Joyce NdalichakoJanuari 20, mwaka huu, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, alitoa taarifa kuhusu matumizi ya GPA katika upangaji madaraja ya ufaulu. Kwa kuzingatia umuhimu na nia njema ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kufufua na kuboresha hali ya elimu nchini, Gazeti la JAMHURI limeonelea vema kuichapisha taarifa hiyo neno kwa neno ili wasomaji wapate kufahamu vema maudhui na dhamira njema ya Waziri Profesa Ndalichako. 

 

1. Utangulizi

Baraza la Mitihani la Tanzania lina jukumu la kuendesha mitihani ya Taifa na kutunuku vyeti kwa wahitimu. Chombo hiki ni muhimu sana katika kutoa mwelekeo sahihi kwa Taifa kuhusu ubora wa wahitimu katika Elimu ya Msingi na Sekondari.  Baraza la Mitihani ni chujio linalowezesha Serikali kufanya maamuzi ya mahali pa kuwapanga wahitimu wanaomaliza Elimu ya Msingi, Kidato cha Nne na Sita. Kwa hiyo unapozungumzia ubora wa elimu, huwezi kuacha kuangalia vyombo vilivyoundwa kisheria kwa ajili ya kufanya upimaji katika ngazi mbalimbali za elimu kwani utendaji wa vyombo hivyo una athari kubwa katika sekta ya elimu.

 

2. Utaratibu wa Matumizi ya GPA kupanga Matokeo ya Taifa

Utaratibu wa kutumia GPA ulianza mwaka 2014 katika matokeo ya kidato cha sita na kidato cha nne.  Kabla ya kuanza kutumia mfumo wa GPA, Baraza la Mitihani la Tanzania lilitoa mwongozo kuhusu mfumo huo ambapo alama za ufaulu kwa kidato cha 4 na 6 na alama za ufaulu kwa mitihani ya ualimu zilikuwa kama ifutavyo:

 

Yaliyojitokeza Kutokana na Matumizi wa GPA

Tangu kuanza kutumika mfumo wa GPA umekuwa na changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza na kusababisha malalamiko kama ifuatavyo:

i) Baadhi ya watahiniwa waliopitia katika mfumo huo waliofaulu Mtihani wanaonesha kiwango kidogo cha maarifa kuliko kiwango chao cha ufaulu.  

ii) Uwepo wa Gredi E kwenye alama za Ufaulu wakati haihesabiki katika upangaji wa GPA. Hali hii inaleta mkanganyiko na  kunawafanya watahiniwa waliopata E zote kwenye mtihani kujiona kuwa hawatendewi haki kwani wenye D mbili na F zote  wanahesabika wamefaulu mtihani;

iii) Matumizi ya  pointi tofauti za mfiko kwenye madaraja ya ufaulu kwa ngazi mbalimbali za Elimu kunaleta mkanganyiko kwani inakuwa vigumu kuelezea tafsiri ya madaraja hayo.  Kwa mfano “Distinction” ya Kidato cha Nne inaanzia point 3.6 wakati ya Ualimu inaanzia 4.4  

 

ZIARA YA WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI,TEKNOLOJIA NA UFUNDI 

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi alifanya ziara Baraza  la Mitihani Tanzania  tarehe 7/01/2016 ambapo pamoja na mambo mengine alilitaka Baraza kutoa ufafanuzi, katika kipindi kisichozidi siku saba kuhusu sababu za kufanya  yafuatayo:

i) Kuacha kutumia  mfumo wa “Divisions” na kuanza kutumia mfumo wa GPA katika kutunuku matokeo ya CSEE na ACSEE;

ii) Kuanzisha karatasi  ya pili (Paper 2) ya Watahiniwa wa kujitegemea wa kidato cha Nne na cha Sita  iwe sehemu ya alama endelevu.

 

Maelezo yaliyowasilishwa yamebainisha yafuatayo:

5.1 Kuhusu sababu za kuanzisha mfumo wa GPA 

Maelezo yaliyowasilishwa yamejikita zaidi katika kuelezea utaratibu uliotumika kufanya mabadiliko badala ya kueleza sababu za msingi za mabadiliko kama ilivyotakiwa.  Kwa muhtasari taarifa yao imeeleza kuwa yafuatayo:

i) Utaratibu huo ulitokana na maoni ya wadau

Taarifa imebainisha kuwa uanzishwaji wa mfumo wa “Grade Point Average” (GPA) ulitokana na maoni ya wadau bila kuwataja wadau husika na wala kueleza sababu walizozitoa. Aidha taarifa ya utafiti uliofanywa na Wizara ya Elimu haijataja idadi ya wadau waliojaza madodoso na wala haioneshi mikutano ya kupata maoni ya wadau ilihusisha watu gani, ilifanyikia wapi na ilifanyika lini.

 

ii) Maelekezo ya Wizara ya Elimu kwa NECTA

Taarifa ya Baraza imebainisha kuwa kutokana na taarifa ya wadau, Wizara ililiagiza Baraza la Mitihani kuandaa mfumo wa GPA ili uanze kutumika katika matokeo ya Kidato cha Nne 2014.  Hata hivyo, uchambuzi wa nyaraka zilizowasilishwa unaonesha kuwa Wizara ilikuwa imelielekeza Baraza liauandae mfumo huo na kuuwasilisha kwa Kamishna wa Elimu ili upate kibali cha Serikali kabla ya kuanza kuutumia.  Hata hivyo, jambo hilo halikufanyika na badala yake Baraza la Mitihani lilianza kutumia utaratibu huo mwaka 2014 bila kibali cha Kamishna wa Elimu kama inavyotakiwa. 

