“Ugonjwa huu sitapona Watanzania watalia Nitawaombea kwa Mungu”

MIAKA 13 iliyopita Taifa la Tanzania liligubikwa na majonzi  mazito kutokana na kifo cha mwasisi wake, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mwalimu Nyerere alifariki dunia Alhamisi saa 4:30 asubuhi kutokana na maradhi ya saratani ya damu katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas (St. Thomas Hospital) mjini London, Uingereza.


Watanzania na wapenda demokrasia ya kweli, wamo kwenye kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa kutokana na mchango wake mkubwa alioutoa katika kupigania Uhuru na ukombozi wa Taifa letu na nchi za Bara la Afrika zilizokuwa zikitawaliwa na wakoloni.


Watanzania wanakumbuka juhudi zake za kujenga Umoja na Mshikamano wa Taifa kwa kuhimiza utu, upendo, haki na usawa, pamoja na kupiga vita ubaguzi wa aina zote, unyonyaji, ukabila na udini.


Nami mwandishi wa makala hii naungana na Watanzania wenzangu katika kumbukumbu hii. Mtanzania mwenzagu, utakubaliana na mimi kwamba tunapoadhimisha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kwa kweli tunaangalia matendo mema aliyotenda enzi za uhai wake na kutafakari kauli zake iwapo yanaendelezwa na kudumishwa au yameachwa.

 

Ni kweli mara chache watu huzungumza mabaya ya hayati ingawa kufanya hivyo huonwa kama chuki, na si utu. Ndiyo maana yataka moyo kuweka mambo kama haya bayana. Lakini tukumbuke kuwa mchango wa busara huwa mgumu kufunguka kupitisha fikra hiyo.


Nianze kwa kusema kuwa kifo ni tukio ambalo kila nafsi ya binadamu itaonja. Ni tendo kongwe duniani, lakini hakizoeleki. Kinapotokea, iwe kwenye familia, koo, kabila au hata kwenye jamii kwa maana ya Taifa hutia mtikisiko usio kifani na kuumba sura ya majonzi na mfarakano wa aina yake miongoni mwa binadamu.


Kiumbe kipi asiyesitushwa na kifo? Makala hii inakumbusha baadhi ya kauli na matendo maridhawa ya hayati Mwalimu Nyerere aliyopata kutamka enzi za uhai na uongozi wake katika Taifa hili, iwe katika uchumi, siasa au masuala ya jamii.


Naomba tuelewane tangu na mapema kuwa kauli zilizomo humu ni baadhi tu. Kwani kauli na vitendo vyake kama ningeweka hapa ningehitaji magazeti yote nchini na bado yasingetosha kunakili mambo hayo.


Mwalimu Nyerere ametuwekea na ametuachia misingi madhubuti ya kuifuata na na kuitunza katika kudumisha umoja na mshikamano wa Taifa letu; umoja ambao hauna budi kuhimilishwa kwa mizizi watu, haki, upendo, amani na mshikamano.


Inapokosekana mizizi hiyo ni muhali mno kuondoa maadui ujinga, umasikini na maradhi ambayo ni mafisadi wakubwa wanaobomoa juhudi zetu za kuendeleza maendeleo na kudumisha umoja wetu.


Mwalimu Nyerere mara kadhaa aliimba neno “Umoja” kama bohari ya kutunza vikolombwezo vyote vya kisiasa, kiuchumi, na kijamii, yeye akiwa ni mboharia na mlinzi mkuu wa umoja huo. Kuondoaka kwake duniani, Watazania tunayumba! Hili halina kigagaziko kutamka wala ubishi kukanusha.


Hebu angalia nembo ya Taifa letu. Kwa makini utaona nanga ya nembo hiyo ina maneno UHURU NA UMOJA. Maneno hayo hayakuwekwa kama mapambo. Ni somo linalokumbusha wajibu wako kwa Taifa.


Kwanza ukiwa kama kiongozi fahamu kwamba uongozi wako unatokana na watu, wala si wanyama, ndege, wadudu. Pili, mamlaka yako ya uongozi itoe uhuru kwa wananchi waliokuchagua kutoa mawazo yao ya kuendeleza uhuru na umoja wao. Tatu, wewe mwanachi una wajibu wa kutii mamlaka iliyopo madarakani bila shuruti.


Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitambua maana ya nembo hiyo. Alithamini Taifa lake na kutambua dhamana ya uongozi mbele ya Watanzania, hii inatokana na ukweli kwamba asili ya uongozi wetu ni WATU na HAKI.

