Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis, kwa mara nyingine ametoa kauli ya kuwaaga viongozi na waamini wake ulimwenguni kwamba kuna kila dalili za yeye kuachia ngazi hivi karibuni.
Katika mahojiano yake na Kituo cha Televisheni cha Mexico, Papa Francis amenukuliwa akisema; “Naamini huduma yangu kwa kanisa itakuwa fupi, nitajiuzulu kama ilivyofanya mtangulizi wangu na si kuliongoza kanisa maisha yangu yote.”
Katika mahojiano hayo yaliyorushwa muda mchache baada ya maadhimisho ya pili ya uteuzi wake, Papa Francis amesema kuwa hajali kuwa Papa lakini angependa kwenda matembezi nje ya Roma.
“Nahisi utumishi wangu utakuwa mfupi — miaka minne ama mitano. Hata miwili au mitatu. Miaka miwili imepita. Ni kitu ambacho si cha hisia za kawaida," anasema Papa, kwa mujibu wa tafsiri ya Vatican kutoka Kihispania.
“Nafikiri Mwenyezi Mungu ameniweka hapa kwa muda mfupi,” anaongeza Papa Francis, mzaliwa huyo wa Argentina ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 78 na muonekano wenye afya njema.
“Nina wazo ambalo Papa Benedict alikuwa nalo. Mtakumbuka mwaka 2013 Papa aliyepita; Papa Benedict amekuwa ni Kiongozi Mkuu wa Kwanza wa Kanisa Katoliki ndani ya miaka 600 kujiuzulu badala ya kuongoza hadi kifo.”
“Kwa ujumla, nafikiri kile ambacho Papa Benedict alifanya ni kufungua milango kwa Papa watakaomfuatia. Uamuzi wa Benedict usichukuliwe kama mtu pekee bali taasisi," anasema Francis.
Hata hivyo, amesema hapendezwi na wazo la kustaafu kwa kufuata umri ikiwamo la kufikisha miaka 80.
Katika mahojiano hayo yenye kurasa 17, Papa Francis amesema kitendo cha Papa wa Kwanza kutoka Latin America kumtaka kuwasemea wahamiaji na masikini ni kwa sababu mababu zake walitoka Italia kwenda Argentina kutafuta kazi.
“Watu hawakuhitajika na walilazimishwa kwenda kutafuta kazi kwingine,” anasema Francis, ambaye safari yake ya kwanza baada ya kuchaguliwa kuwa Papa ilikuwa nchini Italia katika visiwa vya Lampedusa kuhani maelfu ya wahamiaji waliopoteza maisha wakijaribu kuingia barani Ulaya.
"Francis siku za nyuma alihitaji mabadiliko zaidi ya taratibu za masoko, Francis ameukosoa utajiri usio wa haki, " amesema na kuongeza kuwa ni dhambi kumpatia mtu ujira usio wa haki au tajiri kutumia umasikini wa wengine kujinufaisha.
Kwa upande mwingine, Francis amesema, “Sijali kama ningeulizwa ningependa kuwa Papa. Jambo pekee ambalo ningependa ni uhuru siku moja. Ningependa nitoke bila ya kufahamika. Ningependa kwenda Pizzeria kupata pizza,” anasema.
Ameongeza; “Nazikumbuka na kuzitamani siku zile nilizokuwa Askofu huko Buenos Aires. Huko nilikuwa huru kuzunguka katika jiji hilo. Nilikuwa nikitalii.”
Papa Francis anguruma tena
Jamhuri
Comments Off on Papa Francis anguruma tena
Previous Post
‘Nchi yetu haina dini’