Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imesema imesajili miradi zaidi ya 9,061 ikiwemo ya hifadhi ya mazingira yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 37.55.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo ametoa kauli hiyo wakati akichangia hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Amesema mafanikio hayo ni kutokana na Sera nzuri ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayovutia wawekezaji ambayo inawezesha ujenzi wa uchumi na hifadhi ya mazingira.

Halikadhalika, Dkt. Jafo amesema kuwa kupitia biashara ya kaboni jumla ya miradi 50 imesajiliwa ambapo tayari Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi imepokea shilingi bilioni 14 ambazo zimenufaisha vijiji mbalimbali.

Amesema mafanikio hayo ni kutokana na Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, Oktoba 2022 iliandaa Kanuni na Mwongozo wa Taifa wa Usimamizi wa Biashara ya Kaboni nchini kwa lengo la kuweka utaratibu wa kuzingatia wakati wa utekelezaji wa miradi mipya.

Waziri Jafo amepongeza na kuishukuru Serikali kwa utekelezaji wa miradi katika sekta mbalimbali ambayo kimsingi inagusa moja kwa moja hifadhi ya mazingira ikiwemo usajili wa miradi ya maji 222 na ya ujenzi 1,894.

Amesema kuwa Serikali imesajili miradi ya nishati 1,340 ambayo Ofisi ya Makamu wa Rais inaona kuwa imeleta tija katika kuchagiza upatikanaji wa nishati safi ya kupikia ambapo ajenda ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inafikiwa.

Kutokana na hatua hiyo amesema bajeti hiyo imeakisi uhalisia hasa katika sekta ya mazingira, sanjari na hilo amewaomba wananchi kushiriki kikamilifu katika masuala ya hifadhi na utunzaji wa mazingira hususan mabadiliko ya tabiachi.

“Niwaombe ndugu zangu tushikamane hasa katika kushughulikia masuala ya mazingira kwasababu nchi yetu inapoteza takriban Dola za Marekani milioni 500 kwa mwaka kwa ajili ya kushughulikia miradi ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi, hili jambo ni kubwa kwa hiyo Watanzania wote lazima tushirikiane katika utunzaji wa mazingira,“ amesisitiza.