Rais Barack Obama wa Marekani amekiri kwa mara ya kwanza kwamba serikali yake ilishindwa katika uvamizi wa Libya mwaka 2011. Amesema hilo huenda ndilo “kosa kubwa” zaidi alilolitenda wakati wa utawala wake.
Obama amesema Marekani haikuwa na mpango mahsusi wa jinsi Libya itakavyotawaliwa baada ya kuuliwa kwa mtawala wake, Kanali Muammar Gaddafi tarehe 20 Oktoba 2011. Obama alisema haya katika mahojiano ya hivi majuzi na runinga nchini Marekani. Matokeo yake ni kuwa Libya imetumbukia katika dimbwi la matatizo baada ya nchi hiyo kusambaratika.
Mwanzoni, Shirika la Kujihami la Mataifa ya Magharibi (NATO) walidai kuwa lengo lao lilikuwa kuwalinda raia wa Libya ili wasishambuliwe na majeshi ya Gaddafi. Lakini baada ya muda wakaamua wampindue Gaddafi na kuikabidhi nchi kwa waasi.
Siku za nyuma Obama amewahi kuwalaumu wenzake wa NATO. Amesema Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron hakufanya matayarisho ya kutosha walipoanza uvamizi wa Libya. Pia Obama alimlaumu Rais wa wakati huo wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy.
Matokeo ya “makosa” yote haya ni kuwa Libya ambayo ni nchi iliyo na utajiri mkubwa wa mafuta, sasa imemeguka vipande vinavyotawaliwa na makundi ya waasi waliopewa silaha, mafunzo na fedha na NATO.
Baada ya majeshi ya NATO na waasi kumuua Gaddafi na kupindua serikali yake, waasi wakaanza kugombania ngawira. Kila kikundi chenye silaha kikadai maeneo yake na ndipo wakaanza kushambuliana na kuwashambulia raia. Wakati wa mauaji ya Gaddafi, Benki Kuu ya Libya ilikuwa na akiba ya dola bilioni 85. Waasi wakaanza kupora hazina hii ya wananchi na ndipo vita vipya vikaanza huku NATO wakishangilia.
Kikundi kilichojiita Dola ya Uislamu (ISIS) kikawazidi nguvu wengine. Dola bilioni 1.1 za walipa kodi wa Marekani zikatumika kuisambaratisha Libya na kusababisha kukua kwa ISIS siyo tu Libya, bali katika Bara la Afrika na kwingineko.
Kikundi cha mujahidina kilichosaidiwa na NATO ndio baadaye wakaja kumuua Balozi Christopher Stevens wa Marekani na wasaidizi wake watatu mjini Benghazi tarehe 11 Septemba 2012. Marekani ikabidi wafunge ubalozi wao Tripoli na kuikimbia Libya.
Kosa walilofanya Marekani huko Libya walifanya pia Afghanistan na Iraki. Ukiachia raia wa nchi hizo waliouawa na nchi kusambaratishwa, Marekani nayo ikapoteza askari wake 7,000 na wengine wengi kujeruhiwa vibaya.
Wakati Obama anajutia alichokifanya Libya, anayofanya huko Syria ni mabaya zaidi. Katika nchi hiyo, licha ya maelfu ya raia waliouawa, milioni 12 hawana mahali pa kuishi na milioni nne wameikimbia nchi yao; wengi wakienda Ulaya ambako wanapigwa mabomu na polisi. Mwaka jana tu wamekufa raia 1,500.
Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) linasema nchini Libya wameibuka mujahidina 6,000 wa kikundi cha ISIS. Wanasema nchini Syria wako kati ya 20,000 na 30,000 ingawa wengine wanakisia ni 50,000 ukichanganya na walioko Iraki. Wote hawa wanaeneza harakati zao hadi Ulaya ambako wana mawakala wao. Si ajabu kuwa washambuliaji wa mjini Paris na Brussels walipata mafunzo yao huko Syria. Huu ndio uongozi wa kina Bush, Blair, Obama na Cameron.
Wakati Obama anazungumzia ‘makosa’ yaliyofanyika, Hillary Clinton anaonekana akichukua msimamo tofauti. Yeye wakati anagombea urais nchini Marekani amekuwa akisifu utumiaji wa majeshi huko Libya na kusema Marekani imetumia vilivyo nguvu zake za kijeshi.
Mwaka 2011 Clinton alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Obama. Wakati huo baada ya Gaddafi kuuliwa kikatili na waasi wakisaidiwa na majeshi ya NATO, Clinton alionekana katika TV akisherehekea na kufurahia mauaji hayo.
Clinton ndiye aliyemshauri Obama kuidhibiti anga ya Libya ili Gaddafi asiweze kusafirisha askari wake au kuwashambulia waasi. Matokeo yake waasi waliweza kujiimarisha kwa kupokea misaada ya silaha na mafunzo.
