Chama cha ACT Wazalendo kinapenda kuutangazia umma kuwa mchakato wa ndani ya Chama wa wanachama kujitokeza na kutangaza nia ya kugombea nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi mkuu 2025 umefunguliwa rasmi kuanzia tarehe 15 Januari, 2025.

Hatua hii ni utekelezaji wa agizo la Halmashauri Kuu ya Chama Taifa iliyoelekeza Chama kuweka utaratibu wa wanachama kutangaza nia ya kugombea nafasi za Udiwani, Udiwani Viti Maalum, Ubunge, Ubunge Viti Maalum na Urais.

Masuala muhimu ya kuzingatiwa kwenye mchakato huu ni kama ifuatavyo;-

  1. Watiania wanapaswa kujisajili kwenye orodha ya watiania kwenye ngazi husika kwa kujaza fomu maalum kama ifuatavyo;
  • Watiania wa Udiwani na Udiwani wa Viti Maalum ngazi ya Kata;
  • Ubunge na Ubunge wa viti maalum ngazi ya Jimbo; na
  • Watiania wa Urais Ofisi ya Makao Makuu.
  1. Watiania wanaruhusiwa kujitangaza kupitia njia mbalimbali ikiwemo kuzungumza na waandishi wa habari. Idara ya Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma ngazi ya Taifa kwa kushirikiana na viongozi wa Mikoa na Majimbo imeagizwa kuhakikisha kuwa watiania wote wanapata nafasi ya kujitangaza kupitia kurasa za mitandao ya kijamii ya Chama na kuwaunganisha na waandishi wa habari na kusambaza taarifa za watiania hao.
  2. Viongozi wa Mikoa, Majimbo na Kata wameagizwa kuwaruhusu watiania kutumia Ofisi za Kata, Majimbo na Mikoa kutangaza nia zao. Kwa ngazi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, watiania wanaruhusiwa pia kutangaza nia kupitia Ofisi ya Makao Makuu ya Chama.
  3. Watiania wanapaswa kujipima kwa kuzingatia vigezo vya watiania ambavyo vimewekwa na Halmashauri Kuu ya Chama. Vigezo hivyo ni pamoja na kutimiza sifa za kugombea nafasi husika zilizoainishwa na sheria za nchi na Katiba ya ACT Wazalendo Toleo la Mwaka 2024 pamoja na Kanuni za Uchaguzi za Chama.

Sifa nyingine ni kuwa na haiba, maadili, uwezo wa kujieleza na maono yanayoendana na nafasi ambayo mtiania anakusudia kuigombea.

Watiania watapimwa pia kwa ushiriki wao katika ujenzi wa Chama. Viongozi wa ngazi husika wameagizwa kuweka utaratibu wa kuwashirikisha watiania katika shughuli za ujenzi wa Chama katika ngazi husika na kutunza taarifa za ushiriki wao.

  1. Chama kitaweka utaratibu wa kuwasaili (interview) watiania kabla ya taratibu za kikatiba za uteuzi wa wagombea. Taratibu na jopo la usaili (Interview panel) litatangazwa baadaye kwa ngazi za Ubunge na Urais. Usaili huo utakuwa wazi kwa umma kupitia vyombo mbalimbali vya habari.

Wanachama wote wa ACT Wazalendo wenye sifa za kugombea Udiwani, Udiwani Viti Maalum, Ubunge, Ubunge Viti Maalum na Urais wanakakaribishwa kutangaza nia kwa utaratibu ambao umeelekezwa. Chama cha ACT Wazalendo kitaendeleza utamaduni wake wa kuendesha michakato ya uchaguzi kwa kuzingatia misingi ya uwazi, demokrasia na usawa.

Imetolewa na;

Ado Shaibu
Katibu Mkuu
ACT Wazalendo

15 Januari, 2025.
Dar es Salaam.