JAMHURI MEDIA

Tunaanzia wanapoishia wengine

Latest Posts

TCAA nako kwafukuta ufisadi

*Wakurugenzi wahariri Waraka wa Hazina

*Mbinu hiyo yawafanya walipane mamilioni

 

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), inakabiliwa na tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.

Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Fadhil Manongi, hadi wiki iliyopita bado alikuwa akiendelea na dhima za kiofisi licha ya muda wake wa kung’atuka kuwadia.

Wakati Manongi akijiandaa kuiacha ofisi hiyo, kumekuwa na malalamiko ya matumizi mabaya ya fedha miongoni mwa wakurugenzi ambao ni washirika wake.

Siku za Kipande bandarini zahesabika

*Ni baada ya kuthibitika anatumia vibaya jina la Rais Kikwete, Ikulu

*Amuagiza Mwakyembe amchunguze, wafuatilia kumtukana Balozi

* Mtawa, Gurumo nao wakana, Mwakyembe adaiwa kumwogopa

*Aendelea kukaidi maagizo ya Bodi, amng’oa rasmi aliyeomba kazi yake

Na Deodatus Balile

Siku za Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Mzee Madeni Kipande (58), kuendelea kuwa madarakani zinazidi kuyoyoma baada ya Rais Jakaya Kikwete kukerwa na tabia yake ya kutumia jina la Rais kuhalalisha matendo yake yenye kukiuka sheria za utumishi wa umma.

Habari za uhakika kutoka Ikulu na kwa baadhi ya mawaziri waandamizi, zinasema Rais Kikwete baada ya kupata taarifa za Kipande kutumia vibaya jina lake, alichukia na kuamua kumwita Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, na kumpa maagizo mazito.

Vituko vya DC Geita

Na Victor Bariety, Geita

Sehemu ya kwanza ya makala hii ilielezea vituko vinavyofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Geita, Omari Manzie Mangochie, vikiwamo vya kuzuia ujenzi wa mnara wa simu za mkononi na kutangaza vita na waandishi wa habari. Sasa endelea na sehemu hii ya pili.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Omari Manzie Mangochie ambaye anatajwa kama kiongozi anayezalisha migogoro na kukwamisha shughuli za maendeleo wilayani hapa. Anatuhumiwa pia kumng’oa Mwenyekiti wa Chama chake cha Mapinduzi (CCM) wa kijiji cha Mnyara, hivyo kuwapatia wapinzani mwanya wa uongozi.

Katika tuki hilo la aina yake, Mangochie baada ya kumvua uongozi Mwenyekiti wa Kijiji cha Mnyara, Makoye Roboyanke, aliitisha uchaguzi mdogo na kuwaamuru wananchi kupiga kula za wazi mgongoni mwa wagombea kinyume cha taratibu za uchaguzi.

Kitendo hicho kilizua tafrani kubwa kwani pamoja na wananchi kukubali matakwa ya Mkuu huyo wa wilaya kwa kuwachagua viongozi wao nyuma ya migongo, CCM kilichokuwa kimeweka mizizi eneo hilo kilibwagwa na kusababisha msimamizi wa uchaguzi kukimbia na matokeo ili kujinusuru na kipigo kutoka kwa wananchi hao.

Inadaiwa kuwa uamuzi huo wa Mangochie wa kumvua uongozi kada huyo wa CCM bila kufuata utaratibu umesababisha wananchi wa eneo hilo kukihama chama hicho tawala na kujiunga na vyama vya upinzani ambavyo hapo awali havikuwa na nguvu kwenye kijiji hicho ambapo wameiomba Serikali kuingilia kati mgogoro huo.

Akizungumza na JAMHURI kijijini hapo hivi karibuni, mwenyekiti huyo wa kijiji alisema uamuzi huo wa Mangochie umemdhalilisha na umeonesha ni jinsi gani asivyoheshimu vikao halali vya CCM.

Anahitajika Sokoine mwingine 2015

Mengi mazuri yanayomhusu Waziri Mkuu wa zamani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Edward Moringe Sokoine, yamesemwa na yanaendelea kusemwa.

Kwa Mtanzania yeyote wa kweli, kamwe hatachoka kusikia mengi yaliyofanywa na Sokoine wakati wa uongozi wake.

Miaka 30 sasa tangu alipoaga dunia, shujaa huyu hajulikani kwa vijana wengi wa Tanzania. Safu hii ni fupi mno, kiasi kwamba haiwezi kumweleza japo kwa nukta mtu huyu hata akaeleweka kwa vijana wengi.

Itoshe tu kuwaasa vijana kuyasaka kwa udi na uvumba maandiko yanayomhusu shujaa huyu wa Tanzania, ambaye mfano wake kwenye nafasi ya Waziri Mkuu, haujapatikana.

Licha ya wengi kumzungumza Sokoine, hiyo haitoshi kutufanya nasi tusiweke neno wakati huu wa kumkumbuka.

