PAPA Francis yuko macho baada ya kukumbwa na matukio mawili ya ‘kushindwa kupumua’ siku ya Jumatatu alasiri, imesema Vatican.

Madaktari walilazimika kuingilia kati ili kuondoa kamasi kwenye mapafu ya Papa, imesema taarifa kutoka serikali kuu ya Vatican ya Holy See, ingawa wanasema alikuwa anajitambua wakati wote.

Papa mwenye umri wa miaka 88 ameanza tena matumizi ya mashine ya kupumulia ili kumsaidia kupumua, lakini bado yuko “macho, anajitambua na anatoa ushirikiano,” imesema Vatican.

Hii ni mara ya tatu hali ya Papa kubadilika ghafla tangu alipolazwa hospitalini siku 18 zilizopita kutokana na nimonia. Siku ya Ijumaa, Papa Francis alipata shida ya kupumua iliyohusisha kutapika, ilisema Vatican.

Mamia ya Wakatoliki walikusanyika nje katika uwanja wa St Peter’s Square Jumatatu jioni kumwombea Papa, wengi wao wakiwa wamebeba rozari.

Papa alilazwa hospitalini tarehe 14 Februari baada ya kupata matatizo ya kupumua kwa siku kadhaa. Alitibiwa mara ya kwanza kikohozi kabla ya kugunduliwa na nimonia katika mapafu yote mawili.

Vyanzo kutoka Vatikan vinasisitiza kwamba hali ya Papa bado ni ngumu na madaktari wake wako kwenye uangalifu.