Duniani sisi watoto wote wa Adam na Hawa tumerithi woga wa kuamua mambo. Ili kukwepa lawama, tunasukumia wengine tatizo ili sisi tuonekane tu wasafi. Tabia hii ya kukwepa kuwajibika binadamu tumeirithi toka kwa Adam na Hawa (Eva) pale bustani ya Edeni. Unajua ilitokeaje?
Tunasoma katika maandiko matakatifu maneno haya nanukuu…(Mungu) akasema; “Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je, umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usile?” Adam akajibu; “Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo nikala”. Bwana Mungu akamwambia (Hawa) mwanamke; “Ni nini hili ulilolifanya?” Mwanamke (Hawa) akasema; “Nyoka alinidanganya nikala” (soma hayo toa Kitabu cha Mwanzo sura yile ya 3 mistari 11 – 13).

Wasomaji si mnaona namna babu yetu Adamu alivyokacha kujibu swali la Mungu akasukuma lawama kwa bibi yetu Hawa? Na yeye Hawa kwa kukwepa lawama eti akasukumia lawama kwa nyoka ili mradi asionekane mkosefu! Hiyo ndiyo tabia ya binadamu kushikwa na woga kukabili tatizo. Hapo basi kuepukana na lawama husukumia kwa mtu mwingine. Huu ni udhaifu au upungufu wa kila binadamu, lakini upungufu namna hii unasahihishika hapa duniani.
Katika suala la mafao ya Mzee Paulo Sozigwa watumishi wa Ikulu hawawezi kutupia lawama kwa mwajiriwa Sozigwa. Yeye alitumwa tu kufanya kazi pale kama maafisa wengine wowote. Uwaite watumishi wa Ikulu au vinginevyo ukweli unabaki pale pale alipostaafia ndipo wanatoa waraka wa kumjulisha ukomo wa utumishi wake na wanawajibika kumwandalia malipo ya mafao ya uzeeni. Hazina wanachotaka ni Date of 1ST Appointment, Present salary na Date of Retirement. Maadam Ikulu waliomba nyaraka, na Bwana Joseph Sanga anakiri Mzee na mke wake walikabidhi hapo sasa mzigo wa lawama umo mabegani mwa maafisa wale waliokabidhiwa nyaraka ambao Sanga anasema aliwapa washughulikie. Hapo moja kwa moja wenye kuwajibika ni hao maafisa walio-misplace nyaraka za Mzee. Nashauri watumie photocopy ya Staff List kama kithibitisho cha ajira yake Mzee huyu.

Haya sasa Staff List ya 1965 uk. 272 UTUMISHI wameandika Date of 1st Appointment na Ikulu ni last station yake kama Staff List ya 1972 uk. 5 ilivyoonyesha. Hivyo Mzee huyo ingawa ameshatutoka, mtendeeni haki MLIPENI STAHILI YA MAFAO yake kwa mshahara wa Katibu Mkuu – Presidential Appointment ya mwisho. Je, nani alimpa taarifa ya kustaafu kwake? Huyo huyo amwandalie malipo ya mafao yake. Jamani mtendeeni haki mzee huyu.
Labda nisaidie ushauri wa kizee. Katika gazeti lile la JAMHURi toleo la 294 la Jumanne tarehe 16 – 22 Mei, 2017 uk. 15 kuna picha nzuri, lakini ya majonzi. Pale wanaonekana watu watano; wanne ni wa kuazimwa kutoka Idara ya Maelezo na mmoja tu Baba wa Taifa ndiye mwenyeji wa Ikulu “original”. Lakini cha kusikitisha katika picha ile ni kuwa wanne wao wameshatangulia mbele ya haki kwa Mungu. Alianza Habibu Halahala (kwa kukatwa na panga la helikopta pale Ndanda akiwa kazini na Mzee Hassan Mwinyi) akafuata Mwalimu Baba wa Taifa (kwa ugonjwa wa saratani ya damu kule St. Thomas Hospital, London, Uingereza) akaja Brigedia Jenerali Hashim Mbita (alifariki dunia Lugalo JWTZ kwa ugonjwa wa moyo) na Ijumaa Mei 12, 2017 huyu Mzee Paul Sozigwa ninayemwandikia makala hii katutoka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ugonjwa wa moyo.