 

Uongozi wetu unatokana na watu kwa maana ya kuchaguliwa kutoka mwenyekiti wa kitongoji hadi rais wa nchi chini ya mfumo wa demokrasia ya Tanzania ambao uongozi wake haupaswi kuwa na vimelea vya hongo au rushwa, vitisho, ubabe wala upendeleo, au ujanja ujanja.


Wakati tunamuenzi Mwalimu, viongozi mbalimbali katika kipindi hiki cha miaka 13 ya kutokuwa naye kweli mnatokana na watu? Mbona hivi majuzi tu tumeshuhudia au tumefahamishwa hali ya mshike mshike na vurumai za uchaguzi mbalimbali?


Kuanzia vyama vya siasa hadi serikalini, jinsi viongozi wanavyochaguliwa, je, tuendeleze utamaduni huo wa kuzozana na kukashifiana? Haki inatokana na watu wenyewe katika kuweka stahiki zao za mgao, malipo au ada ambayo wamejiwekea kutokana na misingi ya kisheria au kanuni ndani ya jamii.


Leo baadhi ya malipo hutokana kwa mbinde na masharti ingawa vyombo vya kufuatilia haki vipo, lakini vinalaumiwa kutenda kinyume chake. Vipi unadiriki kutamka hadharani kwamba unamuenzi Baba wa Taifa kwa kudumisha umoja na haki ilhali Watanzania wanalia na kusaga meno? Moyo wa Muungano gani usioweza kuweka simanzi katika hayo?


Hapo awali nilisema Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ametamka na kutenda mengi kwa Watanzania kuhusu umoja na amani, hebu nidokoe kidogo. Novemba 14, 1965 Mwalimu Nyerere alifungua mkutanao mkuu wa kwanza wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) Jijini Dar es Salaam. Katika mkutano huo Baba wa Taifa aliwahusia wanawake wote umuhimu wa kuwa na umoja na serikali yake ilivyokuwa inajitahidi kuondoa tofauti zilizokuwapo miongoni mwa wananchi.

 

Namnukuu, “Tunayo mazoea viongozi. Sisi viongozi wetu tuliozoea tangu mwaka 1954 ni viongozi katika kupingana na makundi, sasa ninachowaonya kina mama na viongozi wote wa Tanzania, nawaomba lazima kama nchi imegeuka, nchi hii ina umoja.


Hakuna hata moja katika Afrika ina umoja kuzidi Tanzania. Hakuna hata moja. Anayejua nchi moja katika Afrika yenye umoja wa hiyari zaidi kuliko ya Tanzania aniambie. Ziko nchi zina umoja wa bunduki. Hapa bunduki ziko wapi? Tanzania ina umoja. Watu wanasikilizana. Watu wanakuja wanashangaa. Kitu kimoja kinachoshangaza dunia ni umoja. Ndicho tulicho nacho vingine hatuna”. Mwisho wa kunukuu.


Ni miaka 47 sasa tangu kauli hiyo itolewe. Je, wangapi leo tunaijali na kuienzi kauli hiyo? Mbona vurugu zinatokea kila pembe ya nchi na tunafanya kinyume chake? Ni vema viongozi wa sasa mchunge ndimi zenu. Viongozi wa Serikali muache purukushani katika madai ya kweli na hoja za msingi zinazotolewa na wananchi.

 

Vyombo vya dola mkumbuke “moyo kabla ya silaha”. Na vyombo vya habari mjitambue ni watu mbele ya silaha. Hivi sasa nchi imo kwenye dalili ya kuzamishwa ndani ya dimbwi la uhasama kutokana na baadhi ya kauli za viongozi wa vyama vya siasa zenye mwelekeo wa kuvunja umoja. Kwa mfano, “Msichague fulani ni fisadi, si mwenzetu, hatuondoki hapa kituoni mpaka kieleweke, tutahakikisha nchi haitawaliki, na liwalo na liwe tumechoka.”

