Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Kilimanjaro imemfikisha mahakamani Ofisa Ardhi wa Wilaya ya Hai, Wilbert Mayila, kwa tuhuma za kudai na kupokea rushwa ya Sh milioni moja kutoka kwa ofisa wa jeshi mstaafu ili amsaidie kupata hati ya kumiliki kiwanja.

Alifikishwa mahakamani hapo hivi karibuni na kusomewa shitaka la kudai na kupokea rushwa kutoka kwa John Mushi kwa maelezo kuwa angemsaidia kupata hati ya kumiliki kiwanja huku akifahamu kuwa kiwanja hicho ni mali ya Shirika la Umeme nchini (Tanesco).

Mayila alisomewa mashitaka hayo na Wakili wa Takukuru, Suzan Kimaro, mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Makahama ya Wilaya, Devota Msofe.

Hata hivyo alikana tuhuma hizo na kuachiliwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na mdhamini mmoja aliyesaini dhamana ya Sh milioni mbili.

Mayila ameshitakiwa chini ya Kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 16, mwaka huu itakapotajwa. Upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Katika hatua nyingine, Takukuru imewatia mbaroni mwenyekiti wa Kijiji cha Ruvu Jiungeni katika Wilaya ya Same, Kilaseko Sokoine, pamoja na Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Mohamed Sanja, wakidaiwa kuomba na kupokea rushwa.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Holle Makungu, inasema viongozi hao wa serikali ya kijiji waliomba rushwa kutoka kwa ukoo wa Ndorosi ili kutoa dhamana baada ya kuwasweka ndani katika mgogoro wa mipaka.

“Uchunguzi wa Takukuru unaonyesha kwamba kabla ya kuwakamata wanandugu hao (viongozi) walituma Kamati ya Uchumi na Mipango ya Kijiji cha Ruvu Jiungeni kwenda Kitongoji cha Mvungwe kupima shamba la ukoo wa Ndorosi lililokuwa likidaiwa kuwa kubwa kuliko walilopewa na Serikali ya Kijiji mwaka 2008,” inasema taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa Takukuru, wajumbe wa kamati hiyo walirejesha taarifa kwa mwenyekiti wa serikali ya kijiji na mtendaji wake kuwa kazi ya kupima shamba haikufanyika kwa kuwa walitishiwa kupigwa na wamiliki wa shamba hilo.

Mkuu huyo wa Takukuru anasema kuwa baada ya viongozi hao kupewa taarifa hiyo waliwaita ndugu watatu wa ukoo huo na kuwapeleka Kituo cha Polisi Makanya na kuwafungulia jalada la kutaka kusababisha uvunjifu wa amani na walidhaminiwa.

“Huku wakifahamu kuwa lalamiko hilo wamekwisha kulifikisha polisi, Sokoine kwa kushirikiana na Mohamed Sanja waliwaita ndugu hao watatu na kuwataka wadhaminiwe tena ofisi ya kijiji kisha wakawataka kutoa pesa taslimu Sh 900,000 ili wasiwachukulie hatua zaidi za kisheria,” inasema taarifa hiyo.

Baada ya kudaiwa kiasi hicho cha fedha, ndugu hao walitoa taarifa Takukuru na mtego uliandaliwa na viongozi hao kutiwa mbaroni wakiwa tayari wamekwisha kupokea Sh 700,000.