Uvumbuzi wa mabaki ya watu wa kale uliofanyika sehemu mbalimbali duniani unaweka rehani hadhi ya Bonde la Olduvai ambalo hadi hivi sasa ndilo eneo linalotambulika rasmi kama sehemu ambayo binadamu wa kwanza kabisa duniani aliishi.





Mtafiti akionyesha baadhi ya mabaki yaliyogunduliwa katika utafiti unaoendelea katika Bonde la Olduvai, eneo la Ngorongoro.

Licha ya kuweka rehani hadhi hiyo ya Olduvai, uvumbuzi huo pia umewaweka wachunguzi wa mambo ya kale katika sintofahamu kuhusu asili ya binadamu. Kila uvumbuzi mpya unatoa sura tofauti na kile kilichokuwa kinaaminika kuhusu historia ya binadamu na kuwafanya wataalamu hao kutokuwa na jibu la uhakika hadi hivi sasa kuhusu suala hilo.

Mathalani, uvumbuzi uliofanyika nchini Morocco mwaka 2017 ulileta shaka kubwa kwenye taarifa zilizopo kuhusiana na asili ya binadamu kuwa ni Afrika Mashariki katika Bonde la Olduvai. Mifupa ya watu wa kale iliyovumbuliwa Morocco mwaka huo ilionyesha kuwa ni ya kale zaidi kuliko ile iliyogunduliwa katika Bonde la Olduvai miaka kadhaa iliyopita.

Watafiti walikadiria kuwa mifupa hiyo iliyopatikana katika eneo la Jebel Irhoud nchini Morocco ina umri wa miaka 315,000, ikiwa ni miaka 100,000 zaidi ya rekodi iliyowekwa na mifupa iliyokuwa inadhaniwa kuwa ndiyo ya binadamu wa kale zaidi. Mifupa iliyokuwa inaaminika hadi wakati huo kuwa ni ya kale zaidi ilivumbuliwa nchini Ethiopia na vipimo vilionyesha kuwa binadamu huyo aliishi miaka 196,000 iliyopita.

Kupatikana kwa mabaki hayo katika eneo la mbali kidogo na maeneo ambako mifupa ya kale zaidi ilipatikana awali, ni jambo linaloibua maswali mapya. Kwanza, wataalamu wanajiuliza iwapo mabaki hayo yanahusiana. Na iwapo yanahusiana, kwa nini yamepatikana katika maeneo tofauti na yaliyo mbali sana? Na kama mabaki hayo hayahusiani, je, yapi yanawakilisha binadamu wa kale zaidi kwa uhalisia?

Mabaki mapya ambayo yanaonyesha kuwa ni ya kale zaidi yamepatikana katika eneo la Afrika Kaskazini, mbali kabisa na Afrika Mashariki ambako mabaki mengine yalipatikana awali.

Watafiti wanahisi kuwa uvumbuzi huu unaweza kuwa unaonyesha kuwa kumbe binadamu wa kale hawakuishi katika eneo moja tu, walikuwa wametapakaa katika maeneo mengi barani Afrika.

“Hakuna Bustani ya Edeni barani Afrika, au kama ipo, basi ni Afrika yote,” anaeleza mtaalamu wa anthropolojia, Jean-Jacques Hublin, ambaye aliongoza uvumbuzi uliofanyika Morocco.

Uvumbuzi mpya wa Morocco kuhusiana na asili ya binadamu unaonyesha kuwa pengine Homo sapiens walitokea kote barani Afrika kwa wakati mmoja, wakiishi katika makundi katika maeneo tofauti ya bara hilo.

Wakitumia matokeo ya uvumbuzi huo, mwaka 2018 timu ya watafiti walianza kuhisi kuwa makundi ya Homo sapiens ambayo yanahusiana, yaliibuka barani Afrika katika maeneo tofauti tofauti. Watafiti hao wanabainisha kuwa matokeo ya uvumbuzi wa Morocco na Ethiopia yanaonyesha kuwa Homo sapiens hawakutokea katika eneo moja kama inavyoaminika hivi sasa.