 

iii) Manufaa ya Kutumia mfumo wa GPA

Baraza la Mitihani limeeleza kuwa faida mojawapo ya mfumo wa GPA ni kuwa unaeleweka kwa urahisi na wadau mbalimbali jambo ambalo linapingana na maoni ya wadau yanayojitokeza kwenye vyombo vya habari kuhusu suala hilo yanayowasilishwa  Wizara ya Elimu.

Aidha Baraza la Mitihani limeeleza kuwa mfumo wa GPA umerahisisha Udahili wa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu (Central Admission System – CAS) jambo ambalo si sahihi kwa kuwa mfumo wa CAS ulianza kutumika Aprili 2010 wakati mfumo wa GPA ulianza kutumika mwaka 2014. Aidha, mfumo wa Udahili huzingatia masomo mawili ya fani anayotarajia kusoma mwanafunzi na siyo ufaulu wa jumla.

Kwa ujumla maelezo ya Baraza la Mitihani hayajaonesha udhaifu wa mfumo wa awali wa “division”.

 

5.2 Kuhusu sababu za Kuongeza “Paper” ya pili kwa watahiniwa wa Kujitegemea kama mbadala wa Upimaji Endelevu (Continuous Assessment – CA)

  Baraza la Mitihani limeeleza kuwa “Paper 2” kama mbadala wa CA kwa watahiniwa wa kujitegemea.  Hata hivyo, kitaalamu “Paper 2” haiwezi kuitwa alama ya maendeleo ya kila siku kwa kuwa inafanyika sambamba na mtihani mingine ya mwisho (summative assessment). Alama ya maendeleo ya kila siku inatakiwa itokane na mazoezi ya mara kwa mara yanayotolewa na mwalimu kwa wanafunzi wake (formative assessment).

 

6.0  Maoni na Wizara

i) Kwa kuzingatia uchambuzi wa taarifa iliyowasilishwa na Baraza la Mitihani, hawajatoa sababu za msingi za maamuzi kuhusu kubadilisha utaratibu wa kupanga matokeo kutoka ule wa zamani wa divisheni kwenda utaratibu wa sasa wa GPA. 

ii) Kuhusu “Paper 2” kwa watahiniwa wa kujitegemea, maelezo ya Baraza la Mitihani hayana sababu za kitaaluma na uanzishwaji wake haukuzingatia utaratibu sahihi wa Upimaji Endelevu wa wanafunzi. 

iii)  Kitendo cha Baraza la Mitihani la Tanzania kuingiza mfumo wa GPA katika marekebisho ya Kanuni zake yaliyosainiwa na Waziri tarehe 28/10/2015 na kuchapishwa tarehe 06/11/2015 kwenye Gazeti la Serikali (GN 509) wakati mfumo ulianza kutumika mwaka 2014 kinaonesha  kuwa utekelezaji wa mfumo wa matumizi ya GPA ulianza kufanyika kabla ya kanuni  kukamilika na wala hapakuwa na waraka wa Kamishna wa Elimu kuruhusu matumizi ya mfumo huo wakati umeanza kutumika. 

Kufuatia uchambuzi uliofanywa na kwa kuzingatia kuwa  Baraza lilikuwa limepanga kufanya mapitio ya mfumo huo mwaka huu 2016,  kwa mamlaka niliyonayo chini ya Kifungu cha 20 cha Sheria ya Baraza la Mitihani Tanzania, Sura ya 107, naliagiza Baraza kufanya yafuatayo: 

i) Kupitia mfumo unaotumika sasa wa Wastani wa Alama (GPA) kwa lengo la kurudi kwenye Mfumo wa awali wa Divisheni. Aidha viwango vya ufaulu vizingatie azma ya nchi yetu ya kuelekea kwenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

ii) Kufuta karatasi ya pili ya watahiniwa wa kujitegemea ambayo imeanzishwa kama alama ya maendeleo wakati huo ni mtihani wa mwisho na hivyo hauna sifa ya kuitwa “alama za maendeleo”.

 

8.0  HITIMISHO

Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi inapenda kusisitiza kuwa ina lengo thabiti la kusimamia ubora wa Elimu katika ngazi zote za elimu nchini. Hata hivyo, Wizara haiwezi kufikia azma yake hiyo muhimu bila kuhakikisha kuwa viwango vya ufaulu vinavyotumika vinawezesha kutoa wataalamu wenye stadi, ujuzi na maarifa stahiki badala ya kuwa na wahitimu wengi wenye vyeti lakini hawawezi kukidhi mahitaji katika soko la ajira na hata katika mazingira wanayoishi.

Wizara inaamini kuwa elimu ndiyo hazina ya nchi yetu. Taifa letu haliwezi kusonga mbele bila kuwa na elimu bora na upimaji thabiti wa wahitimu. Aidha usalama wa nchi yetu unategemea sana elimu na mitazamo chanya ya wananchi. Hivyo Wizara yangu itasimamia zaidi mifumo ya utoaji wa elimu nchini na kuweka utaratibu madhubuti wa kufuatilia kwa karibu kinachoendelea darasani ili kuhakikisha kuwa tunakuwa na wahitimu wanaokidhi matarajio ambao wataweza kuchangia maendeleo ya Taifa letu. 

Asanteni sana kwa kunisikiliza.

 

Prof. Joyce L. Ndalichako

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi

20/01/2016