Mwenyezi Mungu alipoumba dunia yetu alipanga kila kitu kujiendesha kwa namna ya ajabu. Viumbehai na visivyokuwa hai vyote vilipangiliwa kimaajabu kabisa kwa kadiri ya huo utaratibu wa Muumba wetu. 

Pa Bwana Mungu hapawezi kamwe kutokea ombwe. Ndiyo maana Waingereza wanasema kisayansi kabisa kuwa “nature abhors vacuum” ndiyo kumaanisha ombwe kambwe halikubaliki duniani.  Ndiyo utaratibu uliowekwa na Mungu mwenyewe. Mwanadamu amepewa akili ya kutawala viumbe vyote. “…Na kuitiisha, mkatawale samaki wa baharini na ndege wa angani na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi”. (Mwa. 1:26b).

Hii amri ina maana mwanadamu kwanza ajitawale mwenyewe na ndipo aweze kutawala hivyo viumbe vingine. Na ili mwanadamu ajitawale mwenyewe amejiundia utaratibu fulani wa huko kujitawala. Utaratibu wenyewe ndiyo mfumo au umbile linalokubalika (format).

Mfumo unaanzia katika kaya, ukoo, kabila mpaka jumuia kubwa tunayoita taifa. Huko kwenye taifa utaratibu huo wa kujitawala unafuata sheria maalumu ambayo ndiyo Katiba au Sheria Mama.

Kila taifa lina aina yake ya Katiba na linajiendesha kwa msingi wa mfumo uliokubalika kitaifa. Ipo mifumo tofauti katika mataifa. Wengi wanatumia mfumo unaoandikwa. Wanakuwa na Katiba iliyoandikwa (written constitution).

Wengine, kama Waingereza au katika makabila yetu unatumika mfumo wa mapokeo tu kutoka kizazi hadi kizazi (unwritten constitution).

Tanzania tulichaguliwa na wakoloni huo mfumo wa utaratibu ulioandikwa (written constitution). Katiba yetu ya kwanza iliandikwa na wakoloni kule Lancaster House, London, Uingereza kabla ya Uhuru.

Katiba ile ndiyo iliyotumika mpaka tumepata Uhuru Desemba 9, 1961. Kuanzia hapo ndiyo ninapenda kuwaelezea wasomaji namna tulivyoanza kupata Katiba mbalimbali humu Tanganyika. Mwalimu Nyerere amekuwa daima anazungumzia katiba za nchi hii.

Basi tukianzia kule tulikodai Uhuru wa Taifa letu, tunaweza kuona tumefikaje hapa pa kupata Katiba bora ya wananchi tunayoitamani kuongoza maisha yetu kwa miaka 50 ijayo, kizazi hiki kipya chenye mawazo mapya na chenye ari ya kupata Katiba ya kisasa.

Fuatana nami kuanzia 1961, wengi wakiwa bado hawajazaliwa, mpaka leo hii tumekuwa na Katiba ngapi na za namna gani katika nchi yetu hii?

 

Mwalimu Nyerere alituambia haya, nanukuu:- “…For Tanganyika began independence in December 1961 with a constitution drawn up at a time when TANU was concerned almost exclusively with one thing – independence. For that reason we concentrated our attention on the powers of the Governor – General; the control of the Government over the civil service, the police and the army; and on the relationship between the judiciary, the people and the Government. In addition, British agreement to our constitution was necessary. For all these reasons the Independence Constitution of Tanganyika was neither particularly suited to the needs of our development nor was it entirely ours”. (Nyerere: UHURU NA MAENDELEO sura 25 uk. 173).

Hapo Katiba ile ya wakoloni ilipatikana kwa madai ya wananchi kupitia Chama chao cha TANU. Hii ni Katiba iliyojikita kujibu madai ya wananchi kutaka kujitawala.

Waingereza walilainika na kutuambia lazima tusimamiwe nao, ndiyo maana Katiba inamtaja mwakilishi wa Malkia wa Uingereza kama Gavana – Jenerali. Lakini Katiba ilitaja mambo ya muundo wa Serikali, utumishi wa umma (civil service). Majeshi ya Polisi na Ulinzi, huendeshwaji wa Mahakama (Judiciary) ndiyo kusema matakwa ya TANU yalikuwa (were contained) yamekubalika kikatiba.