Hata hivyo, watafiti hawa wanasema kuna uwezekano kuwa makundi hayo, licha ya kuwa yalikuwa yanahusiana, lakini hayakufanana wakati yanaibuka. Watafiti hao wanahisi kuwa makundi hayo yalikuwa na baadhi ya sifa za kijenetiki zinazofanana, hivyo kuyafanya yote yabainishwe kama Homo sapiens kulingana na utafiti unaofanyika hivi sasa.

Kwa mujibu wa tafakuri hii, makundi haya yaliyokuwa na uhusiano wa mbali kijenetiki, ambayo yalikuwa yamesambaa kote barani Afrika, yalianza kuwa na sifa zinazofanana jinsi miaka ilivyokuwa inapita, kwa sababu walikuwa wanakabiliana na hali ya mazingira inayofanana. 

Hivyo, watafiti hawa wanaanza kuamini taratibu kuwa mabaki ya binadamu wa kale yaliyogunduliwa katika Bonde la Olduvai, si mwakilishi pekee wa binadamu wa kale kama ambavyo historia inasomeka hivi sasa kuwa alianzia Afrika Mashariki na kusambaa katika maeneo mengine barani Afrika.

Changamoto

Hii ni changamoto kubwa kwa Tanzania na Olduvai. Ni changamoto ambayo ina sura kama mbili hivi. Kwa upande mmoja ni changamoto kwa Olduvai, kwa sababu ipo katika hatari ya kupoteza hadhi yake kama eneo ambalo binadamu wa kwanza kabisa duniani aliishi.

Uvumbuzi mpya unaofanyika unatishia hilo kwa sababu mabaki hayo mapya yanaonekana kuwa ya kale zaidi ya yale yaliyopatikana Olduvai.

Kwa upande mwingine, uvumbuzi huo mpya unatoa changamoto kwa utafiti kuendelea, tena ikiwezekana kuendelea kwa kasi katika eneo la Olduvai. Kilichogunduliwa mpaka hivi sasa katika utafiti unaofanyika katika Bonde la Olduvai ni sehemu ndogo tu ya vitu ambavyo inaaminika vimefukiwa katika eneo hilo, vikielezea historia ya maisha ya binadamu wa kale. 

Tabaka ambalo tayari limekwisha kufukuliwa na kutoa vitu vilivyobainika kuwa vinahusiana na binadamu wa kale zaidi duniani ni dogo sana. 

Bado kuna matabaka mengine mengi chini yake ambayo iwapo yatatafitiwa kwa kina kuna uwezekano yakavumbuliwa mabaki ya vitu ambavyo ni vya kale zaidi ya vile ambavyo vimebainika katika uvumbuzi uliofanyika katika maeneo mengine Afrika.

Hapa, suala ni kuongeza kasi ya utafiti kama dhamira ni kulinda hadhi ya Bonde la Olduvai. Kwa kawaida, katika kuandika historia ya dunia, ikitokea ikathibitika kuwa mabaki ya vitu vilivyogunduliwa sehemu nyingine ni vya kale zaidi ya vile vya Olduvai, itachukua muda mrefu sana mpaka Olduvai kurejeshewa hadhi yake, hata kama mabaki ya vitu yatapatikana tena Olduvai na kuonyesha kuwa ni vya kale zaidi.

Hivyo, njia nzuri ya kuchukua hivi sasa ni kuongeza kasi ya utafiti ili ugunduzi ufanyike haraka,  hivyo kusaidia kuiweka historia sawasawa.

Ni muhimu hilo likafanyika kwa sababu hadhi na heshima ambayo Bonde la Olduvai limelipatia taifa ni kubwa kuliko ambavyo watu wengi wanafahamu. Olduvai inaiweka Tanzania katika ramani ya dunia. Heshima ambayo Tanzania inapata kimataifa inachangiwa kwa kiasi kikubwa na kile kilichogunduliwa Olduvai.

