Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Dar

“Nilikuwa Dodoma kwenye kazi za uandishi wa habari ghafla nikapigiwa simu na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kichangani, Kata ya Kinyerezi Wilaya ya Ilala kuwa nyumba yangu inapigwa mnada kwa sh.milioni 30 ili kufidia deni ya milioni 5.2 ambalo aliyekuwa mume wangu alikuwa akidaiwa.

Nyumba inayouzwa kwa sh.milioni 30 ili kufikia deni la sh.milioni 5.2

“Nilishtuka sana kwa kuwa sikujua kama bado alikuwa anadaiwa kwa kuwa hatuna mawasiliano naye na pia nataiwa kutoka ndani ya nyumba ndani ya siku 14 yaani kuanzia leo Desemba 5,2022 vinginevyo nitatolewa kinguvu” amesema mwandishi wa habari gazeti la Raia Mwema Mary Victor Mahundi.

Akizungumza na Jamhuri kwa uchungu Mary amesema kuwa taarifa za mumewe kudaiwa alikuwa nazo tangu mwaka 2017 kwani alichukua mkopo na dhamana aliandika nyumba bila ya yeye kumshirikisha na baada ya kupata mkopo alihama nyumba na kwenda kuishi kwingine na kumuacha na watoto.

“Taarifa za yeye kuchukua mkopo mimi ninazo lakini baada ya kupata mkopo huo yeye ( mumewe) alihama nyumba tangu mwaka 2017 na kwenda kuishi kwingine na mimi nilipata shida sana kuwalea watoto wangu kwani kulikuwa hakuna mtu wa kunisaidia kulipa ada za shule.

“Nilipokuwa nikimpigia simu alikuwa hapokei na nilipopata taarifa za kuchukua mkopo huo kupitia nyumba mwaka 2017 nilimtumia ujumbe wa kumsihi sana arejeshe mkopo wa watu kwani sitaki kupata shida nyingine na watoto wangu.

“Sikujua wapi anaishi kwa kuwa kila nikipiga simu hapokei kila siku nikaamua kumwandikia ujumbe mbalimbali na mwishowe aliamua kunijibu kuwa amechukua mkopo na anaendelea kurejesha hivyo hakuna sababu ya yeye kumsumbua wala kumkumbusha,” amesema.

Amesema kuwa cha kushangaza kuwa leo Desemba 5 amepigiwa simu kuwa nyumba yake inapigwa mnada ili kufidia deni la milioni 5.2 na wanatakiwa kutoka ndani ya nyumba.

Amesema kuwa baada ya taarifa hiyo amelazimika kurudi Dar es Salaam haraka ili kufanya taratibu za kusitishwa kwa uuzwaji wa nyumba hiyo.

“Hawa wauzaji wamenipa nakala ya barua ya taratibu za nyumba kupigwa mnada na nakala nyingine inaonyesha imekwenda katika ofisi ya mkuu wa wilaya na hata hivyo benki hiyo wamefuata taratibu nyingine zote inavyotakiwa.

“Nimewasiliana na Mkuu wa Wilaya ya Ilala kumuelezea hali ninayopitia kwa kuwa hii nyumba si ya mume wangu peke yake ni mali ya familia, yeye (mume) kwa sasa sijui anaishi wapi lakini sisi , tunatakiwa kuondoka ndani ya siku hizo 14 vinginevyo wamesema watatuletea mabaunsa na kututoa kwa nguvu.

“Niliwasiliana na DC Ilala ameniahidi kulifuatilia kwa karibu suala hili, hata hivyo ninawaomba wadau mbalimbali wanisaidie ikiwa ni pamoja na wanasheria ili kusimamishwa kwa uuzaji wa nyumba yangu kwa deni ambalo mume wangu ndiye anadaiwa.

“Ninaomba msaada wa kisheria ili kuweka zuio kabla ya mahakimu na majaji hawajakwenda likizo ya kufunga mwaka,” amesema Mary.