“… ingawa kwa nadharia muundo wa Chama chetu (akimaanisha CCM) ni wa kidemokrasia, lakini katika vitendo hatuonyeshi demokrasia wakati wote na kwa shughuli zetu zote.”
Maneno haya ni ya Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambayo ni sehemu ya wosia wake wa kuitaka CCM ijenge dhana ya kuonesha demokrasia ya kweli kwa vitendo.
Ebadi: Tuheshimu haki za binadamu
“Natumaini mfano wa Saddam Hussein utawapa somo viongozi wa nchi nyingine ambako haki za binadamu haziheshimiwi.”
Haya ni maneno ya mwanasheria, mwanaharakati na mwasisi wa watetezi wa haki za binadamu wa nchini Iran, Shirin Ebadi, aliyezaliwa Juni 21, 1947 huko Hamedan. Saddam Hussein alikuwa Rais wa Iraq mwaka 1979 – 2003, aliuawa kwa kunyongwa Desemba 30, 2006 mjini Baghdad, Iraq.
Cuomo: Matishio ya kweli duniani
“Naamini ongezeko la joto duniani na mabadiliko ya hali ya hewa ni matishio ya kweli kwa sayari yetu.”
Gavana 56 wa New York – Marekani, Andrew Cuomo, alitoa kauli hii kuhimiza jamii kukabiliana na matishio hayo ikiwa ni pamoja na kuepuka utengenezaji silaha zinazochangia uchafuzi wa mazingira. Alizaliwa Desemba 6, 1957 huko Queens.
Sheikh Wajed: Lazima tuokoe mito
“Lazima tuokoe mito yetu. Pamoja na ugumu utakaokuwapo, kugharimu muda na mradi wenyewe ni changamoto, lakini tutatekeleza hilo. Kwa gharama yoyote tutafanya kazi hiyo.”
Haya yamesemwa na Waziri Mkuu wa Bangladesh, Sheikh Hasina Wajed, katika maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, mwaka huu. Alizaliwa Septemba 28, 1947 mjini Tungipara Upazila.