Utafiti mwingine zaidi

Ukiacha vitu vilivyovumbuliwa Morocco na Ethiopia, ambavyo rekodi zake zinaonyesha kuwa ni vya kale kuliko vile vya Bonde la Olduvai, Bado kuna mabaki kutoka maeneo mengine ambayo nayo yanaleta changamoto kwa Olduvai. Mathalani, huko Botswana, yamepatikana mabaki mengine ambayo matokeo ya utafiti wa anatomia yanaonyesha kuwa binadamu wa sasa alianza kuishi katika nchi hiyo.

Matokeo ya utafiti huo yaliyochapishwa Oktoba mwaka juzi yanaonyesha kuwa binadamu anayetambulika sasa alitokana na mwanamke aliyeishi miaka 200,000 iliyopita katika eneo ambalo kwa sasa ni nchi ya Botswana. Watafiti waliweza kubaini hilo kwa kutumia utafiti wa vinasaba (DNA) ambavyo vilirithishwa kutoka kwa familia ya mwanamke huyo.

Matokeo hayo yanaendana na dhana kuwa mababu wa binadamu wa sasa walihama kutoka Afrika na kusambaa maeneo mengine duniani na kuzaliana, na hawakutokana na makundi tofauti yaliyokuwa yanaishi katika maeneo tofauti duniani ambayo yalistawi kwa nyakati tofauti.

Maendeleo ya sayansi na teknolojia yanawawezesha watafiti kubaini mababu zetu waliishi vipi ikiwemo walikuwa nini, walikuwa na maumbo gani na walitokea mahali gani.

Kwa upande mwingine, maendeleo haya yanatoa fursa kwa Olduvai kufanya maajabu zaidi kwani sayansi na teknolojia inaweza kusaidia kuonyesha kuwa bado eneo hilo ndilo asili ya binadamu. Kinachotakiwa ni kutengwa kiasi cha kutosha cha fedha kwa ajili ya kuwezesha utafiti kufanyika kwa kasi kubwa.

Kwa kawaida, sampuli za DNA huchukuliwa katika mifupa. Lakini mwaka juzi watafiti walichukua sampuli kutoka katika peremende (chewing gum) iliyokuwa na umri wa miaka 57,000. Uchambuzi uliofanyika ulibaini kuwa mtu aliyetafuna chewing gum hiyo iliyokuwa na urefu wa sentimeta mbili alikuwa mwanamke mwenye ngozi nyeusi, nywele nyeusi na macho ya bluu. Walimpa jina la bandia Lola. Walibaini pia kabla ya kutafuna peremende hiyo, Lola alikuwa amepata mlo wa bata na karanga za kienyeji.

Uchambuzi wa DNA pia umebaini kuwa badala ya kugombana na vizazi vya kale walivyovikuta kama inavyoaminika, binadamu wa sasa walichangamana sana na vizazi hivyo.

Kazi ya kuzichambua taarifa za kijenetiki za mwanadamu huyo wa kisasa ilikamilika mwaka 2010 na kuwafanya wataalamu hao kubaini kuwa mtu huyo wa kale aliyeishi kabla ya kizazi cha sasa, alipitisha jenetiki zake kwenye kizazi cha sasa kwani walichangama kwa kiasi kikubwa. Hivyo, wazo kuwa Homo sapiens alipigana na kizazi cha kale na kukaribia kukiondosha duniani zinaanza kupata shaka.

Utafiti umeonyesha kuwa pamoja na kuchangamana na kizazi hicho cha kale, Homo sapiens pia aliingiliana na kizazi kingine kijulikanacho kama Denisovans, ambacho nacho inaaminika kuwa ni chanzo cha binadamu wa sasa.

