*Yazifadhili asasi kuvuruga amani Loliondo

*Yazichotea mamilioni kufanikisha vurugu


Shirika la Misaada la Kimataifa la Oxfam limejiingiza kwenye ufadhili wa vikundi na asasi za kiraia, zinazozua na kuchochea mgogoro kati ya Serikali na wafugaji wa jamii ya Kimaasai katika Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha.

Kujiingiza kwa Oxfam ni juhudi za asasi za Tanzania zilizo na baadhi ya raia wa kigeni, kuhakikisha kuwa Loliondo haitawaliki. Pia ni mwendelezo baada ya kukwama kwa baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya Ulaya ambao mwaka jana walijiingiza huko kinyemela hata bila kuitaarifu Serikali ya Mkoa wa Arusha.

 

Habari za uhakika zilizopatikana kutoka Arusha zimesema kwamba shirika hilo limetoa mamilioni ya shilingi zilizowezesha baadhi ya asasi hizo kukutana mjini Arusha wiki iliyopita. Fedha hizo, pamoja na kuwawezesha viongozi na wanachama wa asasi hizo, zinatumika pia kulipia matangazo na propaganda katika vyombo vya habari.

 

Asasi zilizo katika mkakati huo ni mtandao wa wanaharakati wa haki za binadamu (FEMA CT), mtandao wa mashirika yanayotetea haki za wafugaji, wawindaji na wachuma matunda nchini (PINGO’s Forum), mtandao wa utetezi wa masuala ya ardhi (TALA), na shirika lisilo la kiserikali lililopo Ngorongoro (NGONET).

 

Asasi hizo kwa mara ya kwanza kwenye tamko lake, kwa vyombo vya habari mwishoni mwa wiki, zimetamka wazi kuunga mkono harakati za kuichafua Tanzania zinazoendeshwa kwenye mtandao.

 

“Kutokana na hayo, sisi mashirika yanayojishughulisha na utetezi wa haki za binadamu nchini Tanzania, tunaunga mkono kampeni za mtandao wa kimataifa wa Avaaz,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

 

Kufanyika kwa mkutano wa pamoja wa asasi hizo kumekuja baada ya hivi karibuni Rais wa Oxfam Ireland, Monica Gorman, na viongozi wengine wa shirika hilo kuzuru Ngorongoro bila kuwataarifu viongozi wa Serikali ngazi ya mkoa.

 

Akiwa Loliondo, Gorman alijaribu kuibua tatizo “lisilokuwapo” na kutaka wananchi wanaoishi hapo wasibughudhiwe. Kimsingi anapinga kusudio la Serikali ya kuandaa Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi katika vijiji vya Loliondo. Mpango huo umelenga kuainisha maeneo ya malisho ya mifugo, maeneo ya uhifadhi wanyamapori, maeneo ya kilimo, na shughuli nyingine za kijamii.

 

Akiwa katika Kijiji cha Arash kilicho karibu na Loliondo, aliwataka wanavijiji wawe makini katika kuingia mikataba na kampuni kwa maelezo kwamba watapoteza ardhi yao.

 

Wengine waliokuwa kwenye msafara huo ni Mkurugenzi Mkuu wa Oxfam, Jim Clarken; Mwenyekiti wa Kamati ya Uhusiano wa Mambo ya Nje wa Bunge la Ireland, Jim Wells, na Pat Breen, ambaye ni Mbunge.

 

Mwenyejiti wa Arash, Kiaro Orminis, aliueleza ujumbe huo kwamba kuna matatizo ya ardhi katika eneo hilo, hasa unaohusisha Kijiji cha Malambo na kampuni ya uwindaji wa kitalii ya Ortello Business Corporation (OBC).

 

Kwa muda sasa, mgogoro katika eneo la Loliondo ulikuwa umetulia hasa baada ya wananchi kuelimishwa juu ya umuhimu wa kupanga matumizi bora ya ardhi.

 

Utulivu huo umekuwa ukiathiri mapato ya asasi zinazojitanabaisha kuwa zinawatetea wafugaji, ilhali zikiwa hazifanyi juhudi za kutosha katika kuwasaidia wananchi hao.

 

Kampeni ya hivi karibuni ilipamba moto kwenye mtandao wa Avaaz, ikidai kwamba Serikali ilikuwa mbioni kuwahamisha wafugaji wa Kimaasai kutoka Serengeti. Taarifa hiyo ilipingwa vikali na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii.

 

Taarifa ya Serikali ya Agosti 15

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Khamis Sued Kagasheki, amekanusha uvumi unaosambazwa na shirika moja kupitia mtandao wake wa AVAAZ.org kuwa Watanzania wa jamii ya Kimaasai wapatao 48,000 watahamishwa kutoka eneo lao (la Serengeti), kupisha wafalme kutoka Mashariki ya Kati ili walitumie eneo hilo kwa uwindaji wa simba na chui.

 

Taarifa hiyo iliyosambazwa na mtandao huo imewataka watu kutoka duniani kote kujiorodhesha ili wafikie angalau 150,000, ili kumshinikiza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuacha kusaini mkataba utakaofanya uhamisho huo utekelezwe.

 

Waziri Kagasheki amesisitiza kuwa uvumi huo si wakweli na hauna msingi wowote kutokana na sababu zifuatazo:

 

Kwanza, hatua kama hii haiwezi kuchukuliwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Hifadhi ya Serengeti maana hakuna watu wanoishi ndani ya hifadhi hiyo. Pia kitendo hicho hakijapangwa kufanyika katika Wilaya ya Serengeti iliyoko mkoani Mara.

 

Pili, hata kama taarifa hiyo ilimaanisha Wilaya ya Serengeti mkoani Mara bado si yakweli maana wilaya hiyo haina idadi ya Wamaasai wanaofikia jumla ya 48,000.

 

Tatu, ndani ya ya Hifadhi ya Serengeti hakuna eneo lolote lililotengwa kwa ajili ya wafalme wa Mashariki ya Kati, ili waweze kulitumia kwa uwindaji wa simba na chui.

 

Nne, habari hizo si za kweli maana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hahusiki kabisa na ugawaji wa vitalu vya uwindaji popote pale nchini. Hii ni kazi ya Wizara ya Maliasili na Utalii, na Wizara haijafanya hivyo katika eneo tajwa.

 

Pamoja na ufafanuzi huo, Waziri Kagasheki amewaasa watu waliojiorodhesha na wanaotarajia kujiorodhesha, kuwa wamepotoshwa, hivyo wanatakiwa wasisaini kubariki kitu ambacho hawakijui wala hakipo.