Operesheni za usalama zinazofanywa kwa msaada na jamii zimedhoofisha uwezo wa kundi la wanamgambo la al-Shabaab kufanya mashumbulizi nchini Kenya. Tangu Februari 17, wakati wanachama wa al-Shabaab waliposhambulia kituo cha polisi katika eneo la Jarajila mjini Garissa, na kumuua polisi mmoja, hapajatokea mashambulizi yoyote yanayohusishwa moja kwa moja na al-Shabaab katika eneo hili, Kamishna wa Jimbo la Kaskazini Mashariki, James ole Seriani, alisema mwishoni mwa wiki.
Kupungua kwa mashambulizi ya magurneti na ya kutega ardhini huko Kaskazini Mashariki mwa Kenya yaliyohusishwa na wanamgambo wa al-Shabaab, kunatokana na kuongezeka kwa ulinzi, ushiriki wa jamii na migawanyiko ndani ya kundi hilo. “Kuna kuongezeka kwa hatua za usalama na ukusanyaji wa taarifa za kiintelijensia ambako kumezizuia operesheni na vitisho vya al-Shabaab kwa usalama wetu. Wakazi nao wanashiriki kwa kujitolea kutoa taarifa baada ya kushuhudia mashambulizi mabaya. Kati ya Oktoba na Januari kulikuwa na angalau mashambulizi mara moja kila wiki. Katika Februari, mashambulizi hayo yalitenganishwa sana,” alisema.
Tangu Oktoba 2011, vikosi vya jeshi la Kenya vilipoanzisha Operesheni Linda Nchi kuwafukuza al-Shabaab nje ya Somalia hadi katikati ya Februari, watu 22 waliuawa na zaidi ya 50 kujeruhiwa katika eneo hilo wakiwamo raia, alisema Seriani na kuongeza: “Kati ya waliouawa alikuwa ni mtoto wa miaka minane, baada ya gurneti kurushwa katika uwanja wa kanisa Novemba 11 mjini Garissa.”
Al-Shabaab wapoteza uungwaji mkono, ufadhili wa kifedha
Meja mstaafu Bashir Hajji Abdullahi, anayefanya kazi kama mshauri wa masuala ya usalama na mchambuzi nchini Kenya, alisema al-Shabaab imepoteza uungwaji mkono mdogo iliokuwa nao kaskazini mashariki ya Kenya, wakati ilipoelekeza mashambulizi yake kwa raia.
Abdullahi alisema migogoro ya ndani ya uongozi wa al-Shabaab kuhusu itikadi na mkakati, imeathiri pia uratibu wake na kuugawa uungwaji mkono waliokuwa nao.
Hivi karibuni, mmoja wa wanapropaganda wakuu wa al-Shabaab, mzaliwa wa Marekani, Omar Hammami, anayefahamika pia kama Abu Mansoor al-Amriki, alituma video kwenye mtandao akisema kwamba maisha yake yako hatarini kutoka kwa wanachama wenzake wa al-Shabaab.
“Maeneo yaliyokombolewa ya Somalia yamechukua jukumu kubwa. Hii kwa sehemu fulani ni kwa sababu KDF inaingia katika maeneo zamani yaliyokuwa yanadhibitiwa na al-Shabaab, inatoa huduma za misaada kama vile chakula na huduma za afya, ambavyo vimekuwa muhimu sana katika kuziteka nyoyo za wananchi na akili za wenyeji,” Abdullahi alisema.
Alisema al-Qaeda katika Ghuba ya Uarabuni ilikuwa inatoa silaha kwa wanamgambo wa al-Shabaab huko Yemen, lakini nchi sasa iko katika migogoro ya ndani. “[Al-Qaeda huko] Yemen wana matatizo yao wenyewe ya kuyashughulikia na imegeuzia misaada yake kutoka kwa al-Shabaab na kuiweka katika matumizi ya kupigana na uongozi wa Yemen,” alisema.