 

Lugha kama hii kweli zinamuenzi Baba wa Taifa au zinampuuza kwa zile juhudi zake za kuhimiza umoja? Wanafalsafa wetu mahiri, weledi na mshauri maarufu wa lugha yetu ya Kiswahili hapa nchini hata Afrika Mashariki, marehemu Sheikh Shabani Robert alipata kunena maneno yafuatayo:


“Ulimi hulainisha, neno likafurahisha, ni furaha ya maisha kila wakati tumia. Ulimi wa pilipili hutenga watu wawili, kuishi mbalimbali, hii hasara sikia. Ulimi uliotamu, hupenda wanadamu, cheka na tabasamu, unalosema hupewa. Hupendeza wasikizi, wakati wa maongezi, hili ni jambo uzizi, wajibu kuliania. Ulimi nzuri mali, huvuta walio mbali, kusikiliza kauli, namna unavyotoa.”


Hapo mwanzoni nimesema kuhusu mshike mshike na vurumai za uchaguzi mbalimbali iwe ndani ya chama cha siasa au serikali. Sote ni mashuhuda kwa yanayotokea. Kwa sura ya nje wagombea uongozi wanahitaji ridhaa ya kuongoza kuleta maendeleo. Kwa sura ya mioyo wanataka nafasi ya kufanya mambo binafsi kwa malengo binafsi.

 

Kwa wao, ndani ya chama ni ubarakala na madaraka. Serikalini ni  ubwana na utajiri. Tunashuhudia vikumbo vya watu katika kugombea kuwa mwenyekiti wa ngazi fulani ndani ya chama. Wajumbe wa vikao vya chama na kutumia vikao hivyo kwa masilahi binafsi pia ni vichaka vya kuficha maovu yao. Huko serikalini kila msomi na mwenye visenti anataka kwenda Ikulu akafanye biashara na kuanzisha mifuko ya fedha ya hisani.

 

Majimboni vikumbo vya kutaka kuwa mbunge apate kujaza mifukoni mapesa kwa kuhudhuria tu vikao vya Bunge, vya kamati na vya bodi fulani. Kwenye halmashauri za majiji, miji na wilaya apate posho za vikao kuidhinisha mikataba feki ya utoaji na uuzaji wa viwanja vya makazi na maeneo ya wazi yaliyotengwa kwa michezo na mikutano. Ukweli vyote hivyo kimsingi ni rushwa.


Leo, sina hakika wapo wana-TANU wangapi. Wao walikuwa na ahadi zao 10 za wana –TANU. Kati ya ahadi hizo, ahadi ya nne ilisema, “Rushwa ni adui wa haki, sitapokea au kutoa rushwa”. Ahadi hiyo walirithishwa wana CCM, inasema “Rushwa ni adui wa haki sitatoa wala kupokea ruishwa”.


Kwa mantiki hiyo, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mnamo Machi 13, 1995 jijini Dar es Salaam akiwafahamisha waandishi wa habari jinsi TANU ilivyopambana na rushwa na kuwajuza rushwa ilivyokithiri nchini.


“Sasa Tanzania inanuka rushwa. Ufa mwingine tuliopata. Tunataka kiongozi anayejua hivyo ambaye atasema rushwa kwangu mwiko. Mwaminifu kabisa kabisa hawezi kugusa rushwa na wanajua rushwa”. Mwisho wa kunukuu.


Si hayo tu. Katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa ajili ya mwaka 2010-2015 ibara ya 189 kuhusu mapambano dhidi ya rushwa inasema, “Rushwa ni kikwazo cha maendeleo ya Taifa na utoaji wa haki nchini. Isipodhibitiwa kwa dhati uovu unaotendwa na watoaji na wapokeaji rushwa unaweza kuenea katika sekta zote za maisha ya jamii na kusababisha mmomonyoko mkubwa wa uwajibikaji na maadili ya uongozi.”


Ibara ya 190 nayo inasema, “Ili kukomesha madhara ya rushwa, Chama Cha Mapinduzi katika kipindi hiki cha 2010-2015 kitaitaka Serikali kuimarisha na kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa.” mwisho wa kunukuu.


Nimechukua Ilani ya CCM tu kwa sababu ndicho kilichopo madarakani. Ndicho chenye dhana naya kuongoza na kusimamia uhai wa umoja na haki ya wananchi wa Tanzania. Je, wana CCM hebu mjiulize kweli tuhuma zote hizi zinazoelekezwa kwenu hazina vimelea vya rushwa? Kama vipo, kweli ndiyo mnamuenzi Baba wa Taifa, muasisi wa chama na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM- Mwalimu Julius Kambarage Nyerere?


