Dar es Salaam

Na Andrew Peter

Baada ya hekaheka za muda mrefu hatimaye pazia la Ligi Kuu ya Tanzania Bara litafungwa rasmi Jumatano hii lakini macho yatakuwa kwa timu nne za mwisho zinazowania kubaki katika ligi hiyo.

Wageni Mbeya Kwanza wanaburuza mkia wakifuatiwa na Biashara United, Tanzania Prisons na Ruvu Shooting zote zimekalia kuti kavu, kwa kuwa timu mbili zitashuka daraja na mbili zitakwenda kucheza mechi ya mtoano na timu mbili za Daraja la Kwanza ili kupigania hatima yao ya kubaki au la.

Ratiba ya mwisho ya timu hizo itashuhudia Mbeya Kwanza ikiwakaribisha Simba kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Biashara United watakuwa wageni wa Azam pale Azam Complex, Chamazi lakini Ruvu Shooting wataonyeshana kazi na  Prisons kwenye Uwanja wa Mabatini.

Michezo mingine itashuhudia mabingwa wapya Yanga wakiwa wenyeji wa Mtibwa Sugar wakati Kagera Sugar watacheza dhidi ya Polisi Tanzania huku mabingwa wa 1988, Coastal Union wakiwa nyumbani Mkwakwani kuivaa Geita Gold FC, nayo Dodoma Jiji wataikaribisha KMC kwenye Uwanja wa Jamhuri, wakati Namungo akiivaa Mbeya City.

Pamoja na kufungwa kwa pazia la ligi, ilikuwa ni safari yenye milima na mabonde, achilia mbali vilio na vicheko vilivyotawala kila kona ya nchi kutokana na burudani nzuri iliyopatikana viwanjani.

Kutokuwapo viporo

Kuwapo kwa viporo vingi ni moja ya mbinu za upangaji matokeo, lakini katika msimu huu Bodi ya Ligi na TFF wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa kwa timu zote kupewa muda sawa wa kucheza mechi zao pamoja na kuwa zinashiriki katika mashindano ya kimataifa. 

Kitendo hicho kimeondoa yale malalamiko ya upendeleo wa timu moja hasa kwa klabu kubwa; Simba na Yanga, lakini bado Bodi ya Ligi wanaweza kutengeneza ratiba bora zaidi msimu ujao ili timu zote zipate muda sawa wa kupumzika kila wanapotoka kucheza mechi za mbali kama ilivyokuwa kwa miamba ya Kariakoo.

Mechi kuchezwa usiku

Msimu huu tumeshuhudia kwa mara ya kwanza Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma mechi zake zikichezwa usiku. Hili ni jambo la kuwapongeza  Azam na wadhamini kwa sababu tulizoea kuona mechi za usiku zikichezwa Dar es Salaam pekee pale – Kwa Mkapa na Azam Complex. 

Pia mechi nyingi zikichezwa usiku ni hatua kubwa, kwani inatoa nafasi kwa timu nyingi kuonekana kwenye TV na kutoa fursa kwa mashabiki kufuatilia klabu zao bila ya presha ya kutoroka kazini au kufunga biashara zao mapema.

Vita ya ufungaji bora

Hizi mbio za ufungaji bora zilikuwa na ushindani mkubwa tangu mwanzo wa msimu, washambuliaji kadhaa wakionyesha umahiri wao katika kuzifumania nyavu. Hadi sasa zimebaki za nyota wawili – George Mpole wa Geita Gold (16) na Fiston Mayele wa Yanga (16) kabla ya mechi za mwishoni mwa wiki.

Mbali ya wawili hao, washambuliaji wengine waliotikisa nyavu ni pamoja na Reliant Lusajo (Namungo) mabao 10, Roggers Kola wa Azam (9), Matheo Antony wa KMC (9), Kibu Denis wa Simba (8), Saido Ntibazonkiza wa Yanga (7), Anuary Jabil wa Dodoma Jiji (7), mkongwe Meddie Kagere wa Simba (7) na Abdul Suleiman Sopu wa Coastal Union (7).

Washambuliaji hawa na nyota wengine ndio waliokuwa wakileta furaha kwa mashabiki wa soka kutokana na umahiri wao wa kuzifumania nyavu, kwa maana Waswahili wanasema ‘raha ya mechi bao’.

Ngome imara

Kama kuna kitu Kocha wa Yanga, Nabi, alifanikiwa msimu huu ni kutegeneza safu bora ya ulinzi ambayo hadi mechi 28 ilikuwa imeruhusu mabao saba, wakifuatiwa na Simba iliyoruhusu wavu wake kuguswa mara 13 katika idadi hiyo ya michezo.

Timu zenye safu mbovu za ulinzi ni Ruvu Shooting, wenyewe wameruhusu kufungwa mabao 38, wakifuatiwa na Mbeya Kwanza (37), jambo lililoziweka timu hizo katika janga la kushuka daraja.

Timuatimua ya makocha

Kaulimbiu ile ile ‘kocha ameajiriwa ili atimuliwe’ ndiyo iliyotekelezeka msimu huu kwa klabu 12 kuwafukuza makocha 13 kwa sababu mbalimbali.

Simba na Biashara United zikiweka rekodi ya kuwatimua makocha wawili msimu huu. Pamoja na kuwafukuza makocha hao Simba imeondoka mikono mitupu, wakipoteza mataji yao yote ya ndani wakati Biashara United ikiwa katika hatihati ya kushuka daraja.

Makocha waliotimuliwa na Simba ni Gomes na Pablo Martin, wakati Biashara United ikiwatupia virago Odhiambo na Bahati. Wengine waliotupiwa virago ni Joseph Omog (Mtibwa Sugar), Ndayiragije (Geita Gold), Geogre Lwandamina (Azam),  Salum Mayanga (Prisons), Medo (Coastal Union), Hemed Morocco (Namungo), Mbwana Makata (Dodoma Jiji), Habib Kyondo (KMC) na Haruna (Mbeya Kwanza).

Hii ni moja ya rekodi za kutisha katika ligi yetu. Unaweza kujiuliza, kweli makocha 13 wote hawana sifa hizo au kuna kitu cha tofauti nyuma? Kwa sababu timu nyingi zilizofukuza makocha bado hali zao ni mbaya.

Naamini viongozi wanapaswa kukaa chini na kufanya uamuzi sahihi wa kutafuta makocha bora watakaokaa na timu kwa muda mrefu, japo hata misimu miwili ili kujenga kikosi bora. Ila hii timuatimua kila mara haitaweza kuleta tija katika klabu zetu.

Dirisha la usajili limefunguliwa, ni wazi wachezaji wa Kitanzania wanapaswa kujitambua kwa kutafuta mawakala makini watakaowasimamia katika kukamilisha masuala yao ya usajili.

Ni kipindi kizuri kwa wachezaji kuvuna fedha na kujipanga kimaisha, lakini hiyo inawezakana zaidi ukiwa na uongozi imara utakaokusimamia katika kuingia mikataba na klabu kwa faida ya pande zote.