utajiri wa biashara na rasilimali wanazokamua kutoka kwa watu bilioni 7 duniani.

Oxfam imekuwa ikifanya kampeni ya kukomeshwa kuwapo kwa nchi zinazoruhusu kupokea mapato ya mashirika ya kimataifa na matajiri bila kutoza kodi kama hatua ya kwanza ya kupunguza ukwepaji kodi. Aidha, Oxfam inajenga hoja kuwa ni muhimu kutoza kodi kwa mapato yote ambayo yamekuwa yakifichwa kwenye nchi hizo, pamoja na kuhimiza kutumika kwa kodi itakayopatikana kwenye sekta za afya, elimu, na huduma muhimu za umma zenye uwezo mkubwa zaidi wa kupunguza umaskini.

Oxfam imetoa taarifa hii ya hivi karibuni kabla ya mkutano unaofanyika kila mwaka mjini Davos, Uswisi, ambako mashirika, watu mashuhuri (miongoni mwao matajiri wakubwa duniani), wasomi, wanasiasa, wachumi, na waandishi wa habari hukutana na kujadili kwa pamoja masuala yanayokabili dunia kwa madhumuni ya kukubaliana kuhusu ajenda ya pamoja ya ulimwengu, kikanda, na katika tasnia mbalimbali. Ni jitihada ya Oxfam ya kuibua mjadala juu ya tatizo hili miongoni mwa wale wanaokutana Davos.

Hata hivyo, baadhi ya watu wanaona mkutano huu wa Davos kama jukwaa la matajiri kuweka mikakati ya pamoja ya kulinda maslahi na utajiri wao.

Mkakati wa Oxfam ni wa kuhimiza tajiri apunguze utajiri wake. Unaweza kufanikiwa tu kwa kuonesha ni jinsi gani pengo kati ya walionacho na wasionacho linapokuwa kubwa linaweza kuathiri maslahi ya walionacho kuendelea kulinda utajiri wao.

Si mkakati rahisi, lakini ni mkakati unaopaswa kuendelezwa kwa manufaa ya wengi.