Nishauri basi, tumuombe Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, kwa neema alizojaliwa na Muumba wake, asaidie kumwombea hayati Paulo Sozigwa alipwe mafao yake ya uzeeni, kwa kile Waingereza wanakiita “posthumously” familia yake warithi wapate kifuta machozi. Sina shaka rais wetu msikivu na mwelewa wa kilichotokea ataidhinisha malipo. Tarehe zile za kwenye Staff List zitumike kama-anthentic document ya ajira yake ili HAKI ya Mzee Sozigwa isipotee.
Warumi hapo kale wakisema hivi “FIAT JUSTITIA RUAT COELUM” haki ifanyika hata mbingu ifunguke! Nadhani JAMHURI na wapenda utawala wa HAKI na wa SHERIA wataliona hili na kusaidia Mzee Sozigwa alikolala apumzike kwa amani akiona warithi wake wamepata mafao aliyoyatabikia sana wakati wa uhai wake.
Watu watauliza vipi mzee mimi kulivalia njuga namna hii suala hili la mafao ya Mzee huyu wa Kizaramo? Mimi namzidi kidogo kiumri maana leo nina miaka 87 wakati Paulo alikuwa na miaka 84 hivi. Lakini taabu ya kufuatilia mafao nimeipata wala sijui kukata tamaa!

Hapa nilipo nalilia MSAMAHA WA KODI YA MAJENGO, huu sasa ni mwaka wa 10 tangu Serikali iagize wakurugenzi wote wa Miji, Halmashauri na Majiji watoe misamaha kwa wazee, lakini bado ninazungushwa tu. Basi kwa kuchelea yaliyomfika mzee mwenzangu naona nami naelekea huko huko.
Kila mwaka ifikapo Oktoba Mosi wazee duniani kote kwa maelekezo ya Umoja wa Mataifa (UN) tangu mwaka 1999, huwa tunasherehekea Siku ya Wazee Duniani. Basi, mwaka 2005 sherehe zile zilifanyika kitaifa Dar es Salaam pale Mnazi Mmoja na mimi ndiye nilikuwa Mwenyekiti wa sherehe zile. Mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Frederick Sumaye.

Wazee katika risala yao kwa mgeni rasmi waliweka maombi kadhaa moja wapo lilikuwa Serikali iwape MSAMAHA WA KODI YA MAJENGO kwa nyumba zile walizojenga kabla ya kustaafu na wanaishi wenyewe na familia zao. Hii ilikuwa kutokana na ukali wa maisha ya kustaafu na wanalipwa ka-pensheni kiduchu kila mwezi. Wakati ule tukipata Sh 50,000 wachilia mbali ulikuwa nani katika utumishi wa umma-Karani au Katibu Mkuu – Serikali iliamua kuwarundika wazee wale wote wa 1954Pension’s Ordinance walipwe “flat rate”ndiyo hizo Sh 50,000. Hivi sasa tunalipwa Sh 100,000 kila mwezi. Hata hizi jamani hazitoshi kitu kwa hali ya maisha ya sasa. Sote tunanunua vitu kwa bei ile ile kumbe anayelipwa mamilioni kwa mwezi na sisi wa laki moja kwa mwezi tunauziwa kwa bei moja tu. Tunaumia sana wazee. “There is no justice under the sun” wanasema wanafalsafa wa kale.

Mheshimiwa Waziri Mkuu Sumaye aliona hali ya wazee wale pale Mnazi Mmoja akaomba apatiwe muda akaliwakilishe OMBI la wazee wastaafu kwa Mheshimiwa Rais Benjamin Mkapa kwa uamuzi wa jambo nyeti kama lile.
Jambo la kufurahisha sana kwa wazee ni kule kuona Mheshimiwa Rais Mkapa, alilipokea ombi lile kwa uzito wake na akalitolea uamuzi muafaka kwa wazee.
Ndipo Serikali ilitoa waraka elekezi kwa halmashauri zote hapa nchini kupitia wakurugenzi wa miji, manispaa na majiji katika WARAKA wa Serikali wenye Kumb. Na. CHA/91/387/01/86 wa Februali 1, 2007, ambao unajieleza wazi wazi na unajitosheleza kabisa.
Kwa uzito wa uamuzi ule mimi kwa upande wangu katika Tawi la SAWATA la Wazee wa Temeke tuliupokea na kuanza kuufanyia kazi. Niliandika ombi langu kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke kupitia Diwani wangu akiitwa Mzee Mchumila kupitia ofisi ya Mtendaji Uwanja wa Taifa na kupitia Mwenyekiti Serikali ya Mtaa Miburani mwaka 2010. Hivi niandikapo makala hii kwa uchungu nasikitika kusema sikujibiwa na wala sijajibiwa mpaka leo hii 2017!
Pamoja na kukumbushia mara kadhaa ombi langu hilo, nadhani huyu aliyepo ni mkurugenzi wa tatu hivi sasa (kwanza alikuwa mtu akiitwa Kongwa, akaja Mkurugenzi akiitwa Kagimbo na hivi sasa yupo Mkurugenzi aitwaye Nasibu Mbaga) haujatolewa msamaha wowote kwa mzee yeyote. Sisi wazee hatujaorodheshwa ki-wilaya ingawa manispaa imetuma maafisa tathmini hapa nyumbani kwangu kuthibitisha kuwa kweli ninaishi humo na wala sipangishi.

