Ongezeko la idadi ya watu limetajwa kama moja ya mambo yanayosababisha kuongezeka kwa migogoro inayotokana na muingiliano wa wanyamapori na binadamu.
Hayo yamebainishwa katika semina ya mafunzo ya waandishi wa habari iliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) wiki iliyopita. Mafunzo hayo yamelenga kuwapa wanahabari hao elimu zaidi kuhusu uhifadhi wa mazingira, wanyamapori na utalii hapa nchini.
Mafunzo hayo yamefanyika chini ya Mradi wa PROTECT (Promote Tanzania Environment, Conservation and Tourism) unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID).
Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa idadi ya watu nchini huongezeka kwa asilimia nne kila mwaka, hivyo inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2035 Tanzania itakuwa na zaidi ya watu milioni 90.
Ongezeko hilo la watu litasababisha kupanuka kwa matumizi ya ardhi kama vile kufyeka misitu kwa ajili ya kujenga viwanda, makazi ya watu, barabara, kilimo na shughuli nyingine za kibinadamu.
Aidha, ongezeko la watu linaelezwa kusababisha athari kwa makazi ya wanyamapori kama vile kuziba kwa njia za wanyamapori (ushoroba), hivyo kusababisha wanyamapori kupoteza mwelekeo pindi wanapohama kutoka eneo moja kwenda eneo jingine kutafuta malisho na maji.
Ripoti ya Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) iliyotoka hivi karibuni inaonyesha kuwapo ongezeko la matukio ya tembo, nyati, viboko na wanyamapori wengine kama simba, chui na mbweha wanaovamia makazi ya watu.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa mwaka 2016/17 jumla ya matukio 833 yameripotiwa, huku mwaka 2018/19 idadi ya matukio yaliyoripotiwa yakifikia 1,510.
Matukio hayo yanakwenda sambamba na kuongezeka kwa vitendo vya wanavijiji kuwashambulia na kuwaua wanyamapori, ambapo kwa mwaka 2014 hadi 2018 jumla ya simba 36 wameuawa.
Askari Mhifadhi wa Wanyamapori Tarafa ya Mikumi, wilayani Mvomero, Makene Ngoroma, anasema kwa sasa matukio ya migogoro baina ya wanyamapori na binadamu yameongezeka katika eneo hilo.
Anavitaja vijiji vya Luba, Mkata, Melela, Doma, Lubingo na Sokoine Kibaina vilivyoko karibu na ushoroba wa wanyamapori kutoka Hifadhi ya Taifa ya Mikumi kwenda Hifadhi ya Wami Mbiki kuwa kwenye mgogoro mkubwa baina ya wanyamapori na binadamu.
Anasema kwa miaka ya nyuma wanyamapori walikuwa wakipita katika vijiji hivyo wakitoka Hifadhi ya Mikumi kwenda Wami Mbiki lakini kwa sasa hivi wanyamapori wakipita maeneo hayo hubaki hapo hapo kutokana na maeneo hayo kuboreshwa kwa shughuli za kilimo.
Ngoroma anasema hali hiyo imechangia kuharibiwa mara kwa mara kwa mashamba yaliyomo katika ushoroba huo, huku wanavijiji wakiilaumu serikali kutotoa fidia kwa uharibifu wa mazao yao unaofanywa na wanyamapori hao.
“Watu wengi sasa hivi wanailalamikia serikali kwamba inathamini sana tembo kuliko binadamu. Diwani wa Kata ya Melela kila siku unakuta ana malalamiko mengi ya wananchi mashamba yao kuvamiwa na wanyamapori, malalamiko ni mengi kwa kweli,” anasema Ngoroma.
Aidha, anasema kitendo cha kuirudisha Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) katika halmashauri kinaleta mkanganyiko wa kisheria katika utendaji kazi wake.
Anasema askari wanaolinda wanyamapori wako chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii lakini kwa sasa wanafanya kazi chini ya Tamisemi, hali inayosababisha kukosekana kwa utaratibu mzuri wa utendaji.
Anasema kwa sasa askari wamezidiwa na wanyamapori, hali inayoelezwa kuendelea kusababisha migogoro baina ya wanyama na binadmu.
“Hawa askari wako chini ya TAWA, ila bajeti ya kuendesha shughuli zao inatakiwa ipitishwe na kikao cha madiwani katika halmashauri, kama unavyojua halmashauri zetu zinasimamia mambo mengi, unakuta kipaumbele kwa askari wa uhifadhi hakipo.
“Sasa hivi migogoro ya wanyamapori na binadamu imeongezeka lakini sababu kubwa ni askari wa TAWA kukosa vitendea kazi ili kuimarisha doria,” anasema Ngoroma.
Mkurugenzi Mtendaji wa mradi wa USAID PROTECT, John Noronha, anasema ili kupunguza migogoro baina ya binadamu na wanyamapori vijiji vilivyopo karibu na hifadhi vinatakiwa kupatiwa elimu kuhusu wanyamapori.
Anaongeza kuwa jamii inatakiwa kuelimishwa kuhusu matumizi bora ya ardhi kwa kuainisha maeneo kwa ajili ya ufugaji, makazi, kilimo na hifadhi za misitu na mbuga.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo, anabainisha kuwa mradi wa PROTECT kwa mwaka huu utakuwa shirikishi.
Anaeleza kuwa mradi utaendeshwa kwa njia za semina na midahalo, ambapo wananchi watashiriki kujadili mambo mbalimbali kuhusu uhifadhi wa mazingira na utalii.