“Kauli yako utoayo mitaani, inanifikia nduguyo
Ingawa unafikiri sikufahamu, unitetayo sikia
Nakuonya uongo mbona haithamini elewa
Unajitangaza u-mtenda mema, mengi kujisifia ya uongo,
Watoto wamekukimbia nyumbani, umebaki na wajukuu pia watasambaa.
Iliyobaki nitamuliza shemeji, kuna kasoro gani hapo nyumbani.
-Aaah! Aaah ! Pole mzee. Watoto wanakimbia nini huko nyumbani?
-Jirekebishe na waliosalia, pole mzee
-Nitamuliza shemeji kuna kasoro gani.”
Maneno haya yamo katika wimbo ‘Watoto wanakimbia nyumbani.’ Ni utunzi wake marehemu Shaaban Dede, alipokuwa na bendi ya DDC Mlimani Park Orchestra -Wanasikinde, miaka ya 1980.
Nimeukumbuka wimbo huu kutokana na kuhamahama kwa baadhi ya viongozi na wanachama wa vyama vya siasa nchini. Kutoka chama fulani kwenda kingine. Huku tuhuma kadhaa zikitolewa dhidi yao na watu mbalimbali kuwa wao ni wasaliti, vibaraka, wenye tamaa na kadhalika.
Lipo kundi la wanachama na viongozi kutoka Chadema, CUF na ACT – Wazalendo, wakiwamo wanachama, madiwani, wabunge, makatibu na wenyeviti ambao wanahama kwenda vyama vingine. Iwe ndani ya chama chenyewe au katika jumuiya za chama. Hapa ipo haja ya kuwauliza wenyeviti wa vyama, kuna nini huko?
Sababu zinazotolewa ni nyingi. Zipo zinazoelezwa kurubuniwa, kuhongwa (rushwa), ahadi ya kupewa uongozi au madaraka mapya huko waendako. Inawezekana. Lakini ushahidi dhahiri haupo. Umma haujathibitishiwa. Isipokuwa kasoro za watu kuhama vyama zipo, ndiyo maana wanahama.
Mwanadamu anapohama anafanya mabadiliko na anakuwa na sababu. Ama amechoshwa na mazingira, madhara au mazoea. Anafanya mabadiliko ya makazi, kazi na itikadi. Anayehama anajaa furaha. Anayeshuhudia uhamaji anashangaa na anayehamwa anapata mfadhaiko.
Watoto wanapohama nyumbani, wafanyakazi wanapoacha kazi au wanachama na viongozi wanapohama chama, ni dhahiri shahiri kuna kasoro katika maeneo hayo. Ni lazima kwa mzazi, meneja au mwenyekiti kujiuliza na kutoka na majibu yenye maana si kuleta blaa blaa.
Wanasikinde wanauliza: “Kuna kasoro gani hapo nyumbani?” Wanashangaa kuwaona watoto wanakimbia nyumbani na wajukuu kubakia. Wanasema mjirekebishe kwani na hao waliosalia watasambaa. Shahiri wananchi tuna butwaa! Vipi wenyeviti msitaharuki na kutoka na majibu hadharani?
Je, wananchi tumuulize Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini atupatie majibu? Poleni wenyeviti. Ujumbe huu uzingatiwe, usipuuzwe.
Watanzania wanataka mfumo wa vyama vingi vya siasa, vyenye tija na masilahi kwa taifa lao. Si kuwa na vyama vyenye visa na vitimbi kila uchao na kulifanya taifa kuwa hohehahe na shamba la wadhulumati kuvuna watakavyo. Watanzania wanahitaji sana demokrasia makini yenye mizizi ya utu, haki na ukweli.
Hapa nchini tunavyo vyama vya siasa vya aina mbili. Vyama vya siasa vya Demokrasia Jamii na vyama vya siasa vya Kijamaa. Chama Cha Mapinduzi ni miongoni mwa vyama vya Kijamaa. Kinapinga siasa za kibepari. Kinahimiza ujenzi wa Ujamaa na Kujitegemea (Azimio la Arusha). Kinazingatia maadili na miiko ya uongozi, imani na haki za mwanachama.
Vyama vingi vya upinzani nchini ni vya Demokrasia Jamii, kama vile ACT – Wazalendo na Chadema. Vinavyoamini mambo ya kijamii na kibepari. Utaratibu wa sasa duniani, vyama hivi vinakwepa mambo ya kijamaa (inasemekana ujamaa haupo!) na vinashabikia misingi ya kibeberu.
Mwenyekiti wa NCCR – Mageuzi, James Mbatia, anasema: “Upinzani wa kisiasa si uadui. Upinzani ni kujenga hoja na ushirikiano wa kitaifa. Tuweke masilahi pamoja kwa mama Tanzania. Si ubinafsi. Siasa haina formula. Tunahitaji maelewano, umoja na amani.”
Watanzania wenzangu, kuona ni mwalimu mzuri sana kumpita mwalimu kusikia. Uzuri wa mambo tunaona na tunasikia yanayofanyika katika vyama vyote hivyo vya siasa nchini. Wanaohama wanazo sababu. Watanzania tunataka mabadiliko na maendeleo ya watu na vitu. Tuwatafakari Wanasikinde.