Moja ya mashindano yanayojumuisha watu wengi duniani yamekaribia, tena yanafanyika hapa hapa London.
Haya ni Mashindano ya Michezo ya Olimpiki yaliyopangwa kufanyika wakati wa majira ya joto katika jiji hili, lililo kitovu cha biashara, fedha na mahusiano duniani.
Wakati Waingereza, Wazungu na wadau wengine wakijiandaa kwa kila hali, Waafrika na kwa namna ya pekee Watanzania wanayo fursa kubwa ya kuangalia jinsi ya kufaidika.
Mashindano haya yanaanza ndani ya miezi miwili kutoka sasa, maana ni Julai 27 na yataendelea hadi Agosti 12. Yameathiri watu wengi mashindano haya kwa njia hasi lakini pia njia chanya, kwa sababu watu wamevuna na wanaendelea kuvuna.
Asikudanganye mtu, kazi ni kazi, na Wazungu wenyewe wanazichangamkia kazi hizo bila woga wala aibu, hata kama ni za kuchekesha. Moja ya fursa zilizopo wazi na wiki iliyopita nimekuta watu wakiziwinda ni kucheza ngoma za maeneo mbalimbali.
Sikujua mambo haya, lakini nimefika na kukuta makubwa yanafanyika pale. Watu baki kabisa wamepewa jukwaa la kuonyesha ubunifu wao mbele ya halaiki na hapo wanakamata manoti!
Kwa vile mashindano yanajumuisha watu kutoka kila pembe duniani, waandaaji wanataka mashindano hayo yatoe pia picha hiyo kwa kuonekana mambo ya huko.
Kwa hiyo kama ilivyozoeleka kuwaita ‘Wabongo’, basi wana nafasi ya kuchota mapaundi ya Malkia bila kuingia matatani. Kikubwa pale nilichoona ni ubunifu tu…mtu kujiandaa na kufanya utafiti kiasi kuhusu kipi kinafurahisha umma.
Licha ya kucheza ngoma za asili ya makabila ya Tanzania, ruksa pia kucheza ngoma na kuonyesha utamaduni na mila za makabila mengine ya Afrika, na ukiwa mahiri zaidi hata mabara mengine. Na huo ndiyo uzuri wa Wazungu.
Hawaangalii wewe ni nani bali una nini. Na kwa kulingana na jinsi ulivyo na kipaji na hazina kubwa ya mambo, basi watakukumbatia ili wahakikishe unawafaidisha kwa kuzipamba siku zao hizo za mashindano.
Wanataka hatimaye dunia iseme kweli Waingereza wameingia gharama… kweli wamefanya kazi kubwa… hakika wametimiza wajibu wao kwa kuvuta watu wa kila mahali kuwa nao London.
Kwa hiyo, baadhi ya watu wameshaingia kwenye mwelekeo huo. Si tu kwamba wameanza mazoezi ya kuonyesha umahiri wao, bali pia wapo Waswahili wanaotoa mafunzo ya michezo mbalimbali hata kwa ngoma na tamaduni za nje ya mipaka yao – wameula bwana!
Hakuna kitu Mzungu anachokienzi kama utaalamu wa kipekee kwenye jambo fulani. Inapokuwa kwamba wewe ni wa aina yake katika hilo, basi noti yako kwa kweli ni ndefu kabisa.
Mmoja wa jamaa wanaoendelea na mazoezi na kufundisha hapo, amewaambia wenzake anaofanya nao kazi kwamba atakuwa anakwenda siku moja moja kulingana na nafasi.
Na wao wanaelewa kuwa hiyo ni kazi kubwa na adhimu, kwa hiyo hata heshima yake imepanda, maana ni kana kwamba amekuwa mzalendo kwa kuhakikisha anafanikisha jambo la kitaifa na kimataifa kwa Waingereza mbele ya macho ya dunia yote.
Kwa hiyo anafundisha na pia mwenyewe anafanya mazoezi kwa ajili ya Olimpiki kwa mambo ya mila, utamaduni na ngoma ikijumuisha kucheza vidude aina mbalimbali vya muziki wa asili. Na anajulia kweli kweli.
Alikuwa ananiambia hapo alipo sasa hadi amalize atakuwa amechota ‘mahela’ mara zaidi ya mia ya huko anakofanya kazi. Huko wakati mwingine hakuna uhakika wa kazi kila siku, lakini pia zikiwepo malipo si makubwa. Mawazo ya wengi sasa yanaingia kwenye Olimpiki na ujenzi wa picha safi na kubwa ya Uingereza mbele ya mataifa.
Mawazo yanaanza kutoka kwenye majira ya baridi wakati huu mimea inapochipua na kutoa maua, huku mvua na pepo zikiendelea kwa nguvu, lakini baridi nayo ikiwa imerejea kiasi.