Hatua ya Rais wa Marekani, Barack Obama, kutembelea mitambo ya kuzalisha umeme ya Symbion Ubungo jijini Dar es Salaam, imeamsha mjadala mzito katika jamii uliowafanya Watanzania kuanza kumhurumia Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, wakiona alionewa.

Lowassa alijiuzulu Februari 7, 2008 baada ya Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe kutoa taarifa bungeni iliyodai kuwa Lowassa alishinikiza kampuni ya Richmond kupewa zabuni ya kufua umeme nchini, wakati haikuwa na uwezo.

 

Baada ya taarifa ya Mwakyembe na Lowassa kujiuzulu, yaliibuka malumbano makali nchini, ambapo Kampuni ya Richmond iliuhuisha mkataba wake kwa Kampuni ya Dowans ikazalisha umeme kwa miezi 18.

 

Kampuni ya Dowans nayo hatimaye mkataba wake ulivunjwa kwa shinikizo la Bunge ikaenda mahakamani na kuishinda Tanesco, kwa Mahakama ya Biashara ya Kimataifa kuiambia Tanesco kuwa Dowans ilikuwa na mkataba halali, hivyo iilipe fidia wastani wa Sh bilioni 95.

 

Wakati mjadala ukiwa mkubwa, Kampuni ya Dowans ilitangaza nia ya kuiuzia Serikali mitambo kwa wastani wa Sh bilioni 57, siasa zikaingia kati Tanesco ikazuiliwa kununua mitambo hiyo chini ya Dk. Idrisa Rashid na mitambo hiyo ikanunuliwa na Kampuni ya Kimarekani ya Symbion kwa Sh bilioni 115. Kampuni hiyo sasa inaonekana ni mkombozi kwa kuzalisha umeme nchini ikitumia mitambo hiyo iliyodaiwa kuwa chakavu.

 

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe, ambaye wakati huo alishauri Tanesco inunue mitambo hiyo, juzi alishiriki mjadala mzito unaoendelea kwenye mitandao ya kijamii na kudai kuwa Lowassa alitaka mkataba wa Richmond uvunjwe akazuiliwa na mamlaka ya juu.

 

“EL was a PM (Edward Lowassa alikuwa Waziri Mkuu) anahusika na maamuzi yote. Nyaraka nilizonazo zinaonesha kuwa aliagiza mkataba uvunjwe, lakini akapata agizo jingine tofauti. Nina dokezo lenye saini yake kuhusu hilo. Yeye hili halisemi, labda anamlinda bosi wake.

 

“Lazima tujue, lini Richmond na Dowans walikuwa kitu kimoja? Toka mwanzo? … Wamarekani wanahusika kuanzia lini? Kwanini Condoleezza Rice aliandika barua kutetea Richmond? Hizo barua kwanini hazipo public (hazitangazwi)? Huu mradi kwa nini ulianzia na kuishia Marekani? Texas? Bush? Condi? Hillary? Obama? Amb. Wilson?… Tukune vichwa,” anasema Zitto katika andiko lake.

 

Aliyekuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, Hilary Clinton, alikuwa wa kwanza kuzindua mitambo ya Symbion baada ya kuwa imenunuliwa kutoka Dowans mwaka 2010, na sasa Obama amesimama kwenye mitambo hiyo Ubungo kuzindua mpango wa umeme Afrika.

 

Rais Kikwete alipata kukaririwa akisema hawafahamu wamiliki wa Dowans na wala hana sababu ya kuwafahamu.

 

Wengi wa wanaochangia mjadala unaoendelea, wanarejea kauli ya Lowassa aliyoitoa kwenye Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), akimhoji Rais Kikwete ni kipi katika Richmond alichofanya bila baraka au maelekezo yake? Kikwete hajawahi kujibu lolote hadi sasa.