Kikwete

Rais Jakaya Kikwete

Ikulu imeanza kuorodhesha watumishi wa umma wanaopaswa kufukuzwa kazi na kufunguliwa mashitaka, kutokana na kuhusishwa na ufujaji fedha za umma kama ulivyoainishwa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Habari za uhakika kutoka Ikulu zinasema kazi hiyo imeanza ikiwa ni utekelezaji wa kauli ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa kwa Watanzania wiki iliyopita, wakati akitangaza Baraza la Mawaziri.

Rais Kikwete alisema kuanzia sasa mawaziri wanapowajibishwa ni lazima walioshiriki kuwafikisha hapo nao wawajibishwe.

Aliwataja wahusika kwenye kuwajibishwa huko kuwa ni makatibu wakuu, wakurugenzi, menejimenti na bodi za mashirika, idara na taasisi zote za Serikali.

Kwa msimamo huo, walio kwenye orodha ya kuwajibishwa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Joyce Mapunjo. Huyu anatuhumiwa kumbeba Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekelege. Kwa kumbeba Ekelege, Dk. Cyril Chami aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara amepoteza nafasi hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Ekelege, yupo kwenye orodha ya watakaowajibishwa licha ya juhudi za dakika za mwisho za kutaka kujionyesha dhidi ya tuhuma za utafunaji wa mabilioni ya fedha kutokana na ukaguzi feki wa magari nje ya nchi.

Ekelege anatuhumiwa pia kuruhusu matumizi ya vyakula na vifaa visivyofaa kwa matumizi ya binadamu, mitambo, magari, mafuta ya ndege na vifaa mbalimbali.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Ephraim Mgawe, naye yupo kwenye orodha hiyo hasa baada ya kuhusishwa na mpango wa kuwaleta Wachina ili wajenge gati mbili katika Bandari ya Dar es Salaam kwa mkataba wa dola milioni 500. Kashfa hiyo imechochea kung’olewa kwa Waziri Omari Nundu na Naibu wake, Athuman Mfutakamba.

Kwenye sakata hilo anaguswa pia Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Mhandisi Omar Chambo, ambaye naye kuna tetesi kwamba anaweza kuwajibishwa.

Vigogo waliojihusisha na ujenzi wa chumba cha watu maarufu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, kwa gharama ya Sh bilioni 11 nao wapo njia moja, hasa baada ya kuonekana kuwa kiasi cha fedha kilichotumika ni kikubwa mno.

Mkurugenzi wa Bohari ya Dawa (MSD), Joseph Mgaya, kuna dalili kwamba hawezi kunusurika hasa kutokana na uzembe ulioisababishia Serikali hasara ya Sh zaidi ya bilioni tano kutokana na kuharibika kwa dawa katika maghala yake.

Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), naye yupo kwenye mkondo huo akiwa na mwenzake wa Chuo Kikuu cha Mkwawa Iringa, Profesa Philemon Mushi, ambaye imebainishwa kuwa kuna mamilioni ya fedha za mikopo ya wanafunzi yaliyotafunwa.

Hali kama hiyo inaweza kuwakumba pia Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, ambaye naye imebainika kuna mishahara hewa ya mamilioni imeliwa, ingawa kwenye maelezo inaonekana aliwataarifu Hazina na wakashindwa kurekebisha dosari hiyo.

Kadhalika, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Profesa Idrisa Kikula, anaweza kujikuta matatani kutokana na dosari kadha wa kadha za kiuongozi.

Mkuu wa Chuo cha Ubaharia Dar es Salaam (DMI)naye inaonekana nafasi yake ya kupona ni ndogo kutokana na matumizi mabaya ya mali za chuo ukiwamo upotevu wa kompyuta zenye thamani ya mamilioni ya shilingi.

Katika kumbakumba hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Ramadhan Kijjah anaonekana kuwa kwenye wakati mgumu kutokana na ‘madudu’ mengi aliyoyabariki.

Anatuhumiwa kujihusisha moja kwa moja kwenye uuzaji wa mali za umma vikiwamo viwanja na majengo ya Serikali. Alishiriki kikao na baadaye kutoa uamuzi wa kampuni ya SSS kulipwa Sh zaidi ya milioni 900 kutokana na kunyimwa fursa ya kununua majengo ya TMSC yaliyopo katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Maimuma Tarishi, yupo kwenye orodha ya walio katika hatari ya kupoteza kazi.

Nje ya yale yaliyoainishwa kwenye Ripoti ya CAG na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, Tarishi anatuhumiwa kutotoa ushirikiano kwa Kamati hiyo.

Iliilazimu Kamati kuitaarifu Ikulu ili imlazimishe aipe Kamati hiyo ushirikiano, jambo lililotekelezwa kwa msaada wa vyombo vya usalama.

Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu waliotafuna kiasi cha Sh bilioni sita, hawatapona katika kumbakumba hiyo kwani nao ni miongoni mwa viongozi mbalimbali nchini watakaowajibishwa.