Basi Katiba yetu ya kwanza katika nchi yetu ilikuwa ya kiutawala tu. Haikuhusisha malengo ya maendeleo ya wananchi kiustawi wa jamii. Tulisema eti tutafute kwanza Uhuru wa kujitawala/au kujiamulia mambo yetu wenyewe, hayo mambo mengine yatafuata baadaye.

Katika Biblia tunakuta maneno haya…. “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, haki yake, na hayo yote mtazidishiwa” (Mat. 6:33).

Katiba ile ya kwanza ilitekeleza lengo letu lile la kuipatia Uhuru Tanganyika. Ndipo mambo mengine yangefikiriwa baada ya kupata Uhuru wetu. Kwa kuwa tumekuwa nchi huru sasa tuliweza kuandaa Katiba yetu tuliyoitaka kutuwezesha kuendelea. Tukajiandalia Katiba yetu tukajiondoa kabisa kwenye makucha ya mkoloni tukajiandikia KATIBA YA JAMHURI YA TANGANYIKA na ikaanza kutumika kuanzia Desemba 1962.

Kuanzia Januari 1963 tulitumia Katiba yetu mpya ya Jamhuri. Katiba ile iliandikwa na sisi Watanganyika na ikapata baraka za Bunge la Tanganyika na tukawa na Rais wetu katika hiyo Jamhuri yetu ya Tanganyika. Kwa vile Katiba yenyewe iliandikwa kwa harakaharaka mradi tuondokane na wale wakoloni tusiwe na Gavana Jenerali basi ilikuwa na upungufu hapa na pale. Hii ilikuwa Katiba yetu ya pili.

Ndipo Rais wa Jamhuri ya Tanganyika akateua Tume maalum, izunguke nchi nzima kupata mawazo na maoni ya wananchi wa Tanganyika huru ili kupata Katiba ya kidemokrasia kwa Watanganyika. Tume ile ilipewa hadidu za rejea kama hizi:-

  1. Tanganyika ibaki kama Jamhuri inayoongozwa na Rais (Executive Head of State).
  2. Iwe na utawala wa sheria na mamlaka huru ya Mahakama (The Rule of Law and the Independence of the Judiciary shall be preserved).
  3. Yenye usawa kwa raia wote (there shall be complete equally for all Tanganyika citizens).
  4. Yenye Uhuru kabisa wa siasa kwa raia wote kwa msingi wa Serikali ya taifa) (there shall be the maximum political freedom for all citizens within the context of a single national government).
  5. Yenye ushiriki wa kutosha wa wananchi katika Serikali yao na wenye madaraka kamili kuongoza Serikali (there shall be the maximum possible participation by the people in their own government and ultimate control by them over all the organs of state on the basis of universal suffrage).
  6. Yenye uhuru wa watu kuchagua wawakilishi wao katika mabaraza yote ya uwakilishi na kutunga sheria kadiri ya sheria za nchi. (There shall be complete freedom for the people to choose their own representatives on all Representative and Legislative bodies, within the context of the law).

Aidha, Tume ile ya Rais ilipewa pia kazi ya kutia katika Katiba maadili ya kitaifa na kuangalia namna ya kutunga Katiba yenye muono wa chama kimoja (one party state). Katika hilo Tume ilipaswa kuandika ile miiko ya uongozi katika Azimio la Arusha na kuangalia nafasi ya Chama Tawala kama mtunga sera wa Taifa hili. Pia Tume ilitakiwa kuoanisha au kutenganisha (kadiri itakavyoona) uamuzi wa Bunge na ule wa Kamati Kuu ya Chama. Kuweka pia mipaka ya madaraka kati ya viongozi wa Serikali na viongozi wa chama tangu wilayani, mikoani hadi Serikali Kuu.

Katiba pia ilitakiwa itamke sifa za wagombea katika nafasi mbalimbali za uwakilishi na namna chaguzi zitakavyoendeshwa wilayani hadi kitaifa “… (Nyerere: Uhuru na Umoja sura 55 uk. 261).

