Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, amegundulika ana ugonjwa wa homa ya mapafu katika mapafu yake mawili na hali yake sio nzuri.

Papa mwenye umri wa miaka 88, amekuwa akisumbuliwa na maambukizi ya mfumo wa upumuaji kwa zaidi ya wiki moja na kwa sasa anapatiwa matibabu katika hospitali ya Gemelli, iliyopo Roma, Italia.

Vatican ilisema kuwa, “Kipimo cha CT scan kilichofanywa kwa Papa kimeonyesha kuwa anasumbuliwa na nimonia ya pande zote mbili, ambayo inahitaji tiba ya ziada ya dawa.”

Aidha, vipimo vya maabara na X-ray ya kifua vinaonyesha hali ngumu ya afya ya Papa, lakini wataalamu wanachukua hatua stahiki za kumhudumia.

Hata hivyo, Vatican iliongeza kuwa, Papa bado anaendelea na shughuli za kiroho, akijikita katika kusoma, kupumzika na kusali.

Papa pia alitoa shukrani kwa waumini na wapenzi wake wote wanaomtumia salamu za pole, akiwataka waendelee kumuombea ili apate nafuu haraka.

Alikuwa amepanga kuongoza matukio kadhaa ya kidini katika wikiendi hii, ikiwa ni sehemu ya Mwaka Mtakatifu wa Kanisa Katoliki wa 2025, utakaodumu hadi Januari mwaka ujao.

Hata hivyo, kutokana na hali yake ya kiafya, matukio yote ya hadhara yaliyokuwa yamepangwa kwenye ratiba ya Papa, yamesitishwa hadi Jumapili ijayo.

Katika kipindi cha miaka 12 ya uongozi wake kama kiongozi wa Kanisa la Katoliki la Roma, Papa Francis amekuwa akipokea matibabu hospitalini mara kadhaa, ikiwemo mwaka 2023, alipolazwa hospitalini kwa siku tatu.