Mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi, amemtaja Marco Reus wa Borussia Dortmund kuwa ndiye anayefanya apige mabao ya kiufundi dhidi ya Yanga na Mtibwa Sugar, na kusababisha mabao hayo kuwa gumzo.
  Akizungumza na JAMHURI hivi karibuni jijini Dar es Salaam kwa njia ya simu, Okwi anasema amejifunza aina hiyo ya ufungaji kutoka kwa Reus, kiungo mshambuliaji wa Ujerumani.
  “Huyo ndiye mchezaji ninayempenda na kupenda kumfuatilia mara kwa mara na kujaribu kuzichukua mbinu zake na kuzitumia kutokana na uhodari wake awapo uwanjani,” anasema.
  Anasema kwamba mbinu nyingi anazozipata kwa mchezaji huyo ndiyo nyingi anazopenda kutumia wakati awapo uwanjani, kwani ni mchezaji asiyekata tamaa awapo uwanjani.
  “Siwezi kuchukua kila kitu kutoka kwa Reus kutokana na kuwa mie pia nina mbinu zangu za kupiga pasi nzuri, kumiliki mpira na kupiga mashuti kama ulivyoona katika mechi hizo mbili ya Yanga na Mtibwa,” anasema Okwi
 Pia aliwataka mashabiki wa Simba kutojisikia vibaya baada ya timu hiyo kufungwa na Mgambo, badala yake wavute subira kwani Simba ingali na nafasi ya kutwaa ubingwa.
  Mshambuliaji huyo kwa sasa ana mabao saba katika Ligi Kuu Bara huku akiweka matarajio kufunga zaidi na zaidi kuwania 'kiatu cha dhahabu' anachotwaa mfungaji bora wa Ligi.