Tume teule ilifanya kazi yake tangu Januari, 1964 na kukabidhi ripoti yao 1965. Kumbe, wakati Katiba hii inaandikwa na tume, nchi zetu mbili zilikwisha kuungana hapo Aprili 26, 1964. Kwa hali hiyo, ripoti ya Tume ilipelekwa hata kwa Chama cha ASP kule Zanzibar maana unaposema Katiba ya Serikali ya Chama kimoja basi kwa kule visiwani ndiyo ASP na haikuwa TANU.

Kwa maana Katiba itakayotungwa itahusu nchi zote mbili – Tanganyika na Zanzibar ndiyo kusema itatumika katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika kikao cha Bunge cha Juni 8, 1965, Rais aliomba Bunge lile lipokee na kujadili rasimu iliyopendekezwa ya Katiba ya Serikali ya Chama kimoja.

Alisema haya, namnukuu “…We have thus come to a position where the maintenance of institutions and procedures which were supposed to safeguard the practice of democracy, and which are appropriate to a multi-party system, in fact eliminates the people’s choice of the representative.

It was to remedy this situation that the TANU Annual Conference decided, in 1963, to establish a democratic one-party system by law. A Presidential Commission was set up to consider what constitutional and other changes were necessary to implement this objective. Its report is now before you, together with a Government White paper which incorporates the amendments decided upon by the Party and the Government”. (Nyerere: UHURU NA UMOJA uk. 36 – 37).

Hapa inaonekana dhahiri kwamba chama kilishaamua kuachana na mtindo wa demokrasia ya vyama vingi ya kuiga kutoka nchi nyingine. Kila nchi ina mazingira yake na ina watu wa aina yake. Basi kwa wakati ule wa miaka ya mwanzo mwanzo ya Uhuru, demokrasia ya vyama vingi jamani haikueleweka.

Ndipo Tanganyika ikaamua kufuata demokrasia ya chama kimoja na hivyo iliundwa Serikali ya Chama kimoja na uchaguzi uliendeshwa wa chama kimoja. Nasema kwa wakati ule hali iliruhusu. Baadaye Mwalimu alitambua umuhimu wa kuwa na Katiba nzuri ya wananchi.

Mwalimu alitoa wazo la kwa nini anapendelea Katiba namna ile. Alisema hivi, namnukuu tena, “But the Institutions of a democratic government must reflect the national culture and national ambitions of the country in which they are working. Thereafter in 1962, we ourselves worked out a republication constitution under which we have since governed ourselves…” (Nyerere Uhuru na Ujamaa uk. 37).

Hii Katiba iliyotumika kwa sasa, naiita ni Katiba ya Tatu (3) kwa nchi yetu hii ya Tanganyika. Mwalimu alimalizia kwa kusema hivi, “We refused to put ourselves in a strait-jacket of Constitutional devices even of our own making. The constitution of Tanzania must serve the people of Tanzania” (Nyerere Uhuru na Ujamaa uk. 37).

Katiba ya nchi hata ikitungwa na wananchi wenyewe kama haikidhi matakwa ya wananchi au kwa kupitwa na wakati au vinginevyo, haifai kutumika. Tena tusiige Katiba mifano kutoka mahali pengine maana mazingira hayalingani. Katiba ya Tanzania iwe ya watu wa Watanzania kwa hali na mazingira ya wananchi wa Tanzania.

Bunge lile la mwaka 1965, lilipitisha Katiba ya Jamhuri ya Tanganyika na ndiyo iliitwa Katiba ya Muda (interim Constitution). Ilitumika kwa chaguzi za kuanzia mwaka 1965-1975. Ilionekana wazi nayo ilikuwa na upungufu mwingi tu hasa kwa vile ilitungwa wakati nchi zetu mbili hizi zimeungana, lakini Vyama vya Siasa vya TANU na ASP havikuwa vimeungana.

Pamoja na hayo Katiba ile iliweza kumudu kuliongoza Taifa letu kwa amani licha ya upungufu wa hapa na pale hasa katika masuala ya Muungano. Imetumika kwa muda wa zaidi ya miaka 10 ikiwa inaitwa Katiba ya Muda (Interim Constitution).

Mtakumbuka basi uchaguzi wa mwaka ule 1965 ulifanyika huku Bara tu kule Zanzibar haukufanyika. Hali hii inaeleweka kutokana na utete wa Serikali ya Mapinduzi miaka ile ya mwanzo mwanzo. Mwaka 1977 sote tunajua vyama vya siasa vya TANU na ASP viliungana tarehe 5 Februari na kikazaliwa chama kimoja kwa nchi zote mbili Tanganyika na Zanzibar. Hiki ndicho Chama Cha Mapinduzi (CCM) tunachokijua sote.

