SHEHE  Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa amemuonya mwanaharakati maarufu, Mange Kimambi kwa madai kuwa amemporomoshea matusi mazito baada ya kumuona mtandaoni amepiga picha na mgombea Ubunge wa Jimbo la Kinondoni kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Maulid Mtulya.

Shehe Alhadi ameyasema hayo leo wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa picha hiyo alipiga na mgombea huyo baada ya kukutana msibani ndipo baadhi ya wanachama wa CCM waliomba kupiga nae picha jambo ambalo asingeweza kulikataa alisema Alhadi.

Aidha, Shehe huyo alisema hata kama alifanya makosa kupiga picha na mgombea huyo lakini hakustahili kutukanwa vile.

“Kama amezoea kuwatukana viongozi wa serikali asituchezee viongozi wa kidini, ulimi na mikono aliyopewa na Mwenyezi Mungu hakupewa kwa ajili ya kuwakashifu watu hivyo hapa alipochokoza sasa ameingia sipo, nasema mwaka huu hataumaliza salama.,” alisema Shehe Mussa.

Baada ya kusema hayo, Shehe Alhadi alimkaribisha, Mufti Abubakar Zuberi aliyemtembelea ofisini kwake akiwa kwenye ziara za kutembelea ofisi za Bakwata nchi nzima na kuwahimiza waislamu wote kuitambua na kuiunga mkono taasisi hiyo na kuepuka migogoro.