Majangili wamedungua helikopta, mali ya asasi ya Friedkin Conservation Fund yenye uhusiano wa moja kwa moja na kampuni ya uwindaji wa kitalii ya TGT na kumuua rubani raia wa Uingereza.
Tukio hilo limeripotiwa katika eneo la Pori la Akiba la Maswa. Hii ni habari ya kusikitisha, hasa ikizingatiwa kuwa pamoja na mauaji ya rubani, tembo watatu waliuawa na kunyofolewa pembe.
Ujangili huu ni salamu kwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli. Ni ujumbe mzito na wa wazi kwa viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Waziri Profesa Jumanne Maghembe; Naibu Waziri Injinia Ramo Makani; na Katibu Mkuu, Meja Jenerali Gaudence Milanzi.
Wimbi la ujangili nchini lilipungua baada ya kutekelezwa kwa Operesheni Tokomeza, ambayo hata hivyo haikudumu baada ya kuwapo madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu. Pamoja na dosari za hapa na pale, kuna wananchi wengi wanaoamini upo umuhimu wa kurejesha awamu ya pili ya operesheni hiyo.
Tunasema hizi ni salamu kwa Rais Magufuli na viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa sababu hawa majahili wamejiandaa kufanya lolote wanalotaka alimradi wauwe tembo, faru na wanyamapori wengine.
Kwa muongo mmoja Tanzania imepoteza nusu ya tembo wote iliyokuwa nayo. Hii ni kuonyesha kwamba majangili walikuwapo, wapo na kama Serikali, vyombo vyake na wananchi hatutashirikiana kukabiliana nao, basi wanyama hawa watatoweka.
Rais Magufuli ni mtu wa vitendo. Wakati akimtangaza Meja Jenerali Milanzi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, alitamka wazi kuwa mwanajeshi huyo anapelekwa hapo ili pamoja na kazi nyingine, akapambane na majangili. Tunaamini uteuzi huu ni sahihi kwa vigezo na kwa wakati.
Alimradi majangili wamepiga hatua moja zaidi ya kuanza kushambulia na kudungua helikopta, ni wajibu wa Serikali na wananchi sasa kuingia katika vita dhidi ya wahalifu hawa. Lakini vita hii haitakuwa na tija kama sheria zetu hazitabadilishwa kwa kuuweka ujangili kwenye kundi la uhalifu ambao mtiwa hatiani atastahili adhabu kali zaidi, ikiwamo ya kifungo cha maisha.
Kuendelea kuwachekea majangili kwa kigezo cha haki za binadamu, maana yake ni kuwapa fursa na kibali cha kuendelea kuteketeza urithi huu ambao kama mababu zetu wangekuwa na tamaa za kipuuzi kama hizi za majangili, leo tusingewaona tembo, faru wala wanyamapori wengine.
Serikali pekee haiwezi kushinda vita hii. Ni wajibu wa kila Mtanzania mzalendo kushiriki mapambano haya kwa kuwaripoti wahusika kwenye vyombo vya dola.
Wakati huu wa amani nchini mwetu, hatuna budi kulitumia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kulinda rasilimali zetu. Si busara kuona JWTZ ikiacha kutumiwa wakati ambao wanyama na walinzi wa wanyama wakimalizwa. Operesheni Tokomeza II inahitaji haraka. Utalii kwa sehemu kubwa ni wanyamapori. Asilimia karibu 20 ya fedha za kigeni katika pato la Taifa zinatokana na utalii. Tulinde wanyamapori wetu kwa gharama yoyote. Uwezo wa kushinda vita hii uko dhahri.