ARUSHA
Na Mwandishi Wetu
Beki wa kimataifa wa Ufaransa na nyota wa zamani wa miamba wa soko wa Ligi Kuu ya England (EPL), Liverpool, Mamadou
Sakho, ameombwa na kukubali kuwa Balozi wa Hiari wa Utalii wa Tanzania.
Beki huyo wa kati mwenye urefu wa sentimita 187 ambaye kwa sasa anaichezea Klabu ya Crystal Palace inayoshiriki EPL, anasifika kwa aina yake ya uchezaji wa nguvu, uzuiaji na upigaji wa pasi za uhakika.
Sakho aliyekuja nchini kwa ziara binafsi ya utalii, amekubali ombi lililofikishwa kwake na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Betrita Lyimo, wakati nyota huyo akiwa katika Hifadhi ya Mamlaka ya Bonde la Ngorongoro mkoani Arusha, hivyo kulipa taifa heshima kubwa na nafasi ya kutambulika zaidi Ufaransa na katika Bara zima la Ulaya.
Raia huyo wa Ufaransa amewasili nchini Mei 26, mwaka huu, ratiba yake ikionyesha kuwa katika mapumziko ya siku 10, huku akiwa ameambatana na familia yake.
Mbali na Ngorongoro, familia hiyo ?ya kibalozi? wametembelea vivutio vingine kadhaa vya utalii kama Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Kijiji cha Wamasai cha Seneto na visiwa vya Zanzibar.
Baadaye Sakho na mkewe walitembelea Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutambulishwa kwa wabunge na Spika Job Ndugai wakati kikao cha 41 cha Bunge la Bajeti kilipokuwa kikiendelea jijini Dodoma.
Siku moja tu baada ya kuwasili kwake, taarifa zinasema, waandishi kadhaa wa habari kutoka moja ya vituo vya runinga vya Ufaransa, nao walikuja nchini kutengeneza makala maalumu za ziara yake.
Vipindi hivyo vitatumika kutangaza utalii wa Tanzania, hasa maeneo yote aliyoyatembelea, kwenye soko la utalii la Ufaransa.
Sakho, baba wa watoto wawili; Sienna na Aida Sakho, alizaliwa Februari 13, 1990 na akafunga ndoa na Majda Sakho mwaka 2012); ni mchezaji wa timu ya taifa ya soka ya Ufaransa huku kaka yake, Amadou Sakho, akiichezea Real Madrid ya Hispania.
Alianza kung?ara katika soka akiwa na FC kabla ya kujiunga na mfumo wa soka la vijana wa klabu maarufu ya Paris Saint-Germain (PSG) mwaka 2002.
Katika msimu wake wa kwanza kucheza Ligi Kuu ya Ufaransa Oktoba, 2007, akawa mwanasoka wa kwanza mwenye umri mdogo zaidi kuwa nahodha wa klabu inayoshiriki Ligue 1.
Aliichezea PSG mechi 200 na kushinda makombe yote manne ya ndani. Mwaka 2013 akanunuliwa na Liverpool kwa dau la pauni milioni 18.
Mwaka 2017 akaenda kwa mkopo kuchezea Crystal Palace kabla ya klabu hiyo kumnunua moja kwa moja kwa pauni milioni 26 Septemba 1, 2017.
Huyu ni mwanasoka wa kimataifa kweli kweli, akicheza na kupewa unahodha katika ngazi zote za timu za soka za vijana za Ufaransa.
Tangu alipocheza mechi ya kwanza ya timu ya wakubwa dhidi ya England mwaka 2010, Sakho amecheza zaidi ya mechi 25 na
kuiwakilisha Ufaransa kwenye fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2014.
Beki huyo mwenye nguvu hajaonekana uwanjani tangu Januari mwaka huu kutokana na kuwa majeruhi, lakini tayari amerejea mazoezini.
Hata hivyo, inaonekana kwamba kwa sasa si rahisi sana kwake kuwashawishi mabosi wa Crystal Palace kumuongezea mkataba, huku kukiwapo taarifa za mipango ya kumuuza mara mkataba wake utakapomalizika mwezi huu.
Huenda akawa mmoja wa wachezaji wengi watakaoondoka klabuni hapo katika kipindi hiki cha usajili.
Palace wanaripotiwa kuwa na walau wachezaji 11 ambao mikataba yao inamalizika mwisho wa mwezi huu, huku klabu ikiwa kimya kuhusu mustakabali wao na Hocha Roy Hodgson akimsukumia mzigo Mkurugenzi wa klabu, Dougie Freedman.
Tanzania kwa miaka mingi imekuwa ikipokea wanamichezo na watu mashuhuri kutoka mataifa mbalimbali duniani wanaokuja na familia zao kutembelea vivutio vya utalii, hasa hifadhi za taifa zilizopo kaskazini.
TTB wanashauriwa kuichukulia hii kama fursa adhimu na kuendelea kuwashirikisha kutangaza utalii wa Tanzania, hasa wenye wafuasi wengi kwenye mitandao yao ya kijamii ambayo ni nyenzo muhimu yenye kufikisha ujumbe kwa watu wengi ndani ya muda mfupi.
Sakho ana wafuasi zaidi ya milioni moja kwenye ukurasa wake wa Instagram.