Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, ametoa rai kwa Mamlaka pamoja na Jamii, kuzingatia Utambuzi wa Ardhi, ili kuepusha dhulma na migogoro, juu ya raslimali hiyo muhimu nchini.
Mheshimiwa Othman ametoa rai hiyo mapema leo, alipokutana na watendaji na wananchi mbalimbali, huko Makaani Vitongoji alikofika kuwasikiliza malalamiko yao juu ya madai ya kuporwa na kulazimishwa kuondoka katika maeneo wanayoishi pamoja na tishio la athari za mazingira.
Amesema licha ya mantiki kwamba eneo hilo linakabiliwa na changamoto nyingi za muda mrefu, na ambazo zinahitaji juhudi za makusudi za utatuzi wa pamoja, bali chimbuko la yote ni kukosekana Utaratibu sahihi wa kutambua ardhi.
“Tatizo na hitajio kubwa ni kuwepo chombo cha kusimamia matumizi ya ardhi kama inavyohitajika katika miongozo ya kisheria, na kwamba kutofuatwa kwake dhulma ya raslimali hii itaendelea katika maisha yote”, amebainisha Mheshimiwa Othman akibainisha Mapendekezo ya Takriban Sheria Saba (7) zilizopitishwa mnamo Mwaka 1989, ikiwemo ya Utambuzi wa Ardhi, ambayo amesema bado haijafuatwa.
Aidha, ameongeza kwa kusema, “migogoro itaendelea kuchipua kila siku, madhali hapajakuwepo utambuzi wa ardhi; na kama tunataka kutambua umiliki wa ardhi, kwanza tuwahalalishie wananchi kile walichoharamishiwa katika ardhi yao ya haki na halali”.
Ameeleza kuwa tatizo ni la Serikali na mamlaka zake ambapo ni kama kwamba zimeshindwa katika usimamizi wa ardhi kwa utaratibu wa haki, licha ya kwamba inavurumisha lawama kwa wananchi.
“Ukweli ni kwamba kwa kuzingatia maslahi binafsi hata kwa baadhi ya viongozi na watu wengine wenye mamlaka, kinachodhihiri ni kudhulumu na wengi kudhulumiwa haki ya ardhi, na hata baadhi yawakati kwamadai ya kukosa karatasi za nyaraka ambazo wengine wamezipata ili kutenda dhulma”.
Akisisitiza juu ya mkanganyiko katika upatikanaji na utoaji wa nyaraka za ardhi , Mheshimiwa Othman amesema, “tatizo la Nchi yetu ni kwamba kila mmoja ni bosi wa ardhi; haijulikani ni Sheha, Mkurugenzi au yoyote yule maana kila mtu ana mamlaka na anatoa maamuzi ya ardhi”.
Hivyo amesema kunahitajika utaratibu sahihi wa kumiliki ardhi, ili kuepusha dhulma na migogoro, na pia kuwaongoza wananchi kumiliki raslimali hiyo katika misingi ya haki.
Pamoja na rai hizo, Mheshimiwa Othman amewahakikishia wananchi hao kwamba Serikali itakabiliana na changamoto hiyo kwa kuzingatia misingi ya haki, sheria na utaratibu unaostahiki kwakuhusisha sekta zote husika.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Bw. Mattar Zahor Masoud, amefahamisha kuwa Mamlaka yake inajitahidi kukabiliana na malalamiko ya wananchi, zikiwemo changamoto za watu wa Kijiji hicho licha ya kwa kiasi kikubwa kwa sasa ndiyo kwanza zimeibuka na zinahitaji busara ya namna ya kukabiliana nazo.
Akifahamisha azma ya Mkoa wake katika kuzikabili changamoto hizo, Bw. Mattar amesema, “Dhamira yetu na dhamira ya Serikali hii ya Awamu ya Nane siyo kudhulumu wala kuwakosesha wananchi haki zao, bali la msingi ni kukaa na kushirikiana pamoja na kufuata taratibu”.
Hivyo, ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na Ofisi yake pindipo zikijitokeza changamoto, ili kila mtu aweze kuendelea na maisha kwa kuzingatia haki.
Akitolea ufafanuzi baadhi ya Malalamiko ya Wananchi, juu ya madai ya ardhi yanayozunguka pia maeneo ya Vitongoji Kwareni, Liko la Vumba na Kimbu-Sadi, Afisa wa Mazingira Wilaya ya Chake-Chake kisiwani Pemba, Bw. Mwalim Khamis Mwalim, amesema kutokana na uhalisia kwamba maamuzi ya kuipima, kuitumia na kuihaulisha ardhi kwa watumiaji wakiwemo wawekezaji kunahitaji maamuzi ya Sekta Jumuishi, sambamba na kuwashirikisha kikamilifu wananchi, wamiliki wa maeneo hayo walistahiki kushauriwa, kufidiwa na pia kuongozwa juu ya utaratibu wa kulitumia tena kwaajili ya uzalishaji eneo ambalo sasa linatumika kuchimba mawe, kokoto na raslimali za namna hiyo.
Wakiwasilisha kilio chao kwa Serikali mbele ya Mheshimiwa Othman, Wakaazi wa Kijiji hicho, Bw. Saleh Nassor Juma, Bw. Said Ali Burhan, Bw. Faki Hamad Faki, Khamis Ali Khamis, na Bw. Hamad Khamis Maalim, wamesema wanachokishuhudia sasa ni madhila yanayotokana na ugumu wa maisha kufuatia kulazimishwa kuondoshwa katika ardhi yao muhimu kwaajili ya kilimo, makaazi na mifugo, tangu asili na zama, pahala ambapo wao na wazee wao wamezaliwa.
“Ardhi yetu imevamiwa, inachukuliwa na tunalazimishwa kuondoka kama mnavyoona, tunahisi hii ni kusaliti hata ile Sera na Miongozo ya Mzee Karume ya kwamba wananchi wapate ahweni ya kumiliki pahala pa maisha yao”, amelalama akiweka msisitizo Bw. Saleh.
Katika Mkutano huo, Mheshimiwa Othman ameambatana na Viongozi na Watendaji mbalimbali wa Serikali na Vyama vya Siasa wakiwemo Maafisa Wadhamini wa Wizata ya Mawasiliano na wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kisiwani Pemba, Bw. Ibrahim Saleh Juma na Bw. Ahmed Abubakar Mohamed; Mratib wa ACT-Wazalendo hapa, Mhe. Said Ali Mbarouk, na Sheha wa Shehia ya Vitongoji, Bw. Salim Ayoub.
Mheshimiwa Othman amekamilisha Ziara yake ya Siku Nne kisiwani Pemba, kwaajili ya Shughuli mbalimbali za Chama, Jamii na Serikali, akiambatana na Mke wake, Mama Zainab Kombo Shaib