Mabingwa mara 15 wa Ulaya, Real Madrid, wanakabiliwa na changamoto kubwa baada ya kupoteza mara tatu katika mechi tano za Ligi ya Mabingwa.

Baada ya kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Liverpool, wababe hao wa Uhispania wapo katika nafasi ya 24 kwenye jedwali, nafasi isiyozoeleka kwao.

Katika muundo mpya wa Ligi ya Mabingwa, timu nane bora hutinga hatua ya 16 moja kwa moja, huku nafasi za tisa hadi 24 zikilazimika kupambana kwenye hatua ya mtoano. Real Madrid, wakiwa nafasi ya 24, wanahitaji muujiza kujinasua kwenye hali hii tata.


Kylian Mbappe, aliyewasili kwa mbwembwe kubwa, bado hajapata makali yake ndani ya kikosi cha Real. Penalti aliyokosa dhidi ya Liverpool imeongeza shinikizo kwake, huku wachambuzi wakisema kuwa hakutoa kiwango kinachotakiwa katika mchezo huo muhimu.

“Hatujaona ubora wa Mbappe usiku wa leo,” alisema Steve McManaman. “Madrid walihitaji kung’aa lakini wachezaji wakubwa, akiwemo Mbappe, hawakuonyesha uwezo wao.”


Kutokuwepo kwa Vinicius Jr kutokana na jeraha kumeongeza changamoto kwa Mbappe, ambaye bado anatafuta nafasi yake bora katika timu hii yenye nyota wengi. Licha ya changamoto hizi, wachezaji wenzake wanakubali uwezo wake na wanaamini atarejea kwa kasi.

“Kylian anaweza kuweka kichwa chake juu,” alisema Jude Bellingham. “Najua atatoa mchango muhimu kwa klabu hii.”


Huku ikiwa na rekodi mbaya zaidi ya kupoteza mara tatu katika mechi tano, maswali yanaibuka kuhusu hatma ya Real Madrid katika shindano hili kubwa. Je, wanauwezo wa kugeuza matokeo haya na kurejea kuwa mabingwa wa kweli wa Ulaya?