ALEXANDER GRAHAM BELL
Alivumbua simu lakini alikuwa mnyanyasaji mkubwa
Karibu katika safu hii mpya inayolenga kuangalia upande wa pili wa maisha ya watu maarufu ambao wamefanya mambo makubwa duniani. Kwa kawaida, watu hao hujulikana zaidi kwa mambo hayo makubwa waliyoyafanya.
Lakini kwa kuwa ni watu wa kawaida, walikuwa na maisha kama walivyo watu wengine, ambayo yalikuwa na mambo mengi. Lakini umaarufu wao unawakinga na kuwafanya watu wengi wasifahamu upande wa pili wa maisha yao ya kawaida na mambo waliyoyafanya nje ya umaarufu wao.
Safu hii inalenga kukufunulia kidogo maisha ya kawaida na vituko ambavyo baadhi ya watu maarufu duniani walivifanya.
Leo kwa kuanzia tuangalie maisha ya mtu anayeitwa Alexander Graham Bell. Huyu ni mwanasayansi maarufu sana duniani na umaarufu wake ulitokana na kugundua teknolojia ya simu.
Ukijaribu kufikiria iwapo simu hazitakuwepo duniani maisha yatakuwaje, unabaini kuwa kuna uwezekano mkubwa wa maisha kukoma. Kama si Bell, basi dunia isingekuwa hivi tunavyoijua leo.
Lakini, licha ya kuwa mwanasayansi maarufu ambaye alifanya uvumbuzi wa vitu kadhaa, katika maisha yake ya kawaida Bell alikuwa ni mnyanyasaji mkubwa wa walemavu. Anatambulika kama mtu ambaye aliongoza vikundi ambavyo vilikuwa vinawapinga watu waliokuwa wanatetea haki za walemavu wasiosikia.
Bell alikuwa miongoni mwa watu walioamini kuwa walemavu wanapaswa kutengwa ili wasije ‘kuwaambukiza’ watu wengine hali waliyokuwa nayo. Kwa mujibu wa Bell, walemavu wa kutosikia walikuwa ni tishio kubwa kwa kizazi cha watu wasio na ulemavu na katika shughuli zake alihakikisha kuwa watu hao wanatengwa.
Katika harakati zake kuna wakati alijaribu kuanzisha harakati za kutaka lugha za viziwi zipigwe marufuku, walimu wa viziwi wafukuzwe kazi na viziwi wapigwe marufuku kuoa au kuolewa.
Lakini jambo la kutisha zaidi ni kuwa Bell alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wanataka viziwi wahasiwe. Aliyashabikia haya yote ili kuhakikisha utamaduni wa kundi hili unafutwa kabisa.
Kwa maana hiyo, wakati katika maeneo mengine Bell anafahamika kama mtu maarufu ambaye amevumbua kifaa kilichogeuka kuwa moja ya nyenzo kubwa ya maendeleo duniani, lakini maisha yake yalikuwa na makandokando makubwa.
Hakika, iwapo watu wangetakiwa kupiga kura leo hii ya kupima heshima aliyopewa mwanasayansi huyo, haijulikani hali ingekuwa vipi, hasa pale watu watakapofahamu kiwango cha juu cha unyanyasaji alichokuwa nacho dhidi ya binadamu wenzake kwa sababu tu ya ulemavu wao.
Lakini hiyo haiondoi ukweli kuwa uvumbuzi wa simu uliofanywa na Bell ni moja kati ya mambo ambayo yameleta mabadiliko makubwa duniani na bado uvumbuzi huo utaendelea kuleta mabadiliko mengine makubwa zaidi. Kila mtu anatambua umuhimu wa simu katika maisha ya sasa.
Bell
Alexander Graham Bell alizaliwa Machi 3, 1847 na alifariki dunia Agosti 2, 1922. Alizaliwa Uskochi lakini ameishi Marekani ambako ndiko alikofanyia shughuli zake.
Pamoja na kuvumbua simu, Bell ni mmoja wa waanzilishi wa kampuni maarufu ya simu ya American Telephone and Telegraph Company (AT&T) iliyoanzishwa mwaka 1885.
Alifariki dunia kutokana na ugonjwa wa kisukari katika jumba lake la kifahari huko Cape Breton, Nova Scotia, akiwa na umri wa miaka 75.