Makonda kitanzini
*Anyang’anywa ulinzi, vimulimuli
DAR ES SALAAM
NA MWANDISHI WETU
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amenyang’anywa ulinzi.
Tofauti na wakuu wengine wa mikoa nchini, Makonda amekuwa na ulinzi mkali uliohusisha askari maalum.
Mara kadhaa msafara wake ulikuwa na magari manne hadi sita, ukiwa unatanguliwa na gari au pikipiki ya king’ora ya polisi.
Hadi mwishoni mwa wiki iliyopita, Makonda alionekana akiwa amebakiwa na gari moja pekee aina ya Toyota Land Cruiser ‘shangingi’.
Makonda alikuwa na ulinzi mkali kutokana na kile kilichotajwa kuwa ni kumhami dhidi ya watu ‘wabaya’, hasa waliojihusisha na bishara ya dawa za kulevya.
Kwa nyakati tofauti, alitaja hadharani majina ya watu maarufu na wa kawaida aliodai kuwa wanajihusisha na biashara hiyo. Miongoni mwao ni wafanyabiashara na wanasiasa.
Vyanzo vya habari vimeliambia JAMHURI kuwa kuondolewa kwa ulinzi huo ni maagizo yaliyotoka ngazi za juu za uongozi.
Kwenye mitandao ya kijamii watu mbalimbali walihohoji sababu za msingi za Makonda kuwa na ulinzi mkali ambao ulikaribiana kwa kila hali na ule wa viongozi wakuu wa kitaifa.
Mara kadhaa barabara ‘zilisafishwa’ ili kuwezesha msafara wake kupita, jambo lililolalamikiwa na baadhi ya watumiaji wengine wa miundombinu hiyo.
Makonda aliteuliwa Machi 16, 2016 kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, akitoka kwenye nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni mkoani humo. Kabla yake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alikuwa Said Sadick, ambaye kwenye mabadiliko hayo alihamishiwa mkoani Kilimanjaro kuendelea na wadhifa huo.
Baada ya kuteuliwa Makonda alianza kazi kwa makeke mengi akilenga kupambana na watu aliowatuhumu kujihusisha na biashara na matumizi ya dawa za kulevya.
Fabruari 2, mwaka jana alitaja orodha ya watu aliodai wanajihusisha na mtandao wa dawa hizo ndani na nje ya nchi. Akawataja pia polisi tisa aliosema wanajihusisha na uuzaji dawa za kulevya.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano haitovumilia vitendo vya uuzwaji wa dawa hizo na akatoa agizo kwa Jeshi la Polisi kuwakamata maafisa aliowataja akidai wanashirikiana na wauza dawa.
“Nimepata taarifa kuwa baadhi ya askari Jeshi Polisi wanajihusisha na uuzwaji wa dawa za kulevya na wengine wamekuwa na utaratibu wa kwenda kuchukua pesa kila Jumamosi kwa wauzaji wa dawa za kulevya na ndio maana biashara hii inaendelea kuwepo kwa kuwa wanashirikiana na wauzaji,” alisema Makonda.
Akawataka wote waliotajwa kuhusika na kuuza dawa za kulevya kufika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam kwa mahojiano.
Baadaye Makonda aliibuka na orodha ya majina 65 ya watu waliosema wanajihusisha na biashara hiyo. Miongoni mwao ni wafanyabiashara nguli, wabunge na viongozi wa dini.
Februari 13, mwaka jana, Makonda alimkabidhi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga, majina 97 ya watu waliosema ni wauzaji wakuu wa dawa za kulevya. Shughuli hiyo ilifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Kutokana na mapambano hayo kuonekana makali, Baraza la Viongozi wa Dini la Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, likaomba mamlaka husika zimwongezee Makonda ulinzi.
Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, alisema jitihada zinazoendelea dhidi ya dawa za kulevya ni mkakati wa kuokoa nguvukazi ya taifa.
“Tunampongeza kwa dhati Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kwa ujasiri mkubwa aliouonyesha kwa kuwa ameamua kujitoa muhanga kwa ajili ya taifa lake na watu wake na pia ameonyesha uthubutu,” alisema.
Baraza hilo lipo chini ya Tume ya Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania.
Sheikh Salum alisema matumizi ya dawa za kulevya yamekuwa ni kikwazo kikubwa cha maendeleo katika nchi na kupoteza nguvukazi ya taifa kwa kuwa waathirika wa dawa hizo ni vijana.
“Kutokana na ugumu wa kazi hii tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu ili ampe ulinzi na azidi kuwa na moyo wa ujasiri wa kupambana na maovu yote yanayoharibu sifa ya taifa na vijana wetu.”
Mapambano yake dhidi ya watu aliowatuhumu kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya yalizaa vita nyingine iliyomlenga kwa kumtuhumu kutokuwa na vyeti vya elimu anayodai kuwa nayo.
Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima, ambaye ni miongoni mwa waliotajwa na Makonda kwamba wanajihusisha na biashara ya dawa za kulevya, alijitokeza hadharani kupambana naye.
Miongoni mwa ‘makombora’ ya Gwajima ni kwamba Paul Makonda si jina halisi la Mkuu huyo wa Mkoa, bali jina lake ni Daudi Albert Bashite. Makonda hakupata kujitokeza kukanusha wala kukubali madai hayo.
Wakati akiandamwa na maswali kuhusu elimu yake, Rais John Magufuli, alikuwa ametangaza msako dhidi ya watumishi wa umma wenye vyeti feki. Mara kadhaa Rais Magufuli, alitangaza kutowavulia wote wenye vyetu hivyo, na hapo swali likawa kwanini hamgusi Makonda.
Oktoba 4, mwaka jana utetezi wa Rais Magufuli ukawa hadharani. Kwenye Mkutano wa 33 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) ulifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alimsifu kwa vita yake dhidi ya dawa za kulevya. Akawataka viongozi wengine waige mfano wa Makonda.
Akamtaka Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, awambie wakuu wa mikoa wote wajifunze kwa Makonda.
“RC wa Dar es Salaam alipojaribu kusema kuhusu dawa za kulevya kelele zikawa nyingi kweli, mara ooh hajasoma. Mimi hata kama hajui ‘a’ lakini kama anashika madawa ya kulevya huyo ni msomi mzuri,” alisema Rais Magufuli.