Chama hiki kimeleta pia Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katiba ile kwa Tanganyika ni ya 4 na inajulikana kama Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Hakika Katiba hii imetuongoza vizuri chini ya Serikali ya chama kimoja.

Katiba ilisema hivi:- Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa yenye chama kimoja cha siasa. Chama ndicho chenye madaraka ya mwisho katika mambo yote kwa mujibu wa Katiba hii na Katiba ya Chama. Chama cha Mapinduzi, kwa kifupi “CCM” ndicho Chama cha Siasa pekee katika Jamhuri ya Muungano.

Tazama SURA YA KWANZA, SEHEMU YA KWANZA kifungu 3 (1), (2) na (3) uk. 9 wa Katiba. Tangazo la nchi yenye chama kimoja: Sheria ya 1984 No. 15 ibara ya 6. Tulipofika mwaka wa 1992 upepo wa mabadiliko ukaanza kuvuma hapa Tanzania. Kizazi kipya kikaona kuna haja nchi hii sasa kuwa kama nchi nyingine za ulimwengu wa sasa. Mazingira yanaruhusu kuwa na vyama kadhaa vya siasa katika Jamhuri yetu ya Muungano. Ndipo 1992 sheria za Katiba ya Jamhuri zikabadilishwa ili kusomeka ni Jamhuri ya Muungano yenye kuwa na vyama kadhaa vya siasa. Hili lazima tulikubali lilikuwa ni jambo kubwa na ni mageuzi ya kisasa kabisa.

Unapokuwa na vyama kadhaa vya siasa lakini, Katiba bado inaonesha ya Serikali ya Chama kimoja kwa maneno kama haya – UTANGULIZI SURA YA KWANZA: JAMHURI YA MUUNGANO, CHAMA, WATU NA SIASA YA UJAMAA NA KUJITEGEMEA, hapo neno CHAMA lilimainisha Chama kimoja tu. Kumbe upungufu huo ulirekebishwa mara baada ya mwaka 1992 na hapo viraka (amendments) viliendelea kubandikwa katika Katiba kuirekebisha kulingana na hali na wakati uliopo.

Kwa hiyo, Katiba ile ya 1977 toleo lile la 1995 mabadiliko yanaonekana kwa mujibu wa sheria No. 4 ya 1992, lilitolewa tangazo rasmi kuwa Tanzania itakuwa nchi yenye mfumo wa VYAMA VINGI – ndiyo sababu katika sura ya I YANASOMEKA MANENO: JAMHURI YA MUUNGANO, NI NCHI YA KIDEMOKRASIA NA YA KIJAMAA, YENYE KUFUATA MFUMO WA VYAMA VINGI VYA SIASA (Sheria No. 4 ya 1992 ibara ya 5 vifungu (1) na (2).

Kuanzia hapo lilipotolewa tangazo la kuwa nchi yenye vyama vingi vya siasa Sheria No. 4 ya 1992 ibara 5 (1) na (2), mabadiliko yakaanza kuonekana. Ndipo chaguzi zile za miaka 1995-2010 zimekuwa na vyama vingi. Baada ya uchaguzi wa mwaka 2010 upungufu wa Katiba hii ulidhihirika zaidi ndipo Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Mrisho Kikwete, akaja na wazo la kuboresha ile Katiba iliyopo ya 1977 toleo la 2005 na kuonesha sasa umefika wakati mwafaka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipate Katiba sahihi itakayoliongoza Taifa hili kwa miaka 50 ijayo.

Katiba tuliyonayo ni ya nne na imetumika kwa zaidi ya miaka 37 sasa na imeshapitwa na wakati; hali ya nchi imebadilika, mazingira yale ilipoandikwa Katiba yenyewe 1977 sasa yamebadilika sana na kuna kizazi kipya chenye ari kubwa ya maendeleo.

