Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
OFISI ya Mganga Mkuu Mkoa wa Dar es Salaam kwa kushirikiana na USAID Afya Yangu, Mama na Mtoto wametoa mafunzo kwa akina mama 50 kutoka Wilaya nne za Mkoa huo.
Wilaya hizo ni Temeke, Kinondoni, Ilala na Ubungo ambapo wamepatiwa elimu kuhusu malezi na viashiria vya utoaji huduma ya afya kwa mtoto.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mratibu wa Huduma ya Afya na Uzazi wa Mtoto Mkoa wa Dar es Salaam, Agnes Mgaya amesema mafunzo hayo yamehusisha kina mama wenye watoto chini ya miezi sita wenye uzazi wa kwanza au wa pili.
“Mafunzo yalikuwa yakilenga kukumbushana viashiria muhimu katika utoaji huduma ya afya na mtoto ili wapate elimu inayoweza kusaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi,” amesema.
Mgaya amesema katika mafunzo hayo walikuwa wanawapa elimu ya umuhimu wa kumyonyesha maziwa ya mama pekee ndani ya kipindi cha miezi sita ya mwanzo bila kumpatia vyakula vya ziada.
“Pia tumewafundisha jinsi ya kutumia uzazi wa mpango baada ya kujifungua ili kuzuia kupata mimba nyingine ndani ya miaka miwili katika kuruhusu mtoto kukua na kuwa na afya bora. Pamoja na kuhakikisha wanawapeleka watoto kupata chanjo zote kama inavyoshauriwa.
“Sambamba na hilo, pia tumewaambia umuhimu wa kumpeleka mtoto mchanga katika kituo cha kutolea huduma za afya mara tu unapogundua dalili za ugonjwa na sio kumpa dawa ovyo,” amesisisitiza.
Ofisa Mabadiliko ya Tabia wa Mradi huo, Patricia Mkude amesema waliungana na Mkoa huo kutoa mafunzo hayo kupitia jukwaa la Naweza katika kifurushi cha uzazi na malezi ya watoto chini ya miaka mitano kutoa elimu hiyo katika kuunga mkono juhudi za serikali.
“Malengo ni kuwawezesha wazazi na walezi kuwapatia taarifa, motisha, ujuzi na msaada kutoka kwa mama rika na jamii wanaohitaji ili kufuata na kudumisha tabia chanya za kiafya zinazolenga kulinda afya na ustawi wa jumla wa mtoto kuanzia kuzaliwa hadi miaka mitano kwa kuzingatia siku 1000 za mwanzo,” amesema Patricia
Naye, Mkazi wa Kinyerezi, Sozy Edward ambaye ni miongoni mwa wamama walioshiriki mafunzo hayo, amesema kupitia elimu hiyo wamejifunza mengi ikiwemo ukatili wa kijinsia.
“Nawashukuru sana kwa kutupatia eimu hii kwani nimejifunza vitu vingi ambavyo nilikuwa sivijui…Kwa mfano umuhimu wa kupata chanjo ya kumkinga mama dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kupitia mafunzo haya nimesikia kwa mara ya kwanza, pia nimeweza kujua umuhimu wa kunyonyesha mtoto ndani ya muda wa nusu saa.
“Kuna habari nyingi mtaani mtoto anatakiwa apate maji lakini tumelezewa maziwa ya mama yanamtosha mtoto kupata virutubisho vyote kuanzia maji na chakula kwa hiyo mama anatakiwa kumnyomyesha mtoto hasa maziwa ya kwanza,” amesema.
Naye, Giveness Abbas kutoka Keko amesema kupitia mafunzo hayo amepata elimu namna ya kuzingatia lishe ya mtoto katika kujenga afya yake.
“Tumeelezwa jinsi ya kutumia uzazi wa mpango, kutumia chandarua kilicho na dawa na jinsi ambavyo mama na baba tunaweza ‘Kushirikiana mwanzo wa mimba mpaka katika malezi ya mtoto,” amesema.