Moringe alikuwa kipenzi cha Watanzania wengi, hasa makabwela. Alipendwa na watu wa jinsi, hali na rika zote. Hakuwa na makuu. Alikuwa mcha Mungu wa kweli. Hakuwa kiongozi wa kupayuka-payuka, bali alikuwa mpole, msikivu na mwenye kusimama katika ukweli na haki. Uwajibikaji na uadilifu ndiyo uliokuwa msingi mkuu wa Sokoine.

KAGAME NI MTIHANI Viongozi Maziwa Makuu waufanye kwa Uangalifu

Ni wazi kwamba nafasi inayoshikiliwa na Uganda na Rwanda katika roho ya uchumi wa Marekani na Uingereza ni kubwa kuliko nchi yoyote ile katika eneo la Maziwa Makuu kwa sasa.

Hakika Marekani na Uingereza wamelipa gharama kubwa kutengeneza miundo ya kiserikali, nguvu za kijeshi na saikolojia za kisiasa zinazoongoza nchi hizo miaka ya karibuni.

Watu walijiuliza maswali mengi kunako miaka ya tisini juu ya nguvu za Museveni na baadaye kasi ya RPF kuitwaa Rwanda, nchi ambayo ilikuwa imeanza kuimarika kama zilivyokuwa nchi nyingine barani Afrika. Hasa nchi ambazo zilikuwa zimeishi kwa amani toka uhuru mpaka miaka hiyo.

Mwanzoni mwa miaka ya tisini Rwanda ilikuwa na fedha yenye thamani kubwa. Ilikuwa pia na msaada mkubwa wa kijeshi kutoka Ufaransa. Raia wake walikuwa na kipato kizuri cha kutosha. Ilikuwa thabiti.

Matatizo yaliyokuwapo Rwanda miaka ya tisini yaliakisi matatizo yaliyokuwapo kwingineko barani Afrika kama vile vita za wenyewe kwa wenyewe, uongozi mbovu na uamuzi usiyo na tija, ufisadi wa wachache, upendeleo wa kikabila (Wahutu), undugu (nepotism) na zaidi suala la wakimbizi.

Wakimbizi wa Rwanda miaka ya ‘tisini mwanzoni’ walikuwa ni Watutsi waliokuwa wameikimbia nchi baada ya mapinduzi mwaka 1959 yaliyoiondoa dola ya mfalume Kigeri V muda mfupi kabla ya uhuru. Rwanda haikutofautiana na nchi nyingine nyingi barani Afrika.

Ukiilinganisha Rwanda ya sasa ya Kagame ambayo wapinzani wake wanaviziwa na kuuawa hata wakiwa nje ya nchi! Rwanda ambayo wakati wa uchaguzi raia wanapotea kimya kimya na baadhi kuokotwa wakiwa mizoga!

Hotuba ya Lissu iliyosababisha TBC1 ‘izimwe’

Aprili 12, mwaka huu, Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Tundu Lissu aliwasilisha maoni ya Wajumbe walio wachache katika Kamati Namba Nne kuhusu sura ya kwanza nay a sura ya sita ya Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wakati akiwasilisha, Televisheni ya Taifa (TBC1) ilikata matangazo yake katika kile kilichotafsiriwa na wengi kuwa ni kuuepusha umma kupata maoni ‘makali’ yaliyomo kwenye hotuba ya Lissu. Kwa kuzingatia haki ya wananchi ya kupata habari, JAMHURI inawaletea hotuba hiyo neno kwa neno. Endelea

UTANGULIZI

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Sura ya Kwanza na Sura ya Sita ya Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (‘Rasimu’) ndizo msingi ambao Rasimu yote imejengwa juu yao. Wakati Sura ya Kwanza inagusa suala la muundo wa Muungano katika ibara moja tu kati ya ibara tisa, Sura yote ya Sita inahusu ‘Muundo wa Jamhuri ya Muungano.’ Suala la Muungano na hasa Muundo wake limetawala mjadala wa kisiasa na kikatiba wa Tanzania kwa zaidi ya miaka thelathini. Ndio maana katika waraka wake wa siri kwa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (‘CCM’), Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya chama hicho imetamka kwamba “muundo wa Muungano ndiyo moyo wa Rasimu na ndiyo unaoamua ibara nyingine zikae vipi.”

Suala hili pia limetawala mchakato wa Katiba Mpya tangu ulipoanza miaka mitatu iliyopita. Kama alivyosema Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Joseph Sinde Warioba wakati wa kuwasilisha Ripoti ya Tume yake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar tarehe 30 Disemba, 2013: “Moja ya mambo ambayo yamejadiliwa sana na kwa hisia kali tangu Rasimu ya awali ilipotolewa … ni Muungano wa Tanzania. Jambo kubwa limekuwa juu ya muundo wa Muungano.”

Umuhimu wa suala hili unathibitishwa pia na uamuzi wa Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalum kuelekeza kwamba Kamati zake Namba Moja hadi Kumi na Mbili zianze kujadili Sura ya Kwanza na ya Sita ya Rasimu. Haya ni maoni ya wajumbe walio wachache wa Kamati Namba Nne juu ya Sura hizi mbili.