David Ochami, mwandishi wa habari anayesimamia shughuli za kikundi cha wanamgambo katika Mashariki ya Kati na Pembe ya Afrika, alisema al-Shabaab wamepoteza sehemu kubwa ya uwezo wao, hasa katika eneo la Gedo – wamepoteza viongozi wao kutokana na mashambulizi ya anga. “Kushambulia raia ni kitendo cha woga na kukata tamaa,” Ochami alisema.
“Ripoti zinaonyesha kuwa wengi wa wapiganaji wa kigeni ndani ya safu zao ama wanatoroka au wamekuwa kizuizini [na al-Shabaab] kwa tuhuma kwamba ni wapelelezi.”
Hata hivyo, Ochami alitahadharisha dhidi ya matatizo ya usalama. “Kudhoofika kwa shughuli za al-Shabaab haina maana kuwa hawapangi chochote,” alisema.
“Magaidi wanajulikana kwa kuwa na subira ya muda mrefu kabla ya utekelezaji wa mashambulizi makubwa.”
Uwezo [wa Al-Shabaab] wa kuanzisha mashambulizi katika miji ya mpakani na Kenya, ulipungua wakati walipofukuzwa Somalia katika miji ya Dobley, Burhache, Gerille na Ras Kamboni.
“Wengi wa wapiganaji waliong’olewa kutoka Baidoa huko Bay na Beledweyne huko Hiiraan, wamekimbilia kusini pamoja na vifaa vya kijeshi na bado ni tishio,” Ochami alisema.
“Tunaona kuongezeka kwa mashambulizi katika sehemu ya Gedo, hasa Garbaharey, kulitokana na ongezeko hili jipya. KDF, vikosi vya kimataifa na hata vyombo vya Kenya vya usalama vina haja ya kuwa makini zaidi kuhusu changamoto hii mpya.”
Mkuu wa Wilaya ya Wajir-Mashariki, Kennedy Nyaiyo, alisema kutokana mashambulizi, Serikali ilifanya mikutano ya kimkakati na wananchi.
“Tunafanya kazi na makundi binafsi kama vile masheikh, maimamu, wanawake, vijana na viongozi wa kisiasa na kutaka msaada wao. Huwa tunayaomba yalinde amani na utulivu uliokuwapo katika eneo hili kabla ya mashambulizi ya al-Shabaab. Tunawataka kutoa habari muhimu juu ya kuwapo kwa mashabiki miongoni mwa jamii na mipango yao,” Nyaiyo alisema.
Nyaiyo alisema waliokamatwa wako nje kwa dhamana ya polisi wakati uongozi husika unakusanya ushahidi. “Wanawajibika kutoa taarifa kwa kila wiki. Tunatarajia matokeo ya wakemia wa Serikali huko Nairobi, kuongoza mashtaka mwezi Aprili kuhusu wale waliokamatwa kwa kumiliki kemikali hizo,” alisema. Abdurahaman Abdi Ahmed (47), ambaye ni Mkenya mwenye asili ya Somalia anayeishi Wajir, alisema kwamba Mkoa wa Kaskazini Mashariki una uzoefu wa miongo kadhaa ya vita na hauko tayari kuwaficha watu wanaotaka kuvunja amani.
“Kukosekana kwa amani kumeufanya mkoa wetu kuwa na maendeleo duni, na wakati al-Shabaab walipoanza kueneza ghasia, sisi tuliungana ili kutowaruhusu [kufanikiwa katika malengo yao],” Ahmed alisema. “Ndiyo maana sisi huwa tunaviambia vyombo vya usalama – ili kutoa onyo kwamba hakuna mwanamgambo wa al-Shabaab atakayevumiliwa miongoni mwetu.”
Waziri wa Nchi wa Maendeleo ya Kaskazini ya Kenya na sehemu nyingine za Ardhi Kame, Mohamed Elmi Ibrahim, alisema wananchi wanapaswa kuwa na hofu ya kutowaamini wanamgambo wa al-Shabaab.
“Wahalifu hawa hawa wanaweza kuwageuka, kwa vile wao ni mashahidi wakati baadhi ya wananchi wanaathirika kwa mashambulizi. Wanamgambo wa al-Shabaab hawana marafiki wa kudumu, na wakazi wanapaswa kuwakwepa kuwa na urafiki nao,” alisema.