Denisovans walitoweka kama miaka 50,000 iliyopita, lakini alitoweka baada ya kupitisha jenetiki zake kwa Homo sapiens, kwa mujibu wa utafiti uliofanyika mwaka juzi.

DNA ya Denisovan pia inapatikana katika jeni za binadamu wa sasa huko Asia na katika baadhi ya visiwa vya Pacific. Hadi asilimia tano ya wakazi wa Papua New Guinea wana DNA zinazoonyesha mabaki ya muingiliano na Denisovans. Watu wa Tibet leo pia wana chembechembe za Denisovan; jambo ambalo pia linaweza kutumika kueleza kwa nini Sherpas wanaweza kuishi katika maeneo ya miinuko mikubwa.

Wanaanthropolojia waligundua mfupa Machi 2010 ambao uchambuzi wake wa kijenetiki ulibaini kuwa Denisovans walikuwa ni moja ya vizazi vya Neanderthals. Hadi sasa mabaki ya Denisovan yamepatikana katika mapango ya Denisova huko Urusi na Tibet.

Tangu kuvumbuliwa kwa Denisovans, wanaanthropolojia pia wamegundua vizazi vingine kadhaa binadamu wa kale barani Afrika na Asia. Kuna uhakika kuwa kizazi kilichozaa binadamu wa sasa kiliishi pamoja na vizazi hivyo, pia waliingiliana.

Aprili 2010, mwanaanthropolojia Lee Berger alitangaza kuwa yeye na mtoto wake walivumbua kizazi kingine kijulikanacho kama Australopithecus sediba, huko Malapa, Afrika Kusini. Australopithecus sediba alikuwa na meno na miguu vilivyofanana na kizazi cha siku za karibuni cha Homo genus. Miguu yao na nyayo zilikuwa zinawawezesha kutembea wakiwa wamesimama wima kwa kutumia miguu miwili tu.

Ugunduzi huu ulifanyika kwa bahati mbaya, kwani wavumbuzi hao walikutana na mabaki hayo bila kutarajia katika pango. Kwa ujumla, kulikuwa na mabaki ya mifupa 1,550 ambayo inaaminika ilitokana na takriban watu 15 ambao waliishi kati ya miaka 330,000 na 250,000 iliyopita. Muda huu unaonyesha kuwa kuna uwezekano vizazi hivyo viliishi pamoja na Homo sapiens wa awali barani Afrika.

Kipo kizazi kingine cha sasa zaidi kijulikanacho kama Homo luzonensis, ambao waliishi katika kisiwa kati ya miaka 50,000 na 67,000 iliyopita. Hao wana vinasaba vinavyofanana na binadamu wa kale kama vile Australopithecus na Homo erectus. Lakini kwa upande mwingine, pia wana vinasaba vinavyolandana na vinasaba vya binadamu wa sasa.

Lakini, kwa mujibu wa utafiti uliofanyika kuanzia 2017, inaaminika kuwa Homo sapiens wa kwanza aliondoka Afrika na kuhamia Asia zaidi ya miaka 120,000 iliyopita – muda wa zamani kuliko ambavyo wanasayansi walikadiria awali.

“Lakini upo uwezekano kuwa kabla ya miaka 60,000 iliyopita viliondoka vikundi vidogo vidogo ambavyo vilikuwa vikihangaika kutafuta hali bora za maisha. Watafiti wamebaini kuwa vikundi hivi vidogo vidogo navyo viliacha vinasaba vyao kwa vizazi vingine katika maeneo waliyopita na kufikisha vinasaba hivyo kwa kizazi cha binadamu wa sasa,” anasema Michael Petraglia, aliyechapisha matokeo ya utafiti huo.

Lakini baadaye kasi ya makundi haya kuhama iliongezeka katika kipindi cha miaka 60,000 iliyopita au baada ya hapo. Kwa mtindo huo, Homo sapiens wakatawanyika katika maeneo ya Ulaya, Asia na Pacific.