Hivyo mimi kwa kuchelea kupata kile kilichomfika mzee mwenzangu Sozigwa, nikifa familia yangu itajaambiwa – wapi DOCUMENT YA MSAMAHA WA KODI toka kwa mkurugenzi? Jibu litakuwa HAKUNA. Ndipo itaamriwa hakuna proper document, lipeni kodi ya majengo! Hilo naliogopa sana (“I anticipate such happening to be fall on my family”). Mwaka 2016 nilipeleka ombi la tatu kwa mkurugenzi na mpaka leo hii sijajibiwa. Nafungasha nakala ya barua yangu kuthibitisha nisemacho. Huu utekelezaji mbaya wa maagizo ya Serikali unaofanywa kwa makusudi na maafisa vijana ni dhuluma kubwa kwa wazee wastaafu katika nchi hii.
Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Magufuli na Waziri wake Mkuu Kassim Majaliwa ni ya utendaji – Executions of Directives, basi naomba wampe hayati Mzee Paulo Sozigwa mafao yake kwa utumishi alioutekeleza katika Taifa hili, familia yake ione kweli hapa pana KAZI TU na kuna utawala wa HAKI na wa SHERIA.

Pili, nawasihi sana waagize wakurugenzi kwa mujibu wa waraka ule wa Serikali wa Februari 1, 2007 wazee wote wenye kuishi katika nyumba zetu tuorodheshwe na tulioomba misamaha tupatiwe kadri ya maagizo ya ibara (i) na (iv) za waraka ule. Utawala bora ni pamoja na kufuata sheria zilizotolewa na siyo kujibaraguza mpaka wazee tufariki dunia sasa faida ya kuwa senior citizen ni ipi?
Wakurugenzi, kumbukeni vilio vya vyura mle kisimani wakati watoto wakicheza ule mchezo wa kurushia mawe kisimani walimokuwa wakiishi vyura. Kilio cha vyura kilikuwa; “watoto msitupe mawe huku kisimani, sisi tunaishi humu basi mchezo wenu ndiyo mauti yetu sisi tuishio majini”. Hadithi hii imo katika kitabu cha HESOPO yule Myunani sisi tulisoma tukiwa STD III miaka ile ya 1940. Sijui kama wenzetu wa siku hizi wamewahi kusoma hizo HADITHI ZA HESOPO. Nakumbuka mara kadhaa Baba wa Taifa akizitaja katika mazungumzo yake. Mathalani, “Nani atamfunga paka kengele?” Au “Sizitaki mbichi hizi” – au “Mbwa Mwitu na Mwanakondoo” au “Fisi na mkono wa Mwanadamu”, na nyinginezo kemkem. Ni hadithi zilizokuwa na mafunzo fulani katika maisha.

Basi, zembea yenu watawala ni vifo kwa wastaafu tuliojenga Taifa hili wakati tunapigania Uhuru ambao nyie mnaufaidi sasa. Ninaamini Serikali imesikia na haki itatendeka kwa warithi wa hayati Paulo Sozigwa.
Alijulikana sana kwa kile kipindi chake katika Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) kikiitwa “MIKINGAMO”. Isitoshe wakati wa kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977 alibuni neno MANYANG’AU, lililowaumiza sana baadhi ya washirika wa Jumuiya, majirani zetu. Na kipindi cha vita na Nduli Idd Amini, Sozigwa alitoa propaganda safi sana juu ya maendeleo ya vita ile, sasa eti afe bila kulipwa mafao yake ya uzeeni! JE, NI SAWA HIYO? Mzee huyu hakustahili kutendewa vile! APUMZIKE KWA AMANI.

>>TAMATI