Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Tunduru

Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma imeendesha operesheni maalumu ya nyumba kwa nyumba ya kuwasaka wazazi wasiopeleka watoto shule licha ya kuchaguliwa kuingia kidato cha kwanza mwaka huu.

Akizungumzia operesheni hiyo mkuu wa wilaya hiyo Julius Mtatiro, amesema kuwa wazazi 763 wamekamatwa baada ya kutolewa siku 14 za watoto hao kuripoti shuleni na kushindwa kufanya hivyo.

“Tumefanya operesheni ya nyumba kwa nyumba na kuwakamata wazazi na walezi wasiopeleka watoto wao waliochaguliwa kuanza masomo ya kidato cha kwanza mwaka huu kwani tulitoa siku 14 za kupeleka watoto shule kwa hiari lakini bado wazazi hao walishindwa kufanya hivyo,” amesema.

Mtatiro amesema kuwa kabla ya operesheni hiyo kulikuwa na uhamasishaji mkubwa uliofanywa na viongozi wa serikali,kamati ya ulinzi na usalama na madiwani.

Amesema kuwa msako huo umefanyika usiku na mchana kwa nia ya kuwapata watoto wote 5,869 waliomaliza darasa la saba mwaka jana na kuchaguliwa kuendelea na kidato cha kwanza,lakini hadi mwishoni mwa wiki iliyopita wamebaki nyumbani.

Amesema,katika msako huo wazazi wengine 600 wamejisalimisha kwa kupeleka watoto wao shule baada ya kushuhudia wenzao wakikamatwa na kufikishwa Polisi.

Mtatiro amesema,operesheni hiyo imekuwa yenye mafanikio makubwa kwani katika muda wa siku tatu wamewapeleka zaidi ya watoto 1,335 shule kati ya 5,868 wanaotakiwa kuanza kidato cha kwanza na wanaendelea kuwatafuta watoto waliobaki.

Mtatiro ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilayani Tunduru amesema,watahakikisha hadi Jumatatu ya wiki ijayo watoto wote wanaotakiwa kuanza kidato cha kwanza katika muhula wa masomo ulioanza tangu Januari 9,wanaripoti kwenye shule walizopangiwa.

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro,akimsikiliza mtoto (pichani) ambaye amechanguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka huu lakini ameshindwa kuripoti shuleni.

Amesema,Serikali ya Awamu ya Sita imetoa fedha nyingi za kujenga shule mpya, kuongeza madarasa mapya kwa baadhi ya shule za zamani,kununua meza na viti na kusimamia sera ya elimu bila malipo kuanzia darasa la awali hadi kidato cha sita.

Amesema,licha ya Serikali kukamilisha ujenzi wa shule mpya na vyumba vya madarasa kwa asilimia 100,lakini inasikitisha kuona mpaka baadhi ya wanafunzi bado wako nyumbani huku wazazi wao wakitoa visingizio visivyokuwa na msingi.

Amewakumbusha wazazi na walezi wilayani humo kutambua kuwa,muda wa kupeleka watoto shule kwa hiari umepita na sasa wanatakiwa kuwapeleka kwa lazima na atakayeshindwa atachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwamo kufikishwa mahakamani.