Kumbe Mwalimu alikwishaliona hilo tangu mapema miaka ile ya 1960. Basi akatutahadharisha kwa kusema… “The Constitution of Tanzania, both in the past and in the future, is SACRED in ONE SENSE ONLY. That is the sense in which it provides a framework within which – and only within which BOTH the GOVERNMENT and the LAWS can be changed at the WILL of the PEOPLE. Akaonya kuwa… “to attempt to change either the laws or the GOVERNMENT outside that framework – the pattern of procedure – is TREASON to our country”. (Nyerere: UHURU NA UJAMAA uk. 38 ibara ya 2).

Kwa tafsiri yangu, maneno muhimu na mazito haya yalikuwa na maana hivi, Katiba ya Tanzania huko nyuma na hapo baadaye ni kitu KITUKUFU kwa maana moja tu.

Na maana hiyo ni kule kutoa mhimili ambamo Serikali na sheria vinaweza kubadilishwa kwa matakwa ya watu wenyewe. Kujaribu kubadilisha sheria au Serikali nje ya mhimili huo, mfano na utaratibu huo ni UHAINI kwa nchi yetu!

Loo! Mnaona uzito wa kuheshimu Katiba kwa mtazamo wa Baba wa Taifa tangu miaka hiyo ya 1965? Kwa hiyo, Katiba ni andiko tukufu na linapaswa kuandaliwa vizuri kabisa na kukubalika na wananchi wote. Katiba ni sheria mama ya nchi. Hakuna Taifa lisilokuwa na Katiba. Ndiyo sababu ulimwenguni wanasema nchi haitawaliki bila KATIBA.

Kama hivyo ndivyo, sisi Watanzania wote tunaililia hiyo Katiba mpya. Tupate Katiba bora itakayotuongoza miaka chungu nzima ijayo. Siyo bora KATIBA, la hasha tunataka KATIBA BORA na ndiyo itakuwa Katiba ya TANO (5) katika nchi yetu.

Hii Katiba bora inapatikanaje basi? Kwanza ni pale Rais anapoteua Tume ya kuandaa Katiba. Pili, Tume yenyewe inaongozwa na hadidu za rejea kama vile ikusanye mawazo ya wananchi, kutoka nchi nzima, iyaanishe, kisha iyaandike katika mfumo unaokubalika kisheria, tunaita Rasimu, hatimaye ipelekwe Bunge.

Tatu Bunge la nchi liipitie, liichambue na kisha liandike Katiba pendekezwa. Kwa kulinda demokrasia halisi basi hayo mapendekezo ya Bunge yapelekwe kwa wananchi waliotoa mawazo yao. Wananchi wanatakiwa waisome, waielewe na wakisharidhika kwa namna ilivyoandikwa ndipo watoe uamuzi wao kwa kuipigia kura ya ndiyo/hapana hilo andiko kutoka Bunge, au niite Katiba pendekezwa.

Jamani Katiba ya nchi siyo mali ya chama fulani cha siasa kama ilivyokuwa katika ile Katiba ya 1977 kifungu 3 – (2) kiliposema chama ndicho chenye madaraka ya mwisho wa mambo yote kwa mujibu wa Katiba ile. Kwa mujibu wa sheria ya Vyama Vingi Sheria No. 4, ya mwaka 1992 ibara ya 5-(1) na (2). Katiba inapaswa kuwa mali ya wananchi (owned by the people).

La msingi ni kwamba Katiba ya nchi haiandikwi nje ya Bunge. Utaratibu unaofuatwa na nchi zote ni huo wa Katiba kuandikwa na Bunge husika. Kwa mantiki hiyo basi haiwezi kutokea, wala haijawahi kutokea nchi ikaendeshwa bila Sheria Mama, yaani Katiba. Kutokana na utamaduni huo duniani ni wazi ombwe kamwe halikubaliki katika hali yoyote ile. Waingereza wanasema “Nature abhors vacuum” ndiyo kumaanisha ombwe duniani halikubaliki.

Tusijekuwa wa kwanza kama Taifa ulimwenguni kuendesha Serikali bila Katiba. Tujiandae kwa kupokea kile kilichotolewa na Bunge Maalum la Katiba, tukipokee, tukisome na hasa tuelewe ndipo tutoe uamuzi wetu wa kusuka au kunyoa. Kwa vyoyote vile tusikubali ombwe litokee katika Taifa letu. Katiba ni andiko TUKUFU tusilichezee.

Mungu ibariki Tanzania. Dumisha UHURU na UMOJA. AMEN