Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inaongoza Mafunzo ya siku 5 ya Mawakili wa Serikali jijini Arusha kwa lengo la kuwajengea uwezo, ubobevu na umahiri wa utekelezaji wa majukumu yao Mawakili wa Serikali.

Mafunzo hayo ya pili ya Mwaka mahsusi kwa ajili ya Mawakili wa Serikali ( Bespoke Training for State Attorneys 2025) yanayofanyika jijini Arusha kwa siku 5 kuanzia tarehe 24 hadi 28 Machi, yanahusisha Wakurugenzi wa idara za Sheria za Taasisi Mbalimbali ,Wakuu wa Vitengo vya Sheria na Maafisa Sheria
na yana lengo la kuwaongezea uwezo Mawakili wa Serikali, ubobevu na
Umahiri katika Utekelezaji wa majukumu yao na kuisaidia serikali katika maeneo ya kisheria yenye changamoto.

Awali, akiwakaribisha kwa niaba ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi wa Uratibu na Huduma za Ushauri wa Kisheria Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bi.Neema Ringo amesema, Mafunzo hayo ni muhimu kwa Mawakili hao wa Serikali kwani wamekuwa kiunganishi muhimu kupitia taasisi zao kwa kutoa ushauri wa kisheria kwa serikali na Waajiri wao.

Aliongeza kuwa lengo la Mafunzo hayo, ni kuongeza Umahiri, Ubobevu katika maeneo mbalimbali hususana maeneo ya Mikataba yenye maslahi mapana kwa nchi hasa kwa kipindi hiki ambacho Serikali inapotekeleza miradi mingi ya kimkakati kuelekea Dira ya Taifa ya 2050 .

Aidha, Katika Mafunzo hayo Mawakili hao wa Serikali watakumbushwa wajibu wao wa kulinda maslahi ya Taifa Mikataba ya kitaifa na kimataifa, pamoja na kulinda na kukuza Uwekezaji, Uandishi wa Sheria, Ununuzi na masoko ya kimataifa, Majadiliano na Usimamizi wa Mikataba inayoingiwa na serikali na kuboresha maeneo mbalimbali ya kisheria kwa kuongeza Umahiri wa kada hiyo muhimu kwa maslahi mapana ya Nchi.