Na ninyi mlio nje ya CCM, mnaolindwa na ulinzi wa Serikali ya CCM, mnaofaidi haki na maendeleo ya utawala wa CCM, na mnaokebehi au kusifu sera za CCM, kweli mnamuenzi Baba wa Taifa aliyeasisi Taifa hili lenye umoja, amani na mshikamano?


Kumbukumbu zangu zinanirudisha nyuma hadi mwaka 1992. Tanzania ilianza kutazama upya umuhimu wa siasa kutoka chama kimoja cha siasa na kuingia katika mfumo wa vyama vingi. Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikubali mapendekezo ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa kuhusu kuanzishwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini. Katika Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM Taifa uliofanyika Dar es Salaam, Mwalimu alisema yafuatayo. Nanukuu.


“CCM si chombo kinachozama ambacho baadhi ya watu waliomo walitaka kukimbia wasizame nacho. CCM ni chama chenye nguvu na kama Tume ya Rais ilivyobainisha wananchi wengi wangependa tuendelee na utaratibu huu wa chama kimoja chini ya CCM.


“Ndiyo maana mimi kwa upande wangu napenda mageuzi hayo yafanyike hivi sasa. Maana kila mageuzi makubwa huhitaji kiongozi mwenye uwezo na anayeaminiwa na wananchi. CCM ni kiongozi mwenye uwezo huo na anaaminiwa na wananchi. Mageuzi haya hayana budi kusimamiwa na kuongozwa na CCM yenye umoja, nguvu na mshikamano. Ndugu wananchi, ndugu wajumbe naomba mniamini katika hilo. Nalisema na kuliamini kwa dhati ya moyo wangu.


Lakini naomba mniamini pia katika hili lifuatalo: Najua wako watu wanaodhani kuwa vyama vya siasa ni vyama vya uhasama. Matumaini yangu ni kuomba watu hawa hawamo ndani ya CCM. Basi tufanye kitendo ambacho kitawasaidia au kutufanya sisi tuwafanane.


Kwanini tugombane na kutukanana, ni kweli kwamba sasa tutalazimika kuzielewa tofauti zetu waziwazi zaidi na hadharani ili wananchi waweze kuzielewa. Hilo ni jambo la kawaida katika mfumo wa demokrasia wa vyama vingi. Lakini si ajabu ya kutugombanisha.” Mwisho wa kunukuu.


Kwa maelezo hayo na wosia wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere viongozi na wananchi wa vyama vya siasa, hasa vyama vya upinzani kuna sababu ya kutukanana na kugomabana hata kuumizana na kuuana katika mikutano yetu? Ndiyo tunamuenzi Mwalimu hivyo? Ikumbukwe kwamba katika mkutano huo watu mbalimbali walioalikwa walihudhuria akiwamo John Cheyo ambaye hivi sasa ni Mwenyekiti wa United Democratic Party (UDP) na Mbunge wa Bariadi Mashariki.


Wakati wa kuomboleza kifo cha Mwalimu Nyerere mnamo Oktoba 15, 1999 Cheyo alisema, namnukuu. “Nilikuwa kwenye mkutano huo wa 1992 kama mtu wa kukaribishwa kama viongozi wa vyama vya siasa nayo ni kwanza kuamini kwamba amani ambayo msingi wake ni mwalimu.


Amani hii ni ya watanzania wote na sisi ambao tuna nafasi ya uongozi tuna dhima kubwa ya kumuenzi Mwalimu na pia  kuhakikisha kwamba mfumo huu wa amani unaendelea katika Taifa letu.


Kwa hiyo, njia mojawapo ni kuhakikisha kwamba tunaamani na kuongeza nguvu katika mabaraza ya uamuzi. Awali, nilisema leo tuadhimishe kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kujiuliza tangu atutoke, viongozi na wananchi kweli tunamuenzi? Najaribu kuangalia kauli mbalimbali za viongozi wa siasa na serikali, wananchi ndugu na marafiki wa Julius Kambarage Nyerere.


Mmoja kati ya marafiki wapenzi wa Mwalimu Nyerere ni Mheshimiwa George Kahama ambaye aliwahi kuwa waziri, balozi na kushika nyadhifa mbalimbali hapa nchini. Wakati wa maombolezo ya kifo cha Mwalimu, mnamo Oktoba 16, 1999 Mheshimiwa Kahama alisema, namnukuu;


“Ametuwekea misingi ya kupenda utu, ametuwekea msingi wa kupendana, ametuwekea msingi wa kutokuwa na ukabila, kuwa na ubaguzi wa rangi, kuwa na ugomvi wa dini. Sasa miongozo yote tukiifuata nadhani hakutakuwa na chochote kulifanya Taifa tukatetereka.” mwisho wa kunukuu.


