Leo nimeazima busara ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliyesema kwamba kupanga ni kuchagua.

Uongozi wa Mwalimu Nyerere haujapata kutokea, si Tanzania tu bali katika nchi nyingi za dunia, hata kama katika hili kuna wale wasioambilika. Kama mipango yote aliyokuwa ameisuka na kuanza kutekeleza Mwalimu ingepata wasimamiaji wazuri, nakuapia leo tungeweza hata kuandaa michezo ya Olimpiki. Hapo tulipo michezo ya Afrika inatutia tumbo joto, na sidhani kama tunaweza kuandaa zaidi ya ile ya Kagame, ambayo pia zawadi inatolewa na mtu binafsi kutoka nchi jirani anayeitwa Paul Kagame. Hilo sina ugomvi naye, wala kwa Tanzania kuandaa hainipi shida. Mtima wangu unasononeka na jinsi tunavyoshindwa kuvuka vigingi vikubwa.

Nadhani sababu moja kubwa ni kutothubutu, jambo ambalo mwanafunzi mmojawapo wa Mwalimu – Rais Benjamin Mkapa –  alilisemea sana japokuwa sina hakika kama alitoa fursa au kuwezesha watu wa ndani kuthubutu kuwa wajasiriamali.

Kwa nini nimesema kupanga ni kuchagua? Ni kwa sababu kama unataka maendeleo, lazima uwe tayari kuingia kwenye ‘risk’. Ndivyo Uingereza ilivyofanya. Pamoja na ukubwa wa uchumi wake, wapo waliokuwa wanaogopa na kupinga kuandaa kwake Michezo ya 30 ya Olimpiki iliyomalizika mjini hapa juzi Jumapili. Lakini viongozi wote waliungana na hata sasa wapo pamoja – iwe wa Labour, Conservative au Liberal – lao moja. Ilikuwa busara kuamua kuandaa.

Waziri Mkuu, David Cameron aliwatoa wananchi hofu kwamba hachezei pesa sao, maana ile sherehe ya ufunguzi tu iliyodumu kwa saa tatu unusu iligharimu pauni milioni 27 hivi. Je, ujenzi wa viwanja vipya! Tukija kwenye miundombinu mipya iliyolazimika kujengwa kama barabara na reli; hatujazungumzia majengo mapya na hata kukatisha maisha ya kawaida ya Londoners kwa kiasi fulani. Yote hayo ni ‘risk’, ambayo kama mchumi au mfanyabiashara unakuwa hujui kama atajenga woga kuwa itakula kwake.

Shemeji yangu Mrema wa NCCR-Mageuzi wakati huo alikuwa anasema mambo hayo ya kutokuwa na uhakika ni sawa na mchezo wa karata tatu. Sasa Uingereza walifanya kampeni kubwa hadi kupata nafasi hii, wakaandaa na kufanikisha, matokeo yake yatakuja siku si nyingi. Usishangae kuja kusikia mwaka kesho jinsi uchumi wa Uingereza utakavyokuwa unapanda na mafanikio zaidi kwenye sekta ya michezo, ambayo inaingiza pesa nyingi tayari kwa kodi.

Msisimko wa michezo hii kufanyika nyumbani umeifanya Uingereza kuwa na umoja zaidi, uzalendo zaidi na mafanikio zaidi kuliko miaka 104 iliyopita. Wametwaa medali kama hawana akili nzuri achilia mbali wafalme akina China na Marekani. Katika kuenzi michezo hii, tayari wamependekeza michezo shuleni ihuishwe na kupewa kasi kubwa zaidi.

Usishangae kuona watoto wanaofanya vizuri, hata wawe Wanyasa, wanahamishiwa kwenye academia zao na kufunzwa vizuri kuogelea, ili waendane kitandawazi na si kama hapo Ziwa Nyasa kwa Kandoro na Banda.

Leo niishie hapa. Tuwasiliane wengine ili wiki ijayo turejee kwenye masuala yetu, sijawasahau wadau na maombi na masuala yenu, tuvumiliane hadi wiki ijayo.

[email protected]