Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Serikali kupitia Katibu Mkuu wa Wizara ya Mipango na Uwekezaji imeipongeza Ofisi ya Msajili wa Hazina na Taasisi ya Uongozi kwa kuandaa mafunzo elekezi ya siku tatu kwa watendaji wakuu wapya wa taasisi za umma, yenye lengo la kuwajengea uwezo ili kutekeleza majukumu yao kwa weledi.
Pongezi hizo zilitolewa Wilayani Kibaha, mkoani Pwani, na Dkt. Tausi Kida, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mipango na Uwekezaji, kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Moses Kusiluka, wakati wa hafla ya ufunguzi wa mafunzo hayo kwa watendaji wakuu wapya 111 wa taasisi za umma.
“Mageuzi haya kwenye taasisi na mashirika ya umma ni kielelezo cha uongozi imara chini ya Ofisi yako. Natoa wito wa kuendeleza jitihada hizi ili tuongeze ufanisi,” alisema Dkt. Kida.
Aliongeza kuwa, “Sote tunafahamu kuwa taasisi na mashirika ya umma yameanzishwa ili kutoa mchango katika kusaidia serikali kuchochea maendeleo, kuongeza mapato, kuzalisha, kuongeza ajira, na kutoa huduma za msingi kwa wananchi.”
Aidha, viongozi wametakiwa kuzingatia mambo tisa muhimu ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu kwa viwango vinavyokusudiwa. Mambo hayo ni pamoja na kuzingatia sheria na kanuni zinazoongoza viongozi wa serikali, kujenga na kuimarisha uwezo wa taasisi katika kujifunza nyanja mbalimbali, pamoja na usimamizi madhubuti wa rasilimali watu, fedha, na rasilimali nyingine za serikali. Pia, ni muhimu kujenga uhusiano wa kiutendaji wenye afya kati ya viongozi na watumishi wanaowasimamia.
Viongozi hao pia wameaswa kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kutumia vyanzo vipya na kuongeza vyanzo vingine ili kuchangia kwenye mfuko mkuu wa serikali, kuimarisha mifumo ya utoaji huduma, na kujenga maadili bora kazini ili kuwezesha utoaji wa huduma bora.
“Ndugu watendaji wakuu, ni muhimu mkumbuke kuwa taasisi na mashirika mnayoongoza ni mali ya umma, hivyo umma unatarajia kuona matokeo chanya na yenye maslahi mapana,” aliongeza Dkt. Kida.
Kwa upande wake, Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, alisema kuwa iwapo watendaji wakuu watatekeleza kwa umakini ujuzi na mbinu watakazopata katika mafunzo hayo, wataweza kusimamia na kuziendesha taasisi zao kwa ufanisi, hivyo kufikia malengo ya serikali.
Programu ya mafunzo hayo ya siku tatu iliandaliwa kwa ushirikiano wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, Taasisi ya Uongozi, na wadau kutoka sekta ya umma. Kwa mujibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, Tanzania ina taasisi, mashirika ya umma, na wakala wa serikali 309, yenye uwekezaji wa shilingi trilioni 75.8.