Kwa mujibu wa gazeti la The Washington Post Clinton alishauriwa na wanasheria wa wizara yake kuwa kuivamia Libya ni uhalifu wa sheria ya kimataifa. Makamu wa Rais Joe Biden na mshauri wa Obama wa mambo ya Usalama wa Taifa, Tom Donilon nao walipinga mpango wa kuivamia Libya.
Clinton alipuuza ushauri wao na akafaulu kumfanya Obama atoe misaada ya kijeshi na kifedha kwa waasi. Mabilioni ya dola yaliyokamatwa kutoka akaunti za serikali ya Gaddafi yalikabidhiwa kwa waasi.
Katika mkutano nchini Uturuki, Clinton pia alizishawishi serikali 30 za Ulaya na Uarabuni kuwasaidia waasi.
Mara nyingi vyombo vya propaganda vya magharibi vimekuwa vikitulisha uongo kuwa uvamizi wa Marekani na NATO katika nchi kama Iraki, Libya na Syria ni kwa madhumuni ya kuondoa udikteta na kuleta demokrasia.
Ukweli ni kuwa mashambulizi haya ni matokeo ya mikakati iliyopangwa kwa muda mrefu ili kutimiza lengo lao la kisiasa na kiuchumi.
Ushahidi mmoja ulitolewa na Jenerali Wesley Clark wa Marekani, aliyeongoza majeshi ya NATO akiwa Kamanda Mkuu wakati wa uvamizi wa Yugoslavia mnamo 1999.
Yeye alitamka kuwa Marekani siku zote ilikuwa na mpango wa kuzivamia nchi saba katika muda wa miaka mitano. Nchi zenyewe alizozitaja ni Iraki, Syria, Lebanon, Libya, Somalia, Sudan na mwishowe Iran.
Mwaka 2004 Jenerali (mstaafu) Clark alijaribu kugombea urais wa Marekani kupitia chama cha Democratic, lakini hakupitishwa.
Mwaka 2007 mtangazaji Amy Goodman wa runinga ya Democracy Now alimuuliza Clark kuhusu mkakati huu. Clark akasema alipokuwa jeshini alitembelea makao makuu ya wizara ya majeshi jijini Washington na huko akauona waraka wa siri ulioelezea mkakati huo.
Jenerali Clark alisema ni jambo la kawaida kwa marais wa Marekani kuanza kugundua makosa yao baada ya kuachia madaraka. Kwa mfano Rais George W. Bush katika kitabu chake cha 2010 anazungumzia uvamizi wa Iraki akisema alifanya makosa. Halafu naye Rais Clinton mnamo mwaka 2008 alisema alifanya makosa makubwa wakati wa mauaji ya halaiki nchini Rwanda mwaka 1994.
Kuhusu uvamizi wa Iraki hata Waziri Mkuu wa Uingereza, wa wakati huo, Blair aliomba radhi kwa kutoandaa mipango baada ya kumuondoa Saddam Hussein.
Obama anaungama makosa yake ya Libya, lakini kosa lake kubwa (tena kosa la jinai) ni kuungana na Rais Sarkozy wa Ufaransa na Waziri Mkuu Cameron wa Uingereza katika kuivamia Libya kinyume cha sheria ya kimataifa na kinyume cha azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Uvamizi wa Iraki wa mwaka 2003 umesababisha raia milioni moja kupoteza maisha. Kabla ya hapo vikwazo vya NATO vilisababisha raia milioni moja wa Iraki kufa. Ndio maana kuna shinikizo kuwa kina Bush (mkubwa na mdogo) na Tony Blair wa Uingereza wafikishwe Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita.
Na kuhusu Libya kinachofichwa ni kuwa sababu halisi ya kumuua Gaddafi siyo udikteta, bali ni kwa sababu yeye alikuwa anaanzisha mawasiliano ya satelaiti kwa Afrika nzima ili tuache kutegemea kampuni za magharibi. Halafu pia kwa sababu ya ‘kosa’ la kuuza mafuta yake China pamoja na kukataa kuruhusu vituo vya kijeshi vya Marekani nchini mwake.
Gaddafi pia alikuwa akianzisha benki kwa bara zima la Afrika ili tuache kutegemea ‘wafadhili’ wa magharibi. Yote haya yaliwakwanza sana watawala wa NATO.
Baada ya Marekani na NATO kuisambaratisha Libya, sasa wanakabidhi kazi ya kuikarabati nchiyo kwa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, akiwa mwakilishi maalum wa Umoja wa Afrika (AU).
Wakati NATO walipoivamia Libya ni AU ndiyo iliyopaza sauti yake ikipinga. Ilikuwa tayari kuingilia kati na kuzungumza na Gaddafi ili yamalizwe bila ya vita. Ujumbe ulitumwa hadi Libya ukaonana na Gaddafi. NATO waliipuuza AU. Leo wanaifadhili AU eti waikarabati nchi hiyo waliyoibomoa.
Tusidanganyike na radhi wanazoomba. Hatua za kisheria lazima zichukuliwe kama zinavyochukuliwa dhidi ya watawala wa Kiafrika.