Katika kipindi hicho cha maombolezo, aliyekuwa kiongozi wa chama cha waasi cha DRC Kisangani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Profesa Ernest Wamba Dia Wamba mnamo Oktoba 17, 1999 alisema kuhusu Mwalimu, nanukuu; “Alikuwa mtu mwenye busara, utu na juhudi za kuleta maendeleo barani Afrika.

 

Na si tu katika hilo, bali pia alijitolea kwa hali na mali kumuenzi mtu wa kawaida kutanzua matatizo yake, na suala la madeni sugu kwa nchi masikini. Wasiwasi uliopo ni kwamba hatuelewi kama atapatikana mtu atakayeziba pengo lake na kama misingi aliyoacha itaendelezwa.” Mwisho wa kunukuu.


Bwana Joseph Butiku aliyekuwa msaidizi wa karibu wa Mwalimu Nyerere ambaye wakati wa mazishi ndiye alikuwa msemaji mkuu wa familia, mnamo siku ya Jumapili Oktoba 17, 1999 alisema yafuatayo, namnukuu; “Mwalimu alikuwa ni kiongozi hodari. Mtu mnyenyekevu mwenye mapenzi makubwa kwa watu wote. Tuendeleze yale aliyoyasimamia. Mpenda amani ndiyo maana nchi hii ilipata uhuru kwa amani na aliendelea kupigania amani kwa misingi ya haki.” Mwisho wa kumnukuu.


Nimalizie maelezo yangu kwa kuwanukuu watu wawili. Ndugu yangu mwandishi wa habari na mhariri mweledi wa miaka nenda rudi, Ahmed Rajab, alipotoa mtazamo wake baada ya kuulizwa na mtangazaji/mwanahabari mwenzake mnamo Oktoba 14, 1999 huko London, Uingereza.


Swali: Unaangaliaje nini kitatokea baada ya kifo hiki cha Mwalimu ndani nchini Tanzania, tukizingatia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar?”  Mhariri wangu Ahmed Rajab alijibu, “Nifikiri kwamba kwa muda mfupi Tanzania itakuwa katika huzuni, itagubikwa na huzuni, lakini baada ya hapo kutakuwa na mvutano mkubwa.

 

Kwanza ndani ya CCM yenyewe kwa sababu tukumbuke kwamba ingelikuwa si mwalimu Nyerere leo Tanzania, Rais asingelikuwa Bwana Mkapa, pili kinafahamika kwamba kuwa hizi tetesi ya kuwa Rais wa Zanzibar Dk. Salimin Amour anataka kubadili katiba na Mwalimu Nyerere hayuko tayari. Sasa hayako mengi yanaweza kutokea. Nabashiri huu muungano utakuwa wa aina nyingine ikiwa utakuwapo.”


Mtu wa mwisho ni kaka yangu kiongozi, bosi wangu na Rais wangu wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa alipowafahamisha Watanzania kifo cha Mwalimu mnamo Oktoba 14, 1999, alisema, namnukuu; “Nawaomba wananchi mniamini kuwa Mwalimu alifanikiwa kuweka misingi imara na endelevu katika maeneo hayo yote.

 

Sisi tuliorithishwa Umoja na Muungano huo tuliapa kuuenzi na kuuendeleza. Nawaomba wananchi tushirikiane kumpa heshima stahiki Baba wa Taifa kwa kuzingatia wosia na kazi yake, utumishi wake na upendo wake”. Mwisho wa kunukuu.


Kwa nukuu zote hizo za kauli mbalimbali za viongozi ulizopata kuzisikia kabla na baada ya kafariki dunia Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, zinakupa uhalisia kuhusu tendo la kumuenzi. Je, ni kweli tunamuenzi Mwalimu? Kwa vipi?

Umoja na Amani na Mshikamano

Mungu Ibariki Tanzania

Mwandishi wa makala hii, Angalieni Mpendu ni mmoja wa wanahabari wakongwe nchini, akiwa mmoja wa watangazaji mahiri waliowahi kufanya kazi katika Redio Tanzania Dar es Salaam. Kwa sasa amestaafu na anajishughulisha na shughuli binafsi. Anapatikana kwa simu: 0787113542/0717113542.