Na Moshy Kiyungi
Oliver Mtukudzi ni mwanamuziki mkongwe, anayevuma sana hata nje ya mipaka ya nchi yake
ya Zimbabwe.
Nyimbo zake zinazohamasisha amani na kutoa burudani barani Afrika, zimesababisha yeye
kutumika kama alama katika taifa hilo hususan kwa upande wa sanaa ya nchini mwake.
Wasifu wa Oliver ‘Tuku’ Mtukudzi unaeleza kuwa alizaliwa Septemba 22, 1952 mjini Highfield,
Harare. Ni mwanamuziki wa Kizimbabwe ambaye ni miongoni mwa wanamuziki walio maarufu
kwa muda mrefu katika nchi hiyo.
Oliver alianza kutambulika zaidi kimuziki baada ya kuingia katika Kundi la Wagon Wheels
mwaka 1977 akiwa na wenzake kadhaa, akiwamo Thomas Mapfumo.
Wimbo wake wa kwanza ulikuwa wa ‘Dzandimomotera’ ulioheshimika sana, na hapo ndipo
Tuku alipotoka na albamu yake ya kwanza iliyomletea mafanikio makubwa zaidi.
Aidha, Mtukudzi pia ni mmoja wa wanakundi la Mahube, kundi la muziki la nchi za Afrika Kusini.
Ni baba wa watoto watano na mpaka sasa ana wajukuu wawili. Watoto wawili kati ya hao, ni
wanamuziki. Oliver ana dada zake wanne. Kaka yake amekwishafariki.
Tuku hufurahia kuogelea katika bwawa lake (swimming pool) ambalo lina umbo la gitaa.
Ametoa zaidi ya albamu 40 na amepata kushinda tuzo nyingi mno hata nyingine hawezi
kuzikumbuka.
Mwanamuziki huyo wa kimataifa kutoka nchini Zimbabwe, amekwishatunukiwa tuzo ya tatu
iliyobeba heshima ya udaktari kutokana na kuwa mshauri na balozi mzuri wa muziki.
Mwaka 2003 alitunukiwa tuzo kubwa ya heshima na Chuo Kikuu cha Zimbabwe kwa kutambua
miongo kadhaa ya mchango wake na kujitolea katika kujenga muziki na msukumo kwa wasanii
wa kizazi kipya nchini Zimbabwe, huku akionesha ushawishi kwenye kazi za wasanii hao.
Mwaka 2009, Chuo Kikuu cha Wanawake cha Afrika kilimpatia tuzo ya shahada ya sanaa na
kumwelezea mwanamuziki huyo kama mbunifu wa hali ya juu kuwahi kutokea nchini Zimbabwe
katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita.
Wengi wanamfahamu Mtukudzi kutokana na umahiri wake mkubwa katika medani ya muziki,
utambulisho wake mkubwa ukiwa ni sauti yake nzito na ya kipekee.
Licha ya Oliver kuwa mwanamuziki, pia ni mfanyabiashara, mwanaharakati wa haki za
binadamu na balozi wa UNICEF Kusini mwa Bara la Afrika.
Mara nyingi Tuku huimba nyimbo katika lugha tatu tofauti za Kishona, Kindebele na Kiingereza.
Huchanganya ala za muziki wa kiasili kwenye nyimbo zake, jambo lililompa umaarufu mkubwa
dunia nzima.
Tofauti na wenzake katika Kundi la Wagon Wheels waliokuwa wakimwimba vibaya Rais wa
zamani wa nchi hiyo, Robert Mugabe, Mutukudzi alikuwa akimsifia sana na kusababisha
anufaike kwa misaada mbalimbali kutoka serikalini.
Mwaka 2010, mwanae kipenzi, Sam Mutukudzi, ambaye naye alikuwa mwanamuziki, alifariki
dunia kutokana na ajali mbaya ya gari.
Mutukudzi amekuwa akidaiwa mara kwa mara kwamba ni mwathirika wa ugonjwa wa Ukimwi,
ingawa mwenyewe amekuwa akikanusha vikali madai hayo.
Kati ya wasanii wenzake waliokuwa wakiunda kundi la Wagon Wheels, ni yeye pekee aliyebaki
hai hadi leo. Wenzake wote wamekufa kwa Ukimwi.
Hivi karibuni, mashabiki wake nchini humo walipatwa na mshangao mkubwa baada ya kitabu
kiitwacho ‘Tuku Backstage’ kuvuja kikiwa na kashfa nyingi za ngono zinazomhusu gwiji huyo,
mwandishi akiwa ni Shepherd Mutamba.
Baadhi ya albamu za mwanamuziki huyo ni ‘Ndipeiwo Zano’ ya mwaka 1978, ikarudiwa tena
mwaka 2000, ‘Chokwadi Chichabuda’ na ‘Muroi Ndiani?’ za mwaka 1979, ‘Shanje’ na ‘Pfimbi’
za mwaka 1981, ‘Nhava’ ya mwaka 2005, ‘Wonai’ ya 2006, ‘Tsimba Itsoka’ na nyingine nyingi.
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba: 0767 331200, 0713 331200 na 0784
331200