Mahakama ya New York, Marekani imetupilia ombi la Msanii, Sean “Diddy” Combs la kutaka kuachiliwa kwa dhamana na kuishi katika nyumba binafsi (Appartment) wakati akisubiri kesi inayomkabili ya mashtaka ya usafirishaji wa Binadamu kwa ajili ya unyanyasaji wa kingono kuanza kusikilizwa mwakani 2025.

Jaji anayesimamia kesi hiyo aitwaye Arun Subramanian amesema hakuna masharti yanayoweza kuhakikisha usalama wa Jamii kutokana na tabia za P Diddy alizofanya katika kesi zinazomkabili huku Msanii huyo akihofiwa kuwa endapo atapewa dhamana atawatisha Mashahidi.

Mawakili wa Didy walitaka Mteja wao aachiliwe kwa dhamana ya dola milioni 50 (zaidi ya shilingi bilioni 125 za Kitanzania) na kugharamia ulinzi pamoja na kuishi katika nyumba binafsi (Appartment) lakini ombi hilo limetupiliwa mbali na Mahakama huku Msanii huyo akiendelea kusalia gerezani.

Didy Ambaye alikamatwa Septemba mwaka huu na kukana mashtaka yote yanayomkabili, kwa sasa anazuiliwa katika gereza la Metropolitan Detention Center, Brooklyn huko New York.


Serikali inasisitiza kuwa kuachiliwa kwake kunaweza kuhatarisha usalama wa Mashahidi na jamii.

Aidha Wakili wa Diddy, Mac Agnifilo amesema watapigania kesi hiyo kwa kadri watakavyoweza na mwishowe Diddy atadhihirika kuwa hana hatia.

Kesi hiyo imepangwa kuanza kusikilizwa rasmi mwezi Mei mwaka 2025.