Wakati Ligi Kuu imeanza rasmi, yapo mambo mengi ambayo yanatakiwa kutazamwa kwa undani na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Nalo ni suala linaloendelea kujirudia kila msimu, ambalo ni tatizo la wachezaji wengi kujikuta wakishindwa kutimiziwa yale yote ambayo wanaahidiwa kupitia mikataba wanayoingia na klabu.

Uelewa wa wachezaji kuhusu haki zao za msingi wanazostahili kutimiziwa ndani ya kipindi wanachokuwa wakichezea timu walizoingia nazo mkataba, ni mdogo na unatakiwa ukuzwe ili wasiuone mchezo wa mpira wa miguu kama vile ni shughuli ya kitumwa, isiyo na masilahi.

TFF kama wasimamizi wa mchezo wa soka, wanatakiwa kuwa wabunifu kwenye suala la utetezi wa haki za wachezaji.

Katika kipindi ambacho msimu wa Ligi Kuu unakuwa umemalizika, huku wachezaji, makocha na viongozi wa timu wakiusubiri msimu unaofuata, si vibaya kama TFF wataandaa semina maalumu kwa ajili ya wachezaji ili wawape mwanga juu ya umuhimu wa mchezaji kuwa na mkataba ambao unalinda masilahi yake.

Badala ya kwenda kucheza mechi za ‘ndondo’ kwenye ligi za mitaani, watumie muda huo kupewa elimu juu ya masuala ya mikataba wanayoingia na timu. Semina hiyo inaweza kuandaliwa kwa ushirikiano kati ya TFF na wanasheria ambao ni wadau wa karibu wa soka.

Mada muhimu inayoweza kuwasilishwa ni ile yenye kuhusiana na umuhimu wa mchezaji kutafuta huduma ya mwanasheria, ambaye atamsaidia katika kuzijua tafsiri za vifungu vya mkataba pamoja na jinsi ambavyo vinafanya kazi.

Wachezaji ni wadau muhimu sana kwenye Ligi Kuu pamoja na zile za ngazi ya chini, bila ya wao kuwa tayari kucheza hakuna atakayekwenda uwanjani kutazama mechi.

Mchezaji anayecheza kwa unyonge kutokana na mambo aliyoahidiwa kwenye mkataba kutotimizwa, hawezi kujituma kwa uwezo wake wote. Tumeshuhudia wachezaji kadhaa wakiwemo Hassan Kessy na Mbwana Samatta wakati huo kususa kuichezea Simba kwa sababu ya vipengele vya mikataba kutotimizwa, ni sehemu ndogo tu ya wachezaji wengi ambao wanacheza soka katika ngazi ya juu, lakini kwa shingo upande.

Siku zote mikataba baina ya klabu na mchezaji ni suala la pande zote mbili kupata faida (win win situation),  haki za mwanasoka zinalindwa na haki za klabu zinalindwa. Kila upande unawajibika kufanya kila liwezekanalo ili kile kilichoahidiwa kwenye maandishi kiweze kutimizwa.

Uelewa wa mikataba kwa maana ya mtu kuzielewa tafsiri za vifungu, ni chanzo cha viongozi wa timu kufanya kazi kwa amani na mchezaji. Uongozi unapoahidi kumtafutia nyumba mchezaji, maana yake ni kuwa suala hilo limo ndani ya uwezo wa klabu.

Mchezaji anapopatiwa nyumba na gari kama ilivyoainishwa kwenye mkataba, maana yake hastahili kuwa na sababu ya kuchelewa kufika mazoezini.

Wachezaji wengi bado hawana uwezo wa kujiwakilisha wao kama wao, halafu wakati huo huo klabu ikiwakilishwa na mwanasheria. Lazima mchezaji atajikuta ananyanyasika wakati Ligi Kuu ikiwa inaendelea.

TFF ijipange katika kuandaa semina maalumu itakayoratibiwa na wanasheria, yenye lengo la kuukuza uelewa wa wanasoka ili wafanye kazi ya kucheza soka wakiwa na amani bila ya uwepo wa dukuduku wala malalamiko.

Lionel Messi anacheza soka kwa uwezo wake wote kwa sababu Barcelona ililiweka suala la matibabu yake kwenye maandishi ya mkataba.

Wanapotoa ahadi kwa wachezaji, wanajikuta wakikabiliana na utekelezaji wa kile walichokiahidi. Mara nyingi mtihani unaowashinda viongozi wa soka ni kule kushindwa kukipata kile walichokitegemea kupitia vyanzo vichache vya mapato.

Matokeo ya kukwama kiuchumi yanaleta athari za moja kwa moja kwa wale wachezaji ambao matakwa ya mikataba waliyoingia na klabu, yanakuwa bado hayajatekelezwa.

Kiongozi anayeyafahamu vizuri madhara ya kutoheshimu utekelezaji wa kile kilichoainishwa kwenye mkataba, lazima atakuwa makini katika ahadi anazomuahidi mwanasoka.

 TFF iwachukulie wachezaji kama ni wadau muhimu katika mchezo wa soka, lazima tufike mahali ambapo wachezaji wawe na haki ya kusikilizwa na si kuendelea kuwaamini viongozi kila mara wanapowashushia mzigo wa tuhuma wanasoka wetu.

 Haki huambatana na wajibu na mchezaji anazo haki zake zinazoambatana na utimizaji wa majukumu yake uwanjani na kwenye mazingira ya kambi ya timu kwa kipindi chote anachokuwa kazini.

Hivyo hivyo kwa upande wa uongozi, wanazo haki zao zinazoambatana na utekelezaji mzima wa wajibu wao. TFF itambue kuwa kuboresha kiwango cha Ligi Kuu, kinaweza kufanyika katika njia tofauti tofauti na hii ya kuukuza uelewa wa wachezaji wetu kwenye masuala ya mikataba wanayoingia na klabu, ni mojawapo ya njia hizo.