Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas akihutubia Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani ametoa wito wa kutipatia Israel silaha.

Mkutano huo wa mjini New York kwa kiasi kikubwa umetawaliwa na wasiwasi kuhusu vita vya Urusi nchini Ukraine, vita vya Israel na Hamas huko Gaza, na uwezekano wa kutanuka kwa mzozo wa Lebanon.

Rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas, ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuacha kuipatia silaha Israel: “Acheni uhalifu huu. Acheni sasa. Acheni kuua watoto na wanawake. Acheni mauaji ya halaiki. Acheni kupeleka silaha kwa Israel. Janga hili haliwezi kuendelea. Dunia nzima inahusika na kile kinachotokea kwa watu wetu huko Gaza na Ukingo wa Magharibi.”

Rais Abbas ambaye hata hivyo haliwakilishi eneo la Gaza amesema Wapalestina wanakabiliwa na moja ya uhalifu mbaya zaidi wa zama hizi na kusisitiza kuwa Israel inaendesha uhalifu wa vita kamili na mauaji ya kimbari. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anatarajiwa kulihutubia Baraza hilo leo Ijumaa.

Ama Mkuu wa serikali iliyo uhamishoni na inayotambuliwa kimataifa ya Yemen, Rashad al-Alimi, amesema kuvimaliza vita vya Gaza ni ‘hatua ya kwanza’ ya kuwatokomeza washirika wa Iran.

Katika hotuba yake kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, al-Alimi amesisitiza kuhusu umuhimu wa kuzuia mtiririko wa silaha za Iran na kuzuia vyanzo vya fedha kuelekea kwa waasi wa Houthi ambao wamechukua udhibiti wa sehemu kubwa ya Yemen huku akionya kuhusu jukumu la Iran katika kuyumbisha usalama wa Yemen na kanda nzima